Wanawake wawili wilayani Igunga mkoani Tabora wameuawa kikatili kwa
kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana huku mmoja akikatwa kiganja cha
mkono wa kulia.
Mtendaji wa Kata ya Tambalale, Salumu Kitindi alimtaja aliyeuawa kuwa ni
Elizabeth Charles (45), mkulima wa kijiji cha Tambalale, kata hiyo ya
Tambalale, Tarafa ya Nsimbo.
Kitindi alisema watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa mama huyo
ambaye kwa sasa ni marehemu usiku kisha kuingia ndani na kumshambulia
kwa mapanga hadi kupoteza uhai wake ambapo baada ya kufanya mauaji hayo
walikata kiganja cha mkono wa kulia kisha kuondoka nacho kusikojulikana.
Naye Mtendaji wa Kata ya Mwisi, Issa Omary alisema katika kata yake,
mwanamke Suzana Alex (24) mkulima mkazi wa Kijiji cha Busomeke, Tarafa
ya Simbo ameuawa kwa mapanga kwa kukatwa sehemu mbalimbali za mwili wake
huku mumewe, John Matheo (27) akijeruhiwa vibaya ambapo amelazwa
Hospitali Misheni ya Ndala iliyoko Nzega.
Aidha, Omary alibainisha kuwa watu hao walifika katika mji huo saa saba
usiku ambako walivunja mlango na kuingia ndani kisha kuanza kuwakata kwa
mapanga wanandoa hao na kusababisha Suzana kuuawa papohapo kisha
kuondoka bila ya kubeba kitu chochote.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na
Usalama wa wilaya hiyo, John Mwaipopo alithibitisha kuuawa kwa
akinamama hao na kueleza kuwa Jeshi la Polisi Igunga linaendelea na
msako wa kuwabaini waliohusika na mauaji hayo huku akitoa onyo kali kwa
watu wanaojihusisha na mauaji kuacha mara moja.
SHARE
No comments:
Post a Comment