Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mke wa Rais Mstaafu wa
Awamu ya Nne na Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete wakati wa hafla
ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo-Makofia-Msata yenye urefu wa
kilomita 64, Wilayani Bagamoyo, Pwani. Mama Salma amekuwa mstari wa
mbele kupinga mwanafunzi wa kike kuendelea na masomo mara baada ya
kujifungua. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhwani
Kikwete.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO
…………………
Na. Frank Shija-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake
haitoruhusu mwanafunzi aliyepata ujauzito kuendelea na masomo kama
ambayo baadhi ya Asasi za Kiraia zinavyopiga kampeni kuruhusu wanafunzi
kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.
Kauli hiyo imetolewa Wilayani
Bagamoyo mkoa wa Pwani na Mhe. Rais alipokuwa akizungumza katika hafla
ya uzinduzi wa Barabara ya Bagamoyo–Makofia-Msata, yenye urefu wa
kilomita 64
“Nataka niwaambie ndani ya utawala
wangu hakuna mwanafunzi mwenye mimba atakaye rudi shuleni, hayo ndiyo
maisha aliyoyachagua, akalee huyo mtoto. Hata hivyo anaweza akaanza
maisha mengine akaenda Veta, akajifunza kushona au kuchukua mkopo na
kujiingiza katika kilimo cha kisasa,” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli aliongeza kuwa
Serikali haiwezi kulipeleka taifa hili katika maadili ambayo hayapo
katika jamii ya Kitanzania, hivyo kuruhusu watoto wa kike waliopata
ujauzito kuendelea na masomo ni kuharibu maadili ya Kitanzania.
Rais Magufuli amesema kuwa lengo
la Serikali ni kuhakikisha watoto wanapata elimu ndiyo maana alianzisha
sera ya kutoa elimu bure, hivyo wanaopiga kelele kuwa watoto wa kike
wanaopata ujauzito wapewe nafasi ya kuendelea na masomo wanataka
kurudisha nyuma nidhamu ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine Rais
Magufuli alimpongeza Mke wa Rais Mstaaafu wa Awamu ya Nne na Mbunge wa
Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete kwa juhudi zake za kupigania haki ya
watoto wa kike kwa kupinga jambo hilo ndani ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania linaloendelea.
Aidha Rais Magufuli alisisitiza
kuwa kamwe Serikali haiwezi kufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya
Asasi za Kiraia na kuzishauri asasi hizo kuwa badala ya kuishawishi
Serikali ichukue uamuzi wa kuwaruhusu watoto wa kike wanaopata ujauzito
kuendelea na masomo ni bora asasi hizo zikaanzisha shule zitakazotoa
fursa hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa Sera ya
Serikali ni kumsomesha mtoto bure na siyo kumfundisha azae na kwamba
suala hilo halikubaliki katika Serikali yake na kusisitiza kuwa hakuna
mwanafunzi mwenye mtoto atakaye ruhusiwa kuendelea masomo.
Hivi karibuni kumekuwa na mijadala
bungeni na katika asasi za kiraia kuhamasisha Serikali iharakishe
mchakato wa kuruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo
katika shule za msingi na sekondari mara baada ya kujifungua.
SHARE
No comments:
Post a Comment