*Wanunuzi wataruhusiwa kuyakagua (Januari 25 na 26) kabla ya mnada *Watakaovuruga mnada kukiona cha mtemakuni
Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili na Utalii, Dodoma
SERIKALI
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) itafanya mnada wa hadhara wa meno ya viboko
vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.
Mnada
huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango umepangwa kufanyika
tarehe 29 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi katika Jengo la Mpingo,
Barabara ya Nyerere Jijini Dar es Salaam, zilipokuwa ofisi za Wizara ya
Maliasili na Utalii (Ivory Room).
Waziri wa Maliasili, Dk Hamis Kigwangalla
Kupitia
taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara amesema
mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya
Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.
Amesema
wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na
26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni
kabla ya siku ya mnada huo.
Aidha,
amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25
ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa
ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.
“Mtu
yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa
asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka
kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake,” ameonya Mkurugenzi huyo.
Amesema
meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au
kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa
kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na
kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.
SHARE
No comments:
Post a Comment