NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akifungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa
Shirikisho la Vyuo Vikuu Seneti ya Unguja uliofanyika Afisi Kuu ya CCM
Kisiwandui Zanzibar.
……………………………………………………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimewaagiza vijana wasomi wa Chama hicho kuanzisha utamaduni
wa kufanya Tafiti mbali mbali za kitaalamu ili kubaini baadhi ya
changamoto zinazokabili kundi la vijana na jamii kwa ujumala hasa
upungufu wa ajira.
Agizo hilo amelitoa wakati
akifungua Mkutano wa Uchaguzi wa Shirikisho la Vyuo vikuu CCM Unguja la
kuwachagua viongozi Watano wa Seneti ya Unguja, ambapo Mkutano huo
umefanyika katika Afisi Kuu CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Dk.Mabodi alisema Wasomi wa Vyuo
vikuu ndani ya CCM ni lazima wakubali mabadiliko ya nyakati kwa kufanya
kazi zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mfumo wa Sayansi na
Teknolojia kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya ndani ya taasisi hiyo
imara ya Kisiasa.
Alisema nchi zilizoendelea
duniani zinategemea msaada mkubwa wa wasomi ambao ni vijana waliohitimu
fani mbali mbali katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ambao wana
uwezo na maarifa ya kitaalamu yanayochochea ufanisi wa kimaendeleo.
Pia, aliongeza kwa kueleza kwamba
CCM ina utajiri wa Rasilimali watu waliobobea katika fani mbali mbali
hivyo ni lazima watoe mchango wao katika kuandaa mipango mikakati ya
kukiletea chama hicho ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola
mwaka 2020.
Hata hivyo amesema vijana hao wa
Vyuo vikuu wana wajibu wa kusoma alama za nyakati kwa kuwa mfano bora wa
kubuni na kutekeleza kwa vitendo mikakati mbali mbali ya kiuchumi na
kijamii ili vijana vya vyama vya upinzani wavutiwe na utamaduni huo na
kujiunga na hatimaye kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Akizungumzia fursa zinazotokana
na usimamizi pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2015/2020 alitaja mchakato wa Utafiti wa Uchimbaji wa mafuta na Gesi
Zanzibar kuwa ni sehemu muhimu inayohitaji vijana wasomi watakaolinda
rasilimali hiyo isifilisiwe na nchi za kigeni.
Alisema fursa ya kuanza utafti
huo ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964
chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume, aliyeasisi mfumo rasmi wa Zanzibar kujitawala
kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“ Utafiti huu umeanza mwaka 1952
ambao ulibaini ndani ya Ardhi na mwambao wa visiwa vya Zanzibar kuwepo
kwa dalili za rasilimali hiyo inayoingia katika kundi la madini asilia,
na juhudi ziliandelea hadi kufikia Serikali ya awamu ya saba chini ya
Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Shein kupigania suala hilo likapewa
baraka za kisheria zilizoruhusu Zanzibar kushugulikia yenyewe mchakato
wa utafiti hadi uchimbaji”,. Alieleza Dk.Mabodi.
“ Nyinyi ni wasomi ambao jamii ya
Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla wanakutegemeeni mlete mabadiliko ya
kweli ndani ya Chama chetu na Serikali zote mbili zinazotokana na CCM.
Lakini pia ni lazima muwe wabuni
kwa kufanya utafiti ndani na nje ya CCM kwa lengo la kupata takwimu
sahihi za mambo mbali mbali yatakayosaidia Chama kuimarika kisiasa
kutokana na mingo yake kutekelezwa Kisayansi.”, alisema.
Akizungumzia kwa ufupi historia
ya Zanzibar Dk.Mabodi alisema kuwa maandiko mbali mbali ya historia
yanadhibitisha kuwa Zanzibar kabla ya kutawaliwa na Wakoloni ilikuwa na
Utawala wake wa jadi uliokuwa katika mfumo wa ujima, ambao wananchi wake
waliishi kwa amani , ujamaa na kujitegemea.
Alisema kupitia muongozo huo wa
historia ni lazima vijana wa sasa wajijue kuwa wana jukumu la
kuhakikisha CCM iliyotokana na vyama vya ASP na TANU inaendelea kutawala
na hakuna Chama chochote cha upinzani kitakachoshika madaraka.
Akizungumzia Uchaguzi wa
viongozi mbali mbali wa Shirikisho hilo alisema ni lazima wachague
viongozi bora wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa waliowachagua
bila ya kusukumwa.
Pamoja na hayo aliwasisitiza
wajumbe wa Mkutano huo kuhakikisha wanachagua wenye uwezo na uthubutu wa
kujenga hoja imara na kujibu hoja za wapinzani bila ya kuteteleka.
Aliwataka wasimamizi wa Uchaguzi
huo kutenda haki bila ya upendeleo wa mgombea yeyote ili kulinda heshima
ya CCM na kuruhusui mkondo wa Demokrasia ifanye kazi yake kwa mujibu wa
miongozo na kanuni za uchaguzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UVCCM
Taifa Tabia Maulid Mwita alisema mafanikio yaliyopatikana Zanzibar
katika sekta mbali mbali yametokana na juhudi za kiutendaji na ushiriki
wa vijana wasomi wa Chama hicho.
Ametoa nasaha wa vijana hao kuwa
ili kufikia malengo waliojiwekea kisiasa ni lazima wafanye kazi kwa
bidii ili kukisaidia chama kufikia malengo yake ya kushika dola kila
uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo ndogo.
Pamoja na hayo alisisitiza
umuhimu wa vijana wa shirikisho hilo la vijana wa CCM wa vyuo vikuu
kusoma Katiba ya CCM pamojana na kanuni ya UVCCM kwa lengo la kutambua
wajibu,haki zao pamoja na mipaka yao kiutendaji.
Akitoa salamu za Mwenyekiti wa
Umoja huo Kheri James, Tabia alisema kuwa kiongozi huyo anawasihi
waendelee kuwa wamoja kwa kila jambo jema lenye malengo ya kuleta
manufaa ndani ya CCM na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Mapema Mwenyekiti anayemaliza
muda wake katika Shirikisho hilo Khamis Kheri Ame alisema lengo la
uchaguzi huo ni kutimiza matakwa ya Kikatiba yanayoruhusu mabadiliko ya
awamu za uongozi kwa kila kipindi cha miaka mitatu.
Pamoja na hayo amewashukru
wajumbe wa Shirikisho hilo alioshirikiana nao kwa kipindi chote cha
uongozi wake na kuwataka viongozi wapya watakaochaguliwa kuhakikisha
wanalivusha salama shirikisho hilo kuelekea ng’ambo ya maendeleo
endelevu.
SHARE
No comments:
Post a Comment