SERIKALI ipo katika hatua za mwisho za kuilipa kampuni ya Bhart Airtel ili kurejesha umiliki wa asilimia 100 katika Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Uamuzi huo unaotarajiwa kutekelezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu utaiwezesha TTCL kurejesha hisa zake asilimia 35 zilizonunuliwa na Airel mwaka 2001 na kuifanya Bhart Airtel kuwa mbia mwenza katika Kampuni hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametangaza uamuzi huo Jumatatu hii mkoani Mtwara alipotembelea Ofisi za TTCL Mkoa wa Mtwara, kukagua mitambo na miundo mbinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
"Serikali inesikia kilio cha muda mrefu cha Watanzania na wadau wote wa TTCL kuhusu kuondoka kwa mbia mwenza Kampuni ya Bhart Airtel. Ubia huu wa TTCL na Bhart Airtel utahitimishwa rasmi kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Tumefanya majadiliano ya kutosha, tumekubaliana kuwa Serikali iilipe Bhart Airtel sh Bilioni 14.9 ili kurejesha hisa asilimia 35 ndani ya TTCL na kuifanya Kampuni hii kuwa mali ya Umma kwa asilimia 100.
"Tutatumia fedha za Mapato ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kukamilisha utaratibu huu. Naiagiza Bodi na Menejimenti ya TTCL kufanya kazi kwa bidii na Ufanisi Mkubwa na kusimamia kikamilifu shughuki za TTCL ili kutimiza jukumu lake kwa Umma," alisema Waziri Prof. Mnarawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Prof. Tolly Mbwette alisema, kukamilika kwa mchakato huu ni hatua muhimu kwa Uhai na ufanisi wa TTCL na kusisitiza kuwa, mpango wa mageuzi ya kibiashara wa kampuni hiyo sasa utatekelezeka kwa kasi kubwa baada ya hatua hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema, jitihada kubwa za TTCL sasa zitaelekezwa katika kuboresha huduma kwa kutumia fedha za ndani na Mikopo ya wadau wa kibiashara ili kuiwezesha kampuni kuendelea kuwa kiongozi katika utoaji wa huduma bora na nafuu katika soko la Mawasiliano nchini.
Hivi karibuni, TTCL imezindua huduma za Mtandao wenye kasi zaidi wa 4G LTE na kuimarisha ubora wa huduma zake za data na sauti. Aidha, TTCL na Benki ya TIB zimeingia makubaliano ya mkopo wa fedha na dhamana za Benki utaoiwezesha TTCL kupata fedha dola za Marekali milioni 329 ili kuingiza mitambo mipya ya kisasa itayoboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma ya miala ya fedha kwa njia ya mtandao.
SHARE
No comments:
Post a Comment