Mfalme Letsie wa III wa Falme ya Lesotho
Mkuu
wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt.
Augustine Mahiga (Mb.) akisalimiana na Mfalme Letsie wa III wa Falme ya
Lesotho, alipo kutana nae na kufanya mazungumzo.
Mkuu
wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa
Afrika na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa
Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amemhakikishia Mfalme Letsie wa III
wa Lesotho kuwa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama
imethibitisha pasipo mashaka utayari wa wapiga kura wa nchi hiyo kupiga
kura siku ya Jumamosi tarehe 3 Juni 2017.
Hayo
yamesemwa kwenye mazungumzo ya viongozi hao ambapo Mhe. Dkt. Mahiga
alimuelezea Mtukufu Mfalme Letsie wa III, hatua mbalimbali za uangalizi
wa uchaguzi zilizochukuliwa na Jumuiya ya SADC tangu alipofika nchini
Lesotho. Jumuiya hiyo mbali na kupeleka waangalizi 41 wa uchaguzi kutoka
kwenye nchi tisa wanachama, pia ina wajumbe wawili wa Baraza la Ushauri
wa Masuala ya Uchaguzi ambapo mmoja wa wajumbe hao ni Jaji Mstaafu John
Tendwa wa Tanzania.
Mhe.
Mahiga pia alisifu jitihada za Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi ya
Lesotho ambao kwa pamoja wamehakikisha kuwa mazingira mazuri
yameandaliwa yatakayoruhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu kufanyika kama
ilivyopangwa.
Kwenye
mazungumzo yao, Mhe. Mahiga alitumia pia nafasi hiyo kumpelekea Mfalme
Letsie salaam za heshima kutoka kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi
ya Ushirikiano ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama ambayo inaundwa na
nchi za Tanzania, Msumbiji na Angola kwa sasa.
Kwa
upande wake, Mtukufu Mfalme Letsie wa III wa Falme ya Lesotho
alimshukuru Mhe. Rais Magufuli kama kiongozi wa asasi hiyo muhimu ya
Jumuiya ya SADC na kuongeza kuwa ni matarajio yake kuwa chini ya uongozi
wake makini na mahiri, nchi wanachama wa Jumuiya watatekeleza kwa
ufanisi majukumu yao muhimu ya kuendeleza jumuiya.
Mfalme
huyo mrithi wa baba yake Mfalme Moshoeshoe wa II anayetawala Lesotho
tangu mwaka 1996 kama Falme ya Kikatiba, alisema anaiheshimu sana
Tanzania kwa mchango mkubwa kwa nchi hiyo hususan kwenye kuendeleza
taaluma mbalimbali nchini humo. Alisema kwa miaka mingi sasa wataalamu
wa masuala ya afya na elimu kutoka Tanzania wameendelea kufanya kazi
Lesotho na kuongeza kuwa hata yeye binafsi alifundishwa Chuo Kikuu cha
Lesotho na Mtanzania masomo ya Sheria na Sayansi ya Siasa.
Mtukufu
Mfalme Letsie alimaliza kwa kuahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu
uliopo baina ya Lesotho na Tanzania ambapo chimbuko lake ni kuwa nchi
zote mbili ni wanachama waanzilishi wa Jumuiya ya SADC. Aidha alionesha
nia kubwa ya kuzuru Tanzania siku za usoni, na kumuomba Mhe. Dkt.
Mahiga, kufikisha salamu za heshima na ushirikiano kwa Rais na wananchi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Maseru, Lesotho 25 Mei, 2017
SHARE
No comments:
Post a Comment