Kampuni ya TBL Group mwishoni mwa wiki imewatunukia vyeti na zawadi wafanyakazi wake ambao wameitumikia kwa muda mrefu kwenye viwanda vilivyopo chini yake vya Konyagi,Chibuku na kampuni ya bia katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni wakati wa hafla hiyo Mkurugenzi wa Ufundi Gavin Van Wijk,aliwapongeza wafanyakazi hao kwa mchango wao mkubwa walioutoa katika mafanikio ya kampuni na kuwa na uvumilivu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali walizokutana nazo katika kipindi cha utumishi wao.
Alisema kampuni itaendelea kuwajali wafanyakazi wake na kuwajengea mazingira bora ya kufanya kazi “Tunaamini kuwa wafanyakazi wetu wote ni familia moja hivyo siku zote tutakuwa nao karibu na kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi na naamini sote tukishirikiana tutafanikiwa na kuendelea kupata mafanikio”.Alisema
Kwa upande wake Meneja wa TBL kiwanda cha Dar es Salaam,Calvin Martin alisema wafanyakazi hao ni mfano wa kuigwa na aliwataka wafanyakazi wengine wote hususani vijana ambao ni wengi kwenye kampuni kufanya kazi kwa bidii na kuwa wavumilivu na kuwa na utayari wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo sehemu za kazi.
“Tuko hapa kwa ajili ya kuwapongeza wenzetu ambao wamefikia sku hii ya leo ya kupewa tuzo ya utumishi wa muda mrefu,naamini sote tukifanya kazi kwa bidii na kuwa na uvumilivu wa kukabiliana na changamoto tunazokabiliana nazo kwenye kazi zetu za kila siku tutafanikiwa kufikia hatua kama waliyofikia wenzetu ambao tunawapongeza siku hii ya leo”.Alisema Martin.
Akiongea kwa niaba ya wafanyakazi wenzake waliotunukiwa vyeti kutokana na utumishi wa muda mrefu,Bw…Kunambi ambaye ametumikia kampuni kwa miaka 35 ,alisema siri kubwa ya utumishi wa muda kwenye kampuni ya TBL ni kutokana na mazingira bora ya kazi yaliyopo kwenye kampuni kwa kulinganisha na sehemu nyinginezo.
“Tunashukuru kampuni kwa kuthamini mchango wetu wa muda mrefu tulioitumikia,tumeanza kazi tukiwa vijana mpaka tumekuwa na umri mkubwa tukiwa tunaitumikia kampuni nah ii inatokana na mazingira bora ya kazi yaliyowekwa na mwajiri wetu na natoa wito kwa wafanyakazi wenzagu hasa vijana kufanya kazi kwa bidii na kuwa wavumilivu katika kazi zao ili malengo yao na malengo ya kampuni yaweze kutimia.
Zaidi ya wafanyakazi 25 waliotumikia kampuni katika kipindi cha miaka 10 mpaka miaka 35 walitunukiwa vyeti na zawadi.
SHARE








No comments:
Post a Comment