Na Salum Vuai, MAELEZO
KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Asha Ali Abdallah, leo amefungua
mkutano wa pili wa kamati za kusimamia chanjo na matumizi ya dawa barani
Afrika na kutahadharisha changamoto zinazotokana na kuibuka kwa dawa
zilizo chini ya kiwango.
Katika
mkutano huo wa siku tano unaofanyika kwenye hoteli ya Zanzibar Ocean
View Kilimani mjini Unguja, Katibu Mkuu huyo alisema nchi za Afrika
zinakabiliwa na changamoto kadhaa katika kusimamia na kusajili dawa.
Alisema baadhi ya changamoto hizo zinahitaji kuelezwa na kuchukuliwa
kama suala la dharura.
Asha
alieleza kuwa, dawa bandia na chanjo, uendeshaji wa kliniki zilizo chini
ya kiwango na usimamizi mdogo wa sheria na miongozo juu ya matumizi ya
dawa, yanahitaji kuwekewa mikakati maalumu ili kuweza kutoa huduma bora
za chanjo katika nchi za Afrika.
“Ikiwa
mamlaka ya usimamizi, AVAREF ina kazi kubwa kuhakikisha usalama wa
chanjo, kuepuka urasimu na ucheleweshaji ambao unaweza kuwakosesha
huduma wananchi wengi,” alisisitiza.
Alisema
katika kuhakikisha ubora na usalama wa chanjo na dawa mbalimbali katika
soko, Zanzibar iliamua kuanzisha Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi
(ZFDB) mwaka 2007.
Alizitaja
kazi za bodi hiyo kuwa ni kuratibu, kusajili na kufuatilia usalama wa
dawa, bidhaa za chakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria namba 2 ya
mwaka 2006 inayohusu bidhaa hizo.
Aliwahakikishia
wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea
kushirikiana na kamati hizo ikitambua umuhimu wa kuwapatia wananchi
huduma bora za afya kwa kusimamia utoaji wa chanjo na dawa zilizo
sahihi.
Mapema,
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) anayefanya kazi hapa
Zanzibar Dk. AndeMichael Ghirmay, alisema katika miaka hii, nchi za
Afrika zimekuwa zikiathirika kwa maradhi yanayoambukiza na yale
yasiyoambukiza, mengi kati yao yakiwa hayana dawa wala chanjo.
“Zikisukumwa
na mahitaji ya dawa na chanjo zilizo bora, ya haraka na rahisi, nchi za
Afrika zinazidi kuwa shabaha ya wamiliki wa viwanda vya dawa katika
mkakati wao wa kuendeleza dawa na chanji mpya,” alisema.
Hata
hivyo, alisema mfumo wa utengenezaji na utumiaji wa dawa na chanjo hizo,
bado ni changamoto kwa kamati za maadili na usimamizi, katika
kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa.
Kutokana
na sababu hizo, Dk. Ghirmay alisema mnamo mwaka 2006, WHO iliunda
chombo cha kuratibu na kusimamia mfumo wa utoaji dawa na chanjo (AVAREF)
ili kuchochea maendeleo na ufanisi katika suala hilo.
Mkutano
huo unashirikisha zaidi ya wajumbe 40 kutoka nchi mbalimbali za Afrika,
pamoja na wawakilishi wa Mamlaka za Mashirikisho ya Dawa (FDA) kutoka
Marekani na Canada, sambamba na wataalamu na wadau wa masuala ya chanjo
na dawa kutoka taasisi tofauti barani Afrika.
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla akifungua mkutano wa
siku tano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika unaofanyika
katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Mwakilishi
wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmay
akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo na kuelezea juu ya majukumu ya
kamati hizo.
Mwakilishi
wa (WHO-AFRO) Dicky Akanmoni akiwasilisha mada juu ya usimamizi wa
matumizi sahihi ya dawa katika mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo
barani Afrika ulioanza leo Februari 20, 2017 mjini Zanzibar.
Baadhi
ya wajumbe wa mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika
wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika siku ya kwanza ya mkutano huo.
Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Ali Abdalla (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa kamati za usimamizi wa
chanjo barani Afrika unaofanyika Zanzibar.
Mkurungezi
Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa chanjo na matumizi
ya dawa kando ya mkutano wa kamati za usimamizi wa chanjo barani Afrika
ulioanza leo Februari 20, 2017 katika hoteli ya Zanzibar Ocean View.Picha na Makame Mshenga-Maelezo.
SHARE
No comments:
Post a Comment