Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma.
Serikali
imetoa kauli kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuna chakula cha
kutosha pamoja na ziada ya asilimia 123. Ziada hiyo ya chakula inatokana
na uzalishaji wa msimu wa mazao mwaka 2015/2016 ambao unapelekea
upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba leo
mjini Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula
nchini.“Takwimu zinaonesha upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini ni
wa kuridhisha kwa kiwango cha utoshelevu wa ziada kwa asilimia 123” Dkt.
Tizeba.
Katika
kufafanua hali hiyo, Dkt. Tizeba amesema kuwa kulingana na takwimu
zilizopo hali ya upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini inautoshelevu
wa ziada kwa asilimia 123 ambapo nafaka ni asilimia 113 na mazao yasio
ya nafaka ni asilimia 140 ambapo viwango vya ziada kwa mazao yote ya
chakula ni tani 3,013,515.
Dkt.
Tizeba ameongeza kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA)
inauwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 246,000 ambapo kufikia Septemba 6,
ilikuwa na akiba ya tani 67,506.920 za chakula kinachojumuisha mahindi,
mpunga na mtama.
Pia
amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango wake wa kuiongezea NFRA uwezo
wa kuhifadhi chakula katika kanda sita baada ya kupata mkopo wa dola za
Kimarekani million 55 kutoka Serikali ya Poland ambazo zitatumika
kujenga vihenge vyenye uwezo wa kihifadhi tani 190,00 na maghala yenye
uwezo wa kuhifadhi tani 60,000.
Kuhusu
muda wa Serikali wa kutoa vibali vya kuuza chakula nje ya nchi, Dkt
Tizeba amesema kuwa lengo ni kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha
taarifa ya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa
mwaka 2015/2016 na hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Mbali na
hayo, Dkt Tizeba amesema kuwa katika kuboresha hali ya usalama wa
chakula nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
inapitia upya mfumo wa utoaji wa vibali vya kusafirisha chakula nje ya
nchi ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu kuliko ilivyo sasa.
Aidha,
Dkt. Tizeba amesema kuwa utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao nje
umejitokeza baada ya kuona chakula kinasafirishwa nje bila kufuata
utaratibu maalumu ambapo wafanyabiashara wa nchi jirani walijihusisha
kununua vyakula vikiwa bado mashambani kabla ya kuvunwa.
Aidha,
ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha kwa matumizi
katika kaya ambapo ameitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki katika
kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye uhaba.
Kuhusu
hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayoikabili dunia ikiwamo
upungufu wa mvua , Dkt Tizeba amesema kuwa Serikali itaendelea na juhudi
za kuhimiza na kupanua kilimo cha umwagiliaji mashambani kwa kuimarisha
miundombinu iliyopo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza uzalishaji
wa mazao wenye tija.
Hata
hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuelimisha wafanya biashara
kuuza unga nje ya nchi badala ya mahindi au mchele badala ya mpunga ili
kuendana na Sera ya kuendeleza Viwanda nchini na kuongeza thamani ya
mazao ya kilimo.(P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment