TRA

TRA

Tuesday, December 29, 2015

Tuanzishe Kampeni ya Reading Books Everywhere

No comments:



Julian Msacky
OKTOBA 15, mwaka huu nilikuwa nazungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashir Ali kuhusu umuhimu wa watu kupenda kusoma vitabu.
Wakati tukiwa katika mazungumzo yaliyotokana na makala yake aliyoandika kuhusu Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Ali alifunga mjadala wa mazungumzo kwa kusema maneno yafuatayo:
"Ahsante. Tusichoke kupiga kelele kwani kazi ya kujenga taifa haiwezi kukamilika ikiwa tutashindwa kujenga utamaduni wa kupenda kusoma vitabu na magazeti yenye maarifa na
taarifa kuhusu mapambano ya ukombozi wa taifa letu na watu wake"
Ni ukweli usiofichika kuwa kama tunataka kujenga taifa la watu wenye uelewa mpana (wide scope) wa mambo ni lazima tuhimize watoto wetu kusoma vitabu.
Lakini pia, kazi hiyo haitafanikiwa vizuri kama sisi wenyewe (wazazi na walimu) hatutakuwa na utamaduni huo.
Ili kufanikisha hilo nilimshauri Dk Ali tuanzishe Kampeni ya Reading Books Everywhere.
Hii ikiwa na maana kila tutakapokuwa tuwe na kitabu cha kujifunza jambo lolote ili kushibisha ubongo wetu maarifa ambayo yatakuwa mtaji mzuri kwa taifa letu.
Unapojenga taifa la watu wanaosoma vitabu maana yake hata shughuli wanazofanya zitakuwa na mabadiliko makubwa. Watazifanya kitaalamu zaidi.
Na hili la mwisho ni changamoto kubwa inayotukabili kama taifa. Mambo yetu mengi hayafanikiwi kwa sababu hatupendi kusoma vitabu.
Matokeo yake vichwa vyetu tunajaza mambo ya ovyo ovyo ambayo hayatusaidii. Kwa maana hiyo tukianzisha kampeni hiyo ni imani yangu taifa letu litabadilika katika mambo mengi.
Tutajenga mijadala yenye afya tunapojadili masuala muhimu yanayogusa ustawi wa nchi na watu wake. Si hivyo tu.
Hata mikataba tutakayoingia kati ya nchi wahisani itafanyika kwa uangalifu mkubwa tofauti na sasa kwa sababu bongo zetu zitafanya kazi vizuri.
Kampeni hiyo ni lazima iende pamoja na kuhakikisha shule zetu zina vitabu vya kutosha. Si bora vitabu tu, bali vikidhi viwango vya kutumiwa katika shule zetu.
Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha vitabu vyetu haviwachanganyi watoto au kuwaondoa kwenye reli.
Wote tunafahamu kuwa kabla ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) haijavunjika mwaka 1977, Tanzania, Uganda na Kenya walikuwa wanatumia vitabu vya aina moja.
Kulikuwa na vitabu vinafahamika kama East Africa Book One, Two, Three, Four, Five na Six. Vilikuwa vya kumjenga mwanafunzi kufahamu kwa usahihi Lugha ya Kiingereza.
Ni ukweli usiofichika kuwa watu wengi waliosoma vitabu hivyo miaka hiyo wanazungumza vizuri Kiingereza bila tatizo lolote pamoja na Kiswahili.
Kwa kusema hivi sina maana kuwa Kiswahili tukiweke pembeni hapana.
Hapa nina lengo la kuhakikisha tunasoma vitabu vya aina mbalimbali ili vitusaidie kupanua wigo wetu kama Watanzania kwa ustawi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Kwa kufanya hivyo maana yake mfugaji atasoma kitabu kinachohusu masuala ya ufugaji.
Akifanya hivyo kitamsaidia kufuga kisasa na kuachana na mfumo wa kienyeji ambao unasababisha hasara kubwa kuliko faida.
Hii ina maana kuwa si lazima kuwa na mifugo mingi ndipo uwe tajiri. Unaweza kuwa na ng'ombe 20 na ukafugaji kitaalamu na kupata faida lukuki na kuepuka uharibifu wa mazingira.

Ufugaji wa aina hiyo unamsaidia mfugaji kuacha kutangatanga na mifugo.Tunapofuga kitaalamu kuna faida nyingi.
Kwanza tunakuwa tumejiajiri, lakini pia tunakuwa  na kipato cha uhakika kwa ajili ya familia zetu. Mfumo huo wa ufugaji unakwenda sanjari na kulima kitaalamu.
Ilivyo sasa tunalima kwa mazao ili mradi siku ziende. Kwa maana hiyo usomaji wa vitabu utatusaidia mambo mengi. Ndiyo maana ninasisitiza kampeni hiyo.
Kwa kufanya hivyo maana yake tutakuwa na uelewa mzuri hata wa chimbuko la dini zetu (Ukristo na Uislamu) na namna gani tuziendeshe katika jamii yetu.
Jamii isiyo na maarifa ni sawa na jamii iliyo gizani. Tunataka tuondoke kwenye giza hilo kwa kusoma vitabu.
Tukisoma vitabu kwa kina ikiwa ni pamoja na kupitia katiba za mataifa mengine jamii itakuwa na upeo mpana kuandaa katiba inayokidhi kiu ya wengi.
Hata tunapokataa katiba hii na ile tutakuwa na hoja za kutosheleza badala ya kudandia hoja za wengine. Faida za kusoma vitabu ni nyingi.
Wakati ninaandika makala haya nilipofungua intaneti nilikutana na jambo linahusu mada hii ya kusoma vitabu. Nilikutana na watu waliosoma vitabu vingi kwa mwaka huu.
Wengine wamesoma vitabu 25. Miongoni mwa vitabu ambavyo Watanzania wenzetu wamefanikiwa kusoma ni pamoja na 
The truth shall make you free- Gustavo Gutiérrez.
Kwa maana Ukweli Utawaweka Huru. Sowing the mastard seed cha Yoweri Museven, The 21 Irrefutable Laws of Leadership cha John C. Maxwell, Hisa, Akiba na Uwekezaji cha Emilian Busara, YES, In My Life Time cha Profesa Haroub Othman na vingine vingi.
Kuna umuhimu wa kubadilika na kuanza kusoma vitabu ambavyo ni nyenzo muhimu kwa kizazi hiki hasa tunapozungumzia dhana ya sayansi na teknolojia.
Tusikubali kuwa maskini wa fikra. Tutafute mitaji kwa kusoma vitabu. Tuwaige wenzetu wa dunia ya kwanza ambao wakiwa wanasafiri wanatembea na vitabu.
Badala ya kupotezea fikra zetu zote kwenye Facebook, Instram, Twitter, WhatSap na mitandao mingine ya kijamii, tuvikumbuke pia vitabu ambavyo vina maarifa lukuki.
Mitandao hiyo inatudumaza kifikra na kiakili. Hebu tubadilike kwa sababu hata waasisi (founders) wa hiyo mitandao hawaipi nafasi kwa kiwango hicho.
Kama kweli walikuwa wanaipa nafasi, wasingesafiri na vitabu wanapokuwa safarini.
Wasomi na waandishi wa habari wawe mstari wa mbele kupigania kampeni hiyo ili kujenga taifa la watu wanaopenda kusoma vitabu.
Kwa kufanya hivyo ile dhana kwamba ukitaka kumficha Mtanzania jambo liweke kwenye maandishi, litakwisha kwa vile wanasoma vitabu ambavyo vina hazina ya mambo mengi mazuri.
msackyj@yahoo.co.uk, 0718981221

Fedha kuokoa vifo vya Wajawazito na Watoto nchini

No comments:



pix 1
Mwenyekiti  wa Jumuiya  wa Makanisa ya Pentekoste,(Katikati)  ambaye pia ni Askofu wa Huduma ya Tanzania Fellowship Churches (TFC), Askofu  Godfrey  Malassy  alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam.
Na  Skolastika Tweneshe-MAELEZO
Fedha zitakazopatikana katika Tamasha la mkesha wa kuombea amani  nchini zitatumika kuwasaidia watu wenye mahitaji  hasa afya ya mama na mtoto.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti  wa Jumuiya  wa Makanisa ya Pentekoste , ambaye pia ni Askofu wa huduma ya Tanzania Fellowship Churches (TFC), Askofu  Godfrey  Malassy  alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Malassy alisema kwamba, fedha zitakazopatikana katika tamasha hilo zitanunua vifaa vinavyotumia nishati ya jua (solar Panels) ili kuwasaidi wamama wajawazito na watoto wanaozaliwa.
“Kina mama wajawazito na watoto wanakufa mahospitalini kutokana  na kukosa umeme hasa vijijini,  hivyo tumeamua fedha zitakazopatikana mkesha huu tutanunua solar” alisema Malassy
Aidha Askofu Malassy  amewaomba wananchi   kuzidi kumuombea Rais John Magufuli katika kuliongoza Taifa la Tanzania ili aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi ambayo tayari imekubalika ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti huyo alitambulisha kitabu  kiitwacho IJUE  SIRI YA AMANI  KWA  TAIFA ambacho kinauzwa Sh.5000 amesema kuwa  kitabu hicho kina lengo la kuelimisha thamani na jukumu la watanzania kuilinda Amani  bila kujali itikadi za  dini, siasa wala ukabila
Pia ameomba kwa atakaeguswa na  matatizo yanayowakumba wamama wajawazito anaweza kutuma mchango wake kwa namba zifuatazo 0755202204, 0719202204, 0684202204.
Mkesha huo  ni wa 18 tangu uanze kufanyika  na mwaka huu utafanyika  katika Uwanja wa Uhuru usiku wa tarehe 31 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Awamu ya Tano Mhe.  John Pombe Magufuli.
pix 2
Wachungaji mbalimbali wa Makanisa ya Pentekoste wakiwa katika mkutano na Waandishi wa Habari kwaajili ya kuzungumzia mkesha utakaofanyika Desemba 31.
pix 3
 Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mwenyekiti  wa Jumuiya  ya Makanisa ya Pentekoste, (Hayupo pichani)  ambaye pia ni Askofu wa huduma ya Tanzania Fellowship Churches (TFC), Askofu  Godfrey  Malassy  alipokuwa akizungumza leo Jijini Dar es salaam. Picha zote  na Ally Daud MAELEZO.(P.T)

WAFANYAKAZI SABA WA TPA WASHIKIRIWA NA JESHI LA POLISI KUHUSIANA NA UPOTEVU WA MAKONTENA MPYA 11,884 NA MAGARI 2,019

No comments:

Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
 Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii
BAADA ya  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  kufanya ziara  katika Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) na kubaini uondoshwaji wa wa kontena 329  ambazo ziliondoshwa bila kulipa kodi zaidi ya sh.bilioni 12, baada ya ziara hiyo Mawakala wa Forodha walifanya ukaguzi  kuona kama kuna upotevu wa mapato  na kubaini jumla ya kontena 11,884 na magari 2019 yalitolewa bila malipo.

Makontena hayoo yalitolewa katika bandari kavu ni MOFED 61,DICD 491, JEFAG 1, 450, AZAM 295, PMM  779, AMI 4384, TRH 4,424 ambazo kodi yake ni zaidi ya sh.bilioni 47.

Magari 2019 yalitolewa bila kulipa kodi katika kampuni za  TALL 309, CHICASA 65, FARION 18, SLVER 97, MASS 171, HESU 1359 kodi yenye thamani zaidi y Tsh.bilioni moja (1) .

Akizungumza na wafanyakazi wa Bandari leo Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa wataendelea kuchukua hatua kwa wale wote watakaohusika kukwepa kodi.

Amesema kuwa wataendelea kuchukua hatua dhidi ya wale ambao wamehusika wakiwemo watumishi wanaoshiriki katika hujuma, Wafanyakazi saba wa TPA wanashikiriwa na polisi kuhusiana na upotevu wa kontena hizo na kusababisha serikali kukosa mapato.

Wanashikiriwa na jeshi la polisi ambao wengine wamekamatwa leo ni John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally ,Masoud Seleman, Benadeta Sangawe.

Wanaotafutwa kwa tuhuma za kusababisha upotevu wa kodi za serikali katika bandari ya Dar es Salaam ni Happygod Naftal, Nathan Edward, Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Benasweet Kamaina, Zainab Bwijo.

WATUMISHI WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI WAMPOKEA NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MH. HAMAD MASAUNI

No comments:

Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Hamad Masauni wa pili kushoto akipokelewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mbarak Abdulwakil wa watatu kulia mara baada ya Naibu waziri huyo kupokea Ua alilokabidhiwa na watumishi wa wizara hiyo ikiwa ni ishara ya kukaribishwa wizarani hapo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli kumuapisha kushika wadhifa huo Ikulu jana jijini Dar es Salaam.
Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Hamad Masauni wa kwanza kushoto akisalimiana na Kamisha wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja wa pili kulia muda mfupi baada ya Naibu waziri huyo kukaribishwa wizarani hapo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli kumuapisha kushika wadhifa huo Ikulu jana jijini Dar es Salaam wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Hamad Masauni wa pili kushoto akisalimiana na Kamisha wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Magereza Gaston Sanga wa pili kulia muda mfupi baada ya Naibu waziri huyo kukaribishwa wizarani hapo mara tu baada ya kuapishwa Ikulu jana jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Lilian Mapfa watatu kulia akimkaribisha Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Hamad Masauni wa pili kushoto muda mfupi baada ya Naibu waziri huyo kukaribishwa wizarani hapo mara tu baada ya kuapishwa Ikulu jana jijini Dar es Salaam wa pili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma kwa Jamii.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII PFOF. JUMANNE MAGHEMBE AKABIDHIWA RASMI OFISI LEO NA ALIYEKUWA WAZIRI WA WIZARA HIYO LAZARO NYALANDU

No comments:

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kushoto) akikabidhiwa taarifa ya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kulia) leo tarehe 29 Desemba 2015 ofisini kwake Mpingo House. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Selestine Gesimba (kulia).
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) akizungumza na Waziri wa sasa wa Wizara hiyo Mhe. Prof. Jumanne Maghembe na Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru (kulia) wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika leo tarehe 29 Desemba 2015 katika ofisi za Wizara hiyo Mpingo House. Katika salamu zake Mhe. Nyalandu amepongeza uteuzi wa Prof. Maghembe ambapo amesema Mhe. Rais amefanya chaguo sahihi kwani Prof. Maghembe anao uwezo wa kufanya kazi nzuri katika Wizara hiyo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akizingumza na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Nyalandu (kulia) muda mfupi baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini kwake leo. Mhe. Prof. Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzrui aliyoifanya akiwa Waziri wa Wizara ya Malisili na kuahidi kuanzia alipoishia katika kuhakikisha Maliasili za nchi zinatunzwa ipasavyo ikiwemo kupambana na changamoto zilizopo za ujangili na uharibifu wa misitu na maliasili kwa ujumla.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri kabla yake Mhe. Lazaro Nyalandu, Makabidhiano hayo yamefanyika leo Makao Mkuu ya Wizara hiyo, Mpingo House jijini Dar es Salaam.

Katika makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amekabidhi taarifa rasmi ya makabidhiano kwa Mhe. Waziri Prof. Jumanne Maghembe kama ishara ya kukabidhi rasmi Ofisi ya Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Makabidhiano hayo ambayo ni utaratibu wa kiserikali wa kukabidhi ofisi umeshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Adelhelm Meru, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Selestine Gesimba, baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo na waandishi wa habari.


Akizungumza baada ya makabidhiano hayo Mhe. Nyalandu amempongeza Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Prof. Maghembe kuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili kwa kuwa ana sifa stahiki za kuongoza Wizara hiyo nyeti.

Aliongeza kwa kusema kuwa Prof. Maghembe ana sifa ya kuwa mhifadhi kwa kusomea na pia ni mhifadhi kwa asili yake hivyo Wizara imepata mtu makini kwenye masuala ya Uhifadhi.
“Natambua umahiri wako katika masuala ya uhifadhi nina imani utapambana na ujangili pamoja na usafirishaji haramu wa magogo kwa kasi inayotarajiwa na wananchi”. Alisema Mhe. Nyalandu.
Kwa upande wake, Waziri aliyechukua nafasi yake Prof. Jumanne Maghembe amempongeza Mhe. Nyalandu kwa kazi nzuri na juhudi aliozoonesha wakati akiwa Waziri wa Wizara hiyo katika kuhakikisha Maliasili zilizopo zinaendelea kuwepo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho. 
Prof. Maghembe ameongeza kuwa kwa sasa vita kubwa iliyoko mbele yake ni vita dhidi ya ujangili na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa rasilimali za misitu kinyume cha sheria. Ameomba ushirikiano kwa wadau wote wa Maliasili nchini kumpa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha anafanikiwa katika vita hiyo.
Pamoja na mambo mengine taarifa hiyo ya makabidhiano inaelezea kazi zilizokwisha kufanyika katika kipindi cha utawala uliopita, kazi zinazoendelea na zilizopo kwenye mpango wa utekelezaji pamoja na changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo Ujangili na uvunaji pamoja na usafirishaji wa magogo. 
(Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii)
 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger