NA
OWM, HAVANA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na
kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Balozi Lucas Domingo
Polledo, ambapo amewakaribisha wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika
ujenzi wa viwanda vya dawa.
Amesema kwa sasa Serikali ya Tanzania inaagiza
dawa kutoka nje ya nchi jambo ambalo linasababisha kutumia fedha nyingi, hivyo
uwepo wa kiwanda utasaidia katika kupunguza gharama. Pia wawekezaji watakuwa na
uhakika wa soko la bidhaa zao.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumanne,
Agosti 22, 2017) wakati akizungumza na Balozi Polledo mjini Havana. Waziri Mkuu
yuko nchini Cuba kwa ajili ya
ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Alisema Serikali imedhamiria kuendeleza sekta ya
viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati, hivyo
wafanyabiashara kutoka nchini Cuba wanakaribishwa kuja kuwekeza nchini,
hususani katika viwanda vya dawa na sukari.
Waziri Mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa ni
nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, pia imeweka mazingira mazuri ya
uwekezaji jambo ambalo litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.
Pia alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya
Cuba kwa ushirikiano mzuri na Serikali ya Tanzania kwa sababu Cuba ni mojawapo kati ya nchi zenye ushirikano
wa muda mrefu na Tanzania hususani katika masuala ya Kisiasa, Kijamii, Kielimu
na Kiuchumi.
“Tanzania na Cuba zina historia ya kutosha.
Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati nchi zote mbili, ambayo yalikuwepo
kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Hayati
Mwl. Julius Nyerere.”
Kwa upande wake, Balozi Polledo alisema Serikali ya Cuba
itahakikisha uhusiano wake na Serikali ya Tanzania unaendelea kuimarishwa. Pia
alipongeza jitihada zinazofanywa
na Serikali katika kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.
Alisema licha ya kuwahi kufanya kazi kama Balozi
katika nchi mbalimbali za Afrika, baada ya kufika Tanzania amefurahishwa na
kasi ya ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarika kwa hali ya siasa na amani.”Hali
hii ni tofauti na mataifa mengine ya Afrika.”
Pia Balozi Polledo alisema kwamba Serikali ya
Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa Sekta za Afya na
Elimu, ambapo alisema jumla ya madaktari 50 wa Cuba wakiwemo maprofesa 11 wako
nchini wakihudumia wananchi katika mikoa mbalimbali.
SHARE








No comments:
Post a Comment