Jovina Bujulu- MAELEZO.
Misitu ni ardhi yoyote yenye uoto
wa mime na wingi wa miti iwe ya asili au ya kupanda yenye kimo
chochote, ivunwayo na isiyonunwa na iliyo na uwezo wa kutoa mbao au
mazao mengine yenye uwezo wa kurekebisha hali ya hewa au mfumo wa
vyanzo vya maji au yenye kuhifadhi mifugo au wanyamapori.
Wakala wa Misitu Tanzania ni
taasisi yenye dhamana ya usimamizi, uvunaji na usafirishaji wa mazao ya
misitu, hususan mkaa, mbao, kuni, magogo, nguzo na mazao ya nyuki na
jukumu lingine ni kusimamia utekelezaji wa sheria za misitu katika
maeneo yaliyo chini yake.
Kutokana na jukumu hilo, Wakala
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) na Jeshi la Polisi wameendelea na kampeni ya kutoa elimu
kwa wananchi kufuata sheria na kanuni za usafirishaji halali wa mazao
ya misitu.
Aidha, Wakala pia inatoa elimu kwa
wananchi juu ya matumizi bora ya vyombo vya moto zikiwemo pikipiki za
magurudumu mawili na baiskeli kutokubeba mazao hayo mazao ya misitu.
Kamanda Mohamed Mpinga
Akizungumzia suala la kusafirisha
mazao ya misitu kwa kutumia pikipiki na baiskeli, Kamanda wa Kikosi
cha Usalama barabarani, Kamishna Msaidizi Mohamed Mpinga alisema kuwa
ubebaji huo hauruhusiwi na ubebaji wa mazao hayo ya misitu kwa njia
zisizoruhusiwa vimekuwa ni miongoni mwa vyanzo vya ajali za barabarani.
“Sheria ya usalama barabarani,
sura ya 58 sehemu ya 1 na 2 inazungumzia upakiaji wa hatari, hivyo ni
marufuku kwa dereva kupakia kupita kiasi pia inakataza ubebaji wa mizigo
kiasi ambacho mwendeshaji anashindwa kuona nyuma na pia anakosa nafasi
ya kukaa vizuri na hivyo kusababisha uendeshaji usio salama” anasema
Kamanda Mpinga.
Kamanda huyo pia amesisitiza kuwa
sheria za usalama barabarani zipo kwa ajili ya kulinda usalama wa
dereva na ametoa wito kwa madereva wa pikipiki na baiskeli kuacha
kubeba mizigo kupita kiasi katika vyombo hivyo.
SUMATRA ambayo ndio wenye dhamana
ya wanasimamia leseni za usafirishaji na masharti yaliyopo kisheria,
imepitisha sheria ambayo inaruhusu pikipiki na baiskeli kubeba abiria
mmoja tu, kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria na kuhatarisha usalama
wa dereva na raia wengine wanaotumia barabara.
Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti na
Usafiri wa Barabarani ndugu Leo Ngowi alisema kuwa kanuni za
usafirishaji za mwaka 2010 zinakataza mtu yoyote kufanya biashara ya
kubeba abiria bila kuwa na leseni na dereva haruhusiwi kubeba mizigo
kama magogo na mkaa.
Aliendelea kusema kuwa mamlaka
haitasita kumkamata na kumfungulia mashtaka mtu yoyote ambaye anakiuka
kanuni hizo za matumizi tofauti ya msingi wa matumizi ya vyombo hivyo
vya usafiri.
Profesa Dos Santos Silayo ambaye
ni mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu alisema kuwa Wakala unasimamia
sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002, kifungu cha 106 pamoja na
kanuni za sheria hiyo za mwaka 2004, inayotoa maelezo na mwongozo wa
uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu ya mwaka 2005.
“Sheria hiyo inatoa maelekezo ya
namna ya uvunaji unavyopaswa kufanywa pamoja na usafirishaji wake, ikiwa
ni pamoja na kutekeleza sheria nyingine za nchi za usalama barabarani
na masharti ya leseni ya usafirishaji yanayosimamiwa na SUMATRA” alisema
Profesa Silayo.
Aliongeza kusema kuwa siku za hivi
karibuni kumekuwa na ongezeko la usafirishaji wa mazao ya misitu kwa
kutumia pikipiki na baiskeli. Aliitaja mazao yanayosafirishwa kwa wingi
kuwa ni pamoja na mkaa, mbao na nguzo ambayo kwa kiasi kikubwa
yanapatikana kwa njia zisizo rasmi na wafanyabiashara wakubwa wanatumia
njia hizi kukwepa vizuia vya ukaguzi.
Kwa kutumia vyombo hivyo
wafanyabiashara hao wanaweza kuingia kwenye maeneo mengi ya misitu na
hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa misitu na kukwepa ushuru wa
Serikali uliowekwa kwa mujibu wa sheria.
Alisema kuwa usafirishaji wa mazao
ya misitu kwa kutumia pikipiki na baiskeli hauruhusiwi kwa mujibu wa
sheria na taratibu za nchi. Alitoa wito kwa kila msafirishaji na
mfanyabiashara wa mazao ya misitu yanayopatikana kihalali, kutumia
vyombo vinavyoruhusiwa kisheria.
Kamanda Mpinga alitoa wito kwa
waendesha pikipiki na baiskeli ambao wamekuwa na mazoea ya kupakia
mazao ya misitu kutoka eneo moja kwenda lingine kiasi cha kuweza
kusababisha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara kuacha mara moja
tabia hiyo.
“Jeshi la Polisi halitasita
kuchukua hatua kali kwa wenye kuendeleza tabia ya kupakia mkaa na mazao
mengine ya misitu, kiasi cha kuhatarisha maisha yao na watumiaji wengine
wa barabara” alisema kamanda Mpinga.
Kamanda Mpinga amewataka madereva
hao kuzingatia sheria na kanuni mbalimbali zilizopo katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha kuwa masuala yote yanayohusiana na
usafirirshaji wa mazao hayo yanakwenda kwa mujibu wa maelekezo
wanayopewa na wataalamu mbalimbali katika maeneo yao wanapoishi.
Naye ndugu Ngowi amewataka watu
wote wanaotumia vyombo vya kusafirishia abiria kuacha mara moja kutumia
vyombo hivyo kinyume cha matakwa ya leseni ya chombo husika.
Hivi karibuni Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania walianza operesheni ya kuimarisha utekelezaji wa sheria
za usafirishaji wa mazao ya misitu hususani mkaa, kwa lengo la
kuwahimiza wananchi kufuata kanuni na sheria hizo.
Akizungumza jijini Dar es salaam
hivi karibuni , Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Misitu na
Nyuki nchini, ndugu Mohamed Kilongo alisema kuwa utekelezaji huo
utafanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na utashirikisha maofisa
wa polisi, SUMATRA pamoja na Wakala wa Misitu.
“Tathmini iliyofanyika inaonyesha
kuwa pikipiki na baiskeli zinachangia uvunaji haramu na usafirishaji wa
haraka wa mazao ya misitu ambapo inakadiriwa kuwa pikipiki 20
zikisafirisha mkaa ni sawa na lori moja la tani saba lililojaa mkaa”
alisema ndugu Kilongo.
SHARE









No comments:
Post a Comment