Katibu
Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Kamishna wa Mambo ya kigeni wa Umoja wa
Ulaya Federica Mogherini wameizuru Uturuki kwa mara ya kwanza tangu
jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15.
Awali
maafisa wa Uturuki waliwatuhumu washirika wao wa Magharibi kwa kushindwa
kuonyesha mshikamano kwa kuitembelea nchi hiyo baada ya jaribio la
baadhi ya wanajeshi kutaka kutwaa madaraka kwa nguvu, ambamo zaidi ya
watu 260 waliuawa.
NATO na
Umoja wa Ulaya walilaani haraka jaribio hilo la mapinduzi, lakini pia
waliionya Uturuki kuheshimu maadili ya kidemokrasia wakati wa
ukandamizaji dhidi ya watumishi wa kijeshi na umma ambao umehusisha
kukamatwa kwa maelfu ya watu.
Stoltenberg
alisema baada ya kukutana na rais Recep Tayyip Erdogan siku ya Ahamisi,
kwamba shambulizi dhidi ya demokrasia katika moja ya mataifa wanachama
wake ni shambulizi dhidi ya misingi ya muungano huo wa kijeshi.
Uturuki
ambayo ni mmoja wa wanachama 28 wa jumuiya ya NATO na ambayo imeomba kwa
muda mrefu kujiunga na Umoja wa Ulaya, inatoa mchango mkubwa katika
masuala ya kikanda, ukiwemo mgogoro nchini Syria - ambako hivi karibuni
ilianzisha mashambulizi ya ardhini, na pia katika wimbi la wakimbizi
wanaoingia barani Ulaya ambao wamesababishwa kwa sehemu kubwa zaidi na
vita vya nchini Syria.
EU, Uturuki waanza kujongeleana tena
Mwanadiplomasia
wa juu kabisaa wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, alizuru mjini
Ankara siku ya Ijumaa pamoja na Kamishna wa sera ya ujirani ya Umoja wa
Ulaya Johannes Hahn, alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki
Mevlut Cavusoglu na waziri wa masuala ya Ulaya Omer Celik.
"Tumeijadili
pia Syria. Kwa ufupi kabisaa: Tumekubaliana kwamba hakuwezi kuwapo na
suluhu ya kijeshi nchini Syria, kwamba suluhu ya kisiasa pekee na
serikali ya mpito ndiyo vinaweza kuleta amani nchini humo. Tumekubaliana
kushirikiana kujaribu kufikia usitishaji mapigano katika siku za
usoni," alisema Mogerini baada ya mkutano huo.
Uturuki yatoa mapendekezo mbadala
Wakati
huo huo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema anaamini Uturuki na
Umoja wa Ulaya wanaweza kufikia muafaka juu ya kuwaruhusu raia wa
Uturuki kusafiri katika Umoja wa Ulaya bila viza.
Mevlut
Cavusoglu amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Uturuki
imetoa mapendekezo mbadala na maelewano kati ya Ankara na Brussels
yalikuwa yanaaza kujitokeza.
Uturuki
imekuwa ikitaka kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa muda mrefu, lakini
imewatuhumu wazungu kwa kukwamisha mchakato huo kwa sababu ya chuki
dhidi ya taifa hilo la Kiislamu. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema
Uturuki bado haijatimiza masharti kuhusu haki za msingi na uhuru.DW
SHARE
No comments:
Post a Comment