Kulia ni Joseph Masikitiko akizungumza katika moja ya mikutano yake..
Julian Msacky
MAPEMA mwezi huu shehena ya mafuta ya petroli yenye
ujazo wa tani 38,521 ilikamatwa nchini baada ya kubainika kuwa mafuta hayo
yalikuwa hayafai kwa matumizi.
Shehena hiyo ni kubwa, lakini jambo la kujifunza
hapa ni kwamba zipo bidhaa nyingi ambazo zinachangia kusababisha madhara kwa
Mtanzania tena ya kujitakia.
Kama mfanyabiashara anaamua kuingiza nchini mafuta
yasiyo na ubora maana yake hathamini maisha ya wengine. Mafuta yake
yakisababisha ajali si tatizo ili mradi apate fedha.
Hii si sahihi hata kidogo. Ni kukosa ubinadamu.
Kimsingi wanaofanya biashara za aina hiyo wanatakiwa kutazamwa mara mbilimbili
kwa sababu hawana nia njema na wengine.
Ni kwa msingi huo ninashauri uroho wa fedha usifikie
hatua ya kugharimu hata maisha yetu. Kuingiza mafuta yasiyofaa athari zake kwa
vyombo vya moto ni kubwa mno.
Miongoni mwa athari hizo ni mitambo ya magari
kuharibika na hivyo kutoa fursa au nafasi kubwa ya vyombo hivyo kusababisha
ajali na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.
Ifahamike kuwa shehena hizo zilikamatwa Bandari ya
Dar es Salaam kwenye meli ya MT. Ridgebury John B kutoka Falme za Kiarabu ambao
ni waagizaji.
Hata hivyo, yalizuiliwa kwa kukosa viwango vya ubora
kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Namba 2 ya 2009.
Ni kwa msingi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Joseph Masikitiko anasema kukamatwa kwa shehena hizo
kunatokana na ukaguzi uliofanywa na wataalamu waliobobea, wakiwemo wa mafuta na
maabara.
Kwa mujibu wa Masikitiko ubora wa mafuta ya petroli
hupimwa kwa kutumia kiwango namba TZS 672:2012/EAS 158:2012 ambacho
kimeoanishwa kwa kuzingatia matakwa ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika
Mashariki.
Masikitiko anasema matakwa hayo ni pamoja na
kuhakikisha yanafaa kwa matumizi ya magari, afya ya wananchi na uhifadhi wa
mazingira.
Hata hivyo, alisema mafuta hayo hayakukidhi viwango
kwani yana uwezo mkubwa wa kuvuta maji au mvuke, jambo ambalo si zuri.
Mkurugenzi huyo anasema mafuta ya aina hiyo hayawezi
kufanya kazi iliyokusudiwa katika injini kutokana na uwepo wa maji katika
petroli.
Anasema mvuke ukiwa mwingi kwenye injini husababisha
mtiririko wa mafuta kwenda kwenye injini kutokuwa mzuri na kisha kuiharibu.
Pia, mafuta ya aina hiyo husababisha kupungua kwa
nishati ya kuendeshea injini hivyo, kuharibika haraka kwani wingi wa ujazo wa
mafuta usiokuwa na uhalisia hutoa nishati isiyolingana na wingi wake.
"Madhara yake ni mnunuzi kununua na kulipa
wingi wa mafuta usio na thamani halisi, pia huongeza uharibufu wa mazingira
kutokana na moshi mchafu wa mitambo unaotoka kwenye magari,"anasema.
Alisema madhara mengine ni kiuchumi kwani, nchi
hulazimika kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza vipuri kwa ajili ya
matengenezo ya magari mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo athari nyingine
husababisha uchumi wa mtu binafsi kuyumba kutokana na kutumia gharama nyingi
kutengeneza injini na vipuri vyake.
"Benzene ikizidi kwenye mafuta ya petroli
husababisha ugonjwa wa kansa, hasa kwa wale wanaotoa huduma za uuzaji wa
petroli," anasema.
Ni kutokana na athari hizo na nyingi nyingi
tunashauri wafanyabishara wetu wawe waaminifu katika shughuli zao hususan
kununua bidhaa zenye ubora.
Bila kufanya hivyo maisha ya wananchi wetu
yataendelea kuwa hatarini kila siku. Ninajiuliza kama shirika hilo halikukamata
mafuta hayo si yangeingia sokoni?
Kama yangeingia kwenye mzunguko athari zake bila
shaka ni nyingi. Ni kwa msingi huo tunaamini hata ajali zinazotokea mara kwa
mara nchini yapo mambo mengi yaliyofichika.
Ni wakati muafaka kwa shirika hilo kuongeza nguvu
katika ukaguzi ili kubaini bidhaa nyingine za vyombo vya moto ambazo
zinaingizwa nchini kwetu kinyemela.
Inawezekana vifaa vingi vinavyofungwa katika vyombo
hivyo, yakiwemo matairi hayana ubora unaotakiwa na hivyo kuwa kitanzi kwa
watumiaji.
Tunaendelea kulitia moyo shirika kufanyakazi zake
kwa uaminifu ili kulinda maisha ya Watanzania kwa sababu ndilo linaloshikilia
maisha yetu kwa asilimia kubwa.
Kwa msingi huo watendaji wake wanatakiwa kupatiwa
nyenzo nzuri ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri. Kwa kufanya hivyo
watatuokoa na mambo mengi.
Jambo jingine ni waagizaji wa bidhaa kuwa na roho ya
huruma kwa walaji. Wakiwa na roho ya huruma hawatakubali kuingiza nchini vifaa
au bidhaa za ovyo ovyo.
Kama alivyosema Masikitiko bidhaa zisizo na ubora
zinachangia umaskini kwa wateja. Hii ni kwa sababu wanapoteza fedha zao kununua
vitu visivyodumu muda mrefu.
Matokeo yake wanaendelea kutoboa mifuko yao kila
siku. Akinunua radio au simu zikipita siku chache tu matatizo yanaibuka na mara
anaachana nayo.
Katika mazingira ya aina hii mteja au mnunuzi
anageuka mwathirika wa kubeba msalaba wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi, hivyo
lazima tushikamane kuumbua wahusika.
Kuwaumbua ni wananchi kutoa taarifa katika mamlaka
husika wanapoona au kuhisi vitu, vifaa au bidhaa wanazouziwa, yakiwemo mafuta
yana matatizo.
Hebu fikiria hiyo ni shehena ya mafuta ya magari au
mitambo. Ingekuwaje kwa mfano, mafuta hayo yalikuwa ya kupikia bila shaka
maisha ya wengi wetu yangekuwa hatarini.
Si hivyo tu, lakini tunaamini yapo mafuta ya kula
yanapenyezwa nchini na shirika kushindwa kubaini wahusika. Ndiyo maana siku
hizi milipuko ya magonjwa imekuwa mingi mno.
Watu wananenepeana ovyo ovyo. Hili nalo linatakiwa
kutazamwa kwa undani. Ni vema shirika likafungua macho zaidi ili kunusuru
maisha ya wananchi wetu.
Hii ina maana kuwa watu wachache wasipewe nafasi ya
kucheza na maisha ya Watanzania kwa sababu ya maslahi yao. Ni imani ya wengi
wetu kuwa mchezo huo utakomeshwa leo au kesho.
SHARE
No comments:
Post a Comment