JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
|
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais
Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki-moon kuunda jopo la watu mashuhuri
watakaomshauri juu ya namna bora ya kuendeleza na kutekeleza malengo ya maendeleo
endelevu hususani katika afya ya uzazi ya Mama na mtoto.
Jopo hilo
la watu mashuhuri linaongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Rais wa Chile
Mheshimiwa Michelle Bachelet na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam
Desalegn, huku Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Finland
Mheshimiwa Tarja Halonen wakiteuliwa kuwa wenyeviti mbadala.
Katika
Pongezi hizo Rais Magufuli amesema kuteuliwa kwa Rais Kikwete kuwa miongoni mwa
jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumeijengea heshima Tanzania
na kumechochea matumaini ya mafanikio ya kukabiliana na changamoto za afya ya
mama na mtoto hususani kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Rais
Magufuli ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano itatoa ushirikiano katika
kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ambayo jopo hilo litamshauri Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa ikiwemo katika kuimarisha afya ya uzazi wa mama na mtoto.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
25 Januari, 2016
SHARE









No comments:
Post a Comment