MWANDISHI WETU
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limewataka walaji na watumiaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha zinakuwa na nembo
ya shirika hilo.
Mwito huo ulitolewa jana na Ofisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Gladness Kaseka wakati akizungumza na waandishi wa habari katika
viwanja vya maonesho ya Sido Kanda ya Kati yanayofanyika Uwanja
wa Chipukizi mkoani Tabora.
Alisema faida za kununua bidhaa yoyote yenye nembo ya ubora
iliyotolewa na TBS huthibitisha pasipo shaka kuwa bidhaa husika iko
katika kiwango kinachokubalika na inafaa kwa matumizi ya binadamu.
Ofisa huyo alisema kuwa bidhaa iliyothibitishwa na shirika hilo huongeza
ubora wake na kuinua soko lake ndani na nje ya mkoa husika ikiwemo nje
ya nchi na humpa uwezo mzalishaji kushindana vizuri zaidi sokoni.
Alitaja faida nyingine ya uwepo wa nembo ya TBS katika bidhaa
humwongezea wateja mzalishaji na humkinga dhidi ya ushindani wa bidhaa
hafifu zisizo na ubora ikiwemo kuaminika zaidi kwa bidhaa hiyo.
Kaseka alibainisha kuwa alama ya ubora ya TBS ikiwa kwenye bidhaa
huonesha kuwa bidhaa hiyo imepimwa na ina viwango vinavyokubalika kwa
mlaji kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha bidhaa husika.
"Wananchi nunueni bidhaa zenye nembo ya shirika la viwango kwani ni
uthibitisho tosha kwa mzalishaji na mlaji kuwa bidhaa husika ni bora na
salama kwa matumizi," alisema.
Alibainisha kuwa Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha
kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati ili
kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinathibitishwa ubora wake.
Alisema katika mpango huo wa serikali, shirika la viwango limetoa
kipaumbele cha kuthibitisha na kutoa nembo za ubora wa bidhaa kwa
wajasiriamali wadogo pasipo kulipia gharama yoyote kwa sababu ya mitaji
yao bado midogo.
Ofisa huyo alisema kuna umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zote
zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo hapa nchini zinakuwa na ubora
unaotakiwa ili kuinua sekta ya uzalishaji na wazalishaji wote.
Alisema shirika lake limejipanga kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa
kwa wazalishaji wote ili kutambua umuhimu wa kutumia nembo ya ubora wa
bidhaa zao.
Kaseka alisema mapambano ya kudhitibiti bidhaa hafifu ni ya Watanzania
wote hasa watumiaji wa vyakula na bidhaa nyingine zinazozalishawa hapa
nchini.
SHARE
No comments:
Post a Comment