Senpai Esther Thomas (kushoto) akipangua chudan tzuki (ngumi ya kifua) wakati semina hiyo ikiendelea.
Anafundisha kwa mifano! Shihan Okuma akishambuliwa na Jerome Sensei kama sehemu ya maelekezo katika semina hiyo.
Na Daniel Mbega
SEMINA
kubwa ya Shotokan Karate kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini,
imeanza leo hii jijini Dar es Salaam ambapo kwa mara ya kwanza katika
historia ya mchezo huo nchini Tanzania, inaongozwa na mkufunzi mkuu,
Shihan Koichiro Okuma (6th Dan), kutoka makao makuu ya chama cha karate
cha Japan Karate Association/World Federation (JKA/WF), Tokyo, Japan.
Semina
hiyo – maarufu kama JKA/WF- Tanzania Southern, Central & East
African Region Gasshuku – ambayo imeandaliwa na chama cha Japan Karate
Association/World Federation-Tanzania (JKA/WF-Tanzania) ni ya nane
kufanyika ambapo kwa mwaka huu inashirikisha makarateka 45 kutoka
Zimbabwe, Zambia, Uganda, Kenya na wenyeji Tanzania.
Kwa mujibu wa JKA/WF-Tanzania, semina hiyo ya wiki nzima inatarajiwa kufikia tamati Jumamosi.
Makarateka
ambao wameanza kushiriki leo hii, kutoka Tanzania ni Jerome Mhagama
Sensei, Justine Limwagu, Seberian Dagila, Said O. Kissailo, Lulangalila
Lyimma, Athumani Kambi, Mikidadi Kilindo Sensei, Marcus George, Khamis
K. Sambuki, Hamis Said Mkumbi, Selemani A. Mkalola, Christopher William,
Eliasa Mohammed, Adson Aroko Sensei, Nestory Federicko, Daniel Mbega,
Willy Ringo, Rwezaura Sensei, na Shihan Dudley Mawala Sensei, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa.
Makarateka
wengine na nchi zao kwenya mabano ni Gibson Sangweni (Zimbabwe), Robert
Chisanga (Zambia), Thobias B. Rudhal (Kenya), George Otieno (Kenya),
Joshua Oude (Kenya), George Warambo (Kenya), George Okeyo (Kenya),
Florence Kieti (Kenya), Asana Mahmoud Ulwona (Uganda), Ofubo Issa Yahaya
(Uganda), Magezi Yasiin (Uganda), Wanyika Abdurahman (Uganda), Frederic
Kilcher (Ufaransa) na Koichiro Okuma (Japan).
Mkufunzi mkuu wa JKA/WF-Tanzania, Jerome George Mhagama Sensei (5th Dan), amesema hata hivyo kwamba, tofauti na miaka iliyotangulia,
safari hii hakutakuwa na mashindano ili kutoa fursa kubwa kwa Shihan
Okuma kufundisha vyema na kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali
kuanzia ngazi ya Sho-Dan, Ni-Dan, San-Dan na Yon-Dan (1st – 4th Dan).
“Tunataka
tupate muda wa kutosha wa kufanya semina pamoja na mitihani, kwani
mbali ya kuwapandisha madaraja makarateka mbalimbali, lakini pia kuna
ambao watafanya mitihani ya ukufunzi na uamuzi wa kimataifa ili kupanua
wigo na kupata walimu na waamuzi wa kutosha katika kanda yetu,” amesema
Jerome Sensei, ambaye alipanda daraja Jumanne, Septemba 6, 2016 baada
ya kufanya vizuri na kufaulu mtihani wa 5th Dan jijini Nairobi, Kenya chini ya Shihan Okuma.
Hata
hivyo, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kesho ambapo makarateka kutoka
Zanzibar nao watahudhuria baada ya kushindwa leo kutokana na sababu
mbalimbali.
Jerome
Sensei amesema kwamba, changamoto kubwa ambayo inawakabili wao pamoja na
mchezo mzima wa Karate nchini Tanzania ni kuwekwa pembeni na wadau
mbalimbali wa michezo ikilinganishwa na michezo mingine, hali ambayo
imekuwa vigumu kwao kupata udhamini.
Ameiomba
Serikali na wadau wengine kuutupia macho mchezo huo, kwani unailetea
sifa kubwa Tanzania kutokana na mafanikio ya mchezaji mmoja mmoja.
Katika
kipindi cha miaka takriban 10, Tanzania imekuwa kinara wa mchezo wa
Karate katika kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini ukitoa Afrika
Kusini pekee, hatua ambayo imechangiwa na mafanikio binafsi ya Jerome
Sensei, ambaye kwa jitihada zake ameshiriki mashindano ya dunia ya
Karate mwaka 2012 na kurudia raundi ya nne, mashindano ambayo
yalifanyika Pataya, Thailand, ambapo alitolewa na mtu ambaye alikuja
kuwa bingwa wa dunia.
Mbali ya
hivyo, ameshiriki mashindano mengine jijini Tokyo, Japan lakini pamoja
na kutotwaa ubingwa, ameweza kupanda madaraja kwa viwango vya kimataifa
na sasa ni mkufunzi, mtahini na mwamuzi wa kimataifa, ambapo ameweka
rekodi ya pekee kwa kuwa mkufunzi mwenye umri mdogo kabisa katika
historia ya JKA/WF tangu chama hicho kilipoanzishwa Mei 1947.
Kwa mujibu wa rekodi za JKA/WF, Jerome Sensei (36) ni karateka wa pili wa Afrika Mashariki kuwa na hadhi ya Dan Tano (5th Dan) baada ya David Mulwa Sensei wa Kenya, hivyo ameteuliwa kuwa mkufunzi mwenza mkuu wa Afrika Mashariki.
Akizungumza
katika ufunguzi huo, Shihan Okuma, ambaye ametokea Kenya ambako
kulikuwa na semina wiki iliyopita, amesema kuwa ujio wake siyo wa bahati
mbaya bali umetokana na jitihada ambazo Tanzania imekuwa ikionyesha
katika maendeleo ya Karate, hususan mafanikio yasiyo na kifani ya Jerome
Sensei.
“Nimetumwa
na makao makuu kuja kuiunga mkono Tanzania pamoja na kufundisha semina
hii, najua semina kama hii mara nyingi huwa inafanyika makao makuu tu au
katika kanda maalum, lakini kwa vile Tanzania imeonyesha mafanikio
makubwa, hatuna budi kuja hapa ili kuwapa fursa makarateka wengi waweze
kushiriki.
“Kuja
Japan ni gharama kubwa, wengi hawawezi kumudu pamoja na kuwa na nia na
mchezo huu, ni wachache tu ambao wanapata bahati ya kuja kuhudhuria,
lakini hapa nimefurahi kuona kuna makarateka wengi wana viwango vya juu
kabisa na hii ni faraja kubwa kwangu na kwa JKA/WF,” amesema. (P.T)
SHARE
No comments:
Post a Comment