NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
Tatizo la ongezeko la idadi ya
vijana na watu wazima waliokosa elimu ya sekondari ni kubwa sio tu hapa
Tanzania bali ni kwa nchi zote za kusini mwa jangwa la sahara, Kwa
mfano, kwa takwimu za sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina jumla ya vijana
wa umri wa miaka 7-17 milioni 3.5 ambao wapo nje ya mfumo rasmi wa
elimu.
Hii hufanya vijana milioni 2.5
kuhitaji elimu ya sekondari na wengine milioni 1 kuhitaji elimu ya
msingi na ukweli ni kwamba vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata
alama za ufaulu chini ya 100 (kati ya 250) wamekuwa wakiachwa bila
kwenda sekondari katika Mikoa mbalimbali isipokuwa wale ambao
wazazi/walezi wao wanauwezo wa kuwapeleka kwenye shule za sekondari za
binafsi ambazo gharama zake ni za juu.
Takwimu za sensa ya mwaka 2012
zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2015 idadi ya vijana walio nje ya shule
itaongezeka kufikia milioni 5.
Ili kukabiliana na tatizo hili,
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzisha programu ya elimu ya
sekondari nje ya mfumo rasmi mwaka 1992 ili kutoa fursa ya elimu ya
sekondari kwa vijana na watu wazima waliokosa nafasi ya kuendelea na
elimu ya sekondari kwa sababu mbalimbali.
akiongea kuhusu programu hiyo
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima Dkt.Kassim Nihuki
alisema Programu inawalenga wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao
hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na wale ambao kwa
sababu moja au nyingine hawakumaliza elimu ya sekondari na wanataka
kumaliza elimu hiyo.
Dkt. Nihuki aliongeza kuwa
programu hii pia inawalenga wanafunzi ambao wamemaliza masomo ya MEMKWA
(mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa) na wale wamemaliza masomo ya
sekondari lakini hawakufanya vizuri na wangependa kurudia mtihani wa
Taifa wa kidato cha nne pamoja na wafanyakazi wa serikali na sekta
binafsi ambao hawana elimu ya sekondari na wanatakiwa wawe na kiwango
hicho cha elimu.
Dkt Nihuki anasema kuwa masomo
katika programu hii yanatolewa katika hatua tatu kubwa ikiwa hatua ya
kwanza inabeba masomo ya kidato cha kwanza na chapili huku hatua ya
tatu ikibeba masomo ya kidato cha tatu na nne na hatua ya tatu inabeba
masomo ya kidato cha tano na sita.
Naye Mkuu wa Idara ya Elimu Msafa
Bw. Baraka Kionywaki amesema kuwa Katika hatua ya I, mlengwa anasoma
kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa
maarifa (yaani “Qualifying test”).
Bw. Kionywaki aliongeza
kuwa jumla ya masomo 7 ya lazima yanayotolewa katika hatua hii ambayo
ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na
Uraia (Civics). Aidha, mlengwa anaweza kuchagua masomo ya ziada ya
sayansi au biashara kwa kadri atakavyoona inafaa. Mlengwa wa hatua ya
II anasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na hivyo kuwa na sifa ya
kufanya mtihani wa kidato cha nne unaoandaliwa na Baraza la Mitihani la
Taifa (NECTA).
Katika hatua ya tatu mlengwa
atasoma kwa kipindi cha mwaka mwingine mmoja na hivyo kuwa na sifa ya
kufanya mtihani wa kidato cha sita unaoandaliwa na NECTA. Ambapo katika
hatua hii, masomo yanatolewa katika tahasusi (“combinations”)
za HGL (Historia, Jiografia na Lugha), HKL (Historia, Kiswahili na
Lugha), HGK (Historia, Jiografia na Kiswahili) na HGE (Historia,
Jiografia na Uchumi). Hata hivyo mlengwa katika kila hatua anaweza
kusoma kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi pale atakapokuwa amejiandaa kiasi
cha kutosha kufanya mtihani wa maarifa au ule wa NECTA.
Katika hatua zote, masomo yanatolewa kupitia mafunzo ya ana kwa ana ya jioni (evening programme)
kuanzia saa 9 alasiri hadi saa 12 jioni pamoja na kujisomea moduli na
vitabu na matumizi ya teknolojia za kujifunzia kama vile “CDs” na elimu
mtandao (e-learning) yakiwemo machapisho huria ya kielimu (open educational resources).
Programu hii ambayo inaendeshwa
katika majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali 83 na shule
za wadau mbalimbali 337 nchini zimewanufaisha vijana na watu wazima
95,140 (wanawake 61049 na wanaume 44893) katika mikoa mbalimbali kwa
kipindi cha tangu mwaka 2010 hadi 2016.
Vijana na watu wazima wana budi
kuendela kutumia fursa hii ili kuweza kupata elimu ya sekondari pamoja
na kuziomba mamlaka za serikali za mitaa kuwahimiza wazazi/walezi
kuwapeleka vijana wao waliokosa alama za ufaulu katika mtihani wa darasa
la saba kutumia fursa ya elimu kupitia Taasisis ya Elimu ya Watu Wazima
SHARE
No comments:
Post a Comment