Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya
Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema (katikati) akisisitiza jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitangaza tarehe ya
uzinduzi wa bodi mpya ya parole taifa tarehe 3 na 4 Machi 2017 mapema
hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Msaidizi wake Bw. Clemence
Munisi na kulia ni Mkewe Bi. Rose Augustino Mrema.
………………………………………………………………………..
Na Eliphace Marwa -Maelezo
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya
Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema amemshukuru Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha
safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya
yake.
Dkt. Mrema ametoa kauli hiyo leo
jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waaandishi wa habari kuhusu
uteuzi uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu
Lameck Nchemba kwa kuwateua wajumbe wawili wa bodi hiyo.
“Nachukua nafasi hii kumshukuru
Rais Magufuli , Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Wizara ya
Afya na Ikulu, kwa kunipeleka nchini India kufanyiwa uchunguzi wa afya
yangu na kupatiwa matibabu na sasa afya yangu imeimarika na niko tayari
kutekeleza majukumu yangu”, alisema Dkt. Mrema.
Akizungumzia uteuzi uliofanywa na
Waziri Nchemba, Mrema amesema kuwa toka alivyoteuliwa na Rais Magufuli
kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi hiyo haikukaa vikao
kutokana na baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo kumaliza muda wao.
“Nilipoteuliwa na Rais kuwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi ilikuwa bado haijakutana na
kufanya vikao kwasababu kuna wajumbe walikuwa wamemaliza muda wao na
Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa bado hajateua wajumbe wengine lakini
kwa sasa amakwisha fanya kazi ya uteuzi”, alisema Dkt. Mrema.
Mrema aliwataja walioteuliwa kuwa
wajumbe wa Bodi ya Parole Taifa ni pamoja na Bwana Francis Kistola na
Bwana John William Nyoka.
Aidha Mrema amempongeza Waziri wa
Mambo ya Ndani kwa kukamilisha kazi ya uteuzi na amewapongeza wajumbe
walioteuliwa na kuwakaribisha kwa mikono miwili kwenye bodi hiyo na
kuomba ushirikiano wao na uzoefu wao ili kukamilisha majukumu ya bodi ya
Parole.
Vilevile Mrema amesema kuwa kikao
cha kwanza cha bodi mpya ya parole kitafanyika tarehe 3 na 4 Machi 2017
jijini Dar es Salaam na bodi hiyo mpya itazinduliwa siku hiyo na Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Nchemba.
SHARE
No comments:
Post a Comment