TRA

TRA

Sunday, February 26, 2017

UTOAJI TAARIFA ZA MIRADI YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMMA UNAVYOSAIDIA KUPAMBANA NA RUSHWA

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika  ujenzi wa miundombinu ya Umma  kwani ni muhimu kuwa na miundombinu mizuri na bora ili kutoa huduma bora na kurahisisha ufanyaji kazi hivyo kuharakisha maendeleo ya nchi katika nyanja zote muhimu zikiwemo za biashara, utalii na mawasiliano.

Matumizi makubwa ya fedha za Serikali yanatumika katika ujenzi wa miundombinu ya Umma ambapo matumizi hayo yanahusisha karibu asilimia 53 ya Bajeti nzima ya nchi.

Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Umma inayoelezewa hapa ni ile ambayo inajengwa kwa fedha za Serikali kwa ajili ya matumizi ya wananchi wote ikiwemo ya barabara, hospitali na vituo vya afya,shule na vyuo,nyumba za kuishi pamoja na ofisi mbalimbali. 

Ingawa Serikali inajitahidi kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu bora itakayochochea maendeleo, lakini jitihada hizo zimekuwa zikikwamishwa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza pindi mradi husika unavyoanza kwani wahusika hawatumii fedha kama zilivyopangwa na badala yake wanafanya kwa makadirio ya chini na kufanya ujenzi kutokuwa imara.

Hali hiyo inasababisha Serikali kupata hasara kwa kupoteza fedha nyingi na kuambulia kubaki na majengo yasiyo na viwango ambayo mwisho wake hushindwa kutumika na kuilazimu Serikali kuanza upya ujenzi husika. 

Kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na imejipanga kuhakikisha nchi inafika katika uchumi wa kati basi mambo hayo hayana nafasi na hayawezi kutokea tena katika nchi hii watu kuachiwa huru kutumia vibaya fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. 

Kwa kuhakikisha hilo,Serikali kupitia Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) chini ya Mkakati wa Kukuza Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Ujenzi Tanzania (CoST-Tanzania) imejipanga kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika sekta hiyo ili kuondokana na rushwa pamoja na ubadhilifu wowote wa fedha za Umma zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Mkakati huo unalengo la kupambana na rushwa, usimamizi mbaya katika ujenzi pamoja na changamoto zingine zinazopelekea ubadhilifu wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miundombinu ya Umma kwa kukusanya taarifa za miradi hiyo ya ujenzi ili  kuhakikisha kama thamani ya miundombinu iliyojengwa inalingana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi husika. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,(Ujenzi), Mha. Joseph Nyamuhanga alikaririwa akisema kuwa “Sekta ya Ujenzi ni sekta moja wapo inayoonekana kukithiri kwa rushwa duniani kwa sababu takribani asilimia 10 hadi 30 ya Bajeti yake inapotea kwa njia ya rushwa na usimamizi mbaya hivyo ili kuondoa dhima hii ni lazima kukusanya na kutoa taarifa kwa wananchi juu ya ujenzi wa miundombinu hiyo”.

Mha. Nyamuhanga aliongeza kuwa ni muhimu CoST-Tanzania ikapewa hadhi ya kujitegemea na kuwa na madaraka yake kwani ni kitengo ambacho ni muhimu na kinafanya kazi kubwa ya kuchochea uwepo wa uwazi na uwajibikaji katika miradi ya ujenzi.

Akifungua mkutano wa wadau wa ujenzi kutoka nchi mbalimbali uliofanyika Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchukuzi), Mha. Leonard Chamuriho alisema rushwa inazungumzwa sana katika suala la ujenzi wa miundombinu ya umma hivyo huu ni wakati wa kuweka wazi taarifa za ujenzi wa miundombinu hiyo ili wananchi waelewe kinachoendelea katika miradi inayotumia fedha zao.

Aliongeza kuwa kufanya hivyo kutaisaidia Serikali kupambana na rushwa na hivyo kufuta kabisa taswira ya rushwa katika miradi hiyo kwani msimamo wa Serikali ni kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa.

Maendeleo ya nchi yanachangiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya ukusanyaji wa kodi na ushuru mbalimbali hivyo hata miundombinu ya umma inajengwa kwa kutumia fedha za wananchi zinazopatikana kwa njia ya ukusanyaji mapato.

Hivyo, ili kuifanya Serikali kuwa na taswira nzuri kwa wananchi wao pamoja na kuwafanya wananchi kuiamini Serikali yao ni vizuri kuwapa taarifa juu ya matumizi ya fedha hizo wanazozikusanya.

Kuwapa taarifa wananchi juu ya miradi mbalimbali haswa ya ujenzi wa miundombinu kutaamsha ile hali ya watu kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa sababu watajua matumizi ya fedha wanazozikusanya.

Taarifa hizo pia zitaendeleza uwajibikaji na uwazi katika ujenzi wa miundombinu hiyo hivyo kupunguza vitendo vya rushwa,kujenga miundombinu inayoendana na thamani ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi husika pamoja na kujenga miundo mbinu bora na imara.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki amesema kuwa shughuli inayofanywa na CoST- Tanzania inalenga kuimarisha uwazi katika sekta ya ujenzi kwa kutoa taarifa juu ya ujenzi wa miundombinu ya Umma kitu ambacho kitasaidia kutambua uwezo, akiba pamoja na ufanisi wa majengo hayo.
"Kazi inayofanywa na CoST- Tanzania ni fursa kwa Serikali na Umma kwa ujumla kufuatilia jinsi fedha za Umma zinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ambapo ukweli na uwazi wa taarifa zinazokusanywa zitasaidia katika kupunguza rushwa na kuboresha usimamizi wa miundombinu hiyo, " alisema Waziri Kairuki.
Nae Mwenyekiti wa CoST-Tanzania, Mha. Kazungu Magili alieleza kuwa utoaji wa taarifa hizo kwa Umma kuhusiana na miradi ya ujenzi ya Umma itaruhusu umma kujua hali ya miradi mbalimbali hivyo kuifanya Serikali kuwa na sifa nzuri mbele ya wananchi.
CoST-Tanzania imejipanga kufanya tathmini ya miradi ya ujenzi isiyopungua kumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja, majengo yaliyojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) hasa ujenzi mpya wa hosteli  za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia majengo yanayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF ) pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ni muhimu kwa Serikali kupitia miradi yote iliyojengwa na inayoendelea kujengwa kwa kutumia fedha za Umma ili kugundua thamani halisi ya majengo hayo na kutoa taarifa kwa wananchi.

Jambo hili pia litasaidia vyombo husika vya kisheria kuwachukulia hatua watu wote walioshiriki kutumia vibaya fedha za wananchi kwa kujenga miundombinu iliyo chini ya kiwango au isiyoendana na thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya ujenzi husika.

BAADA YA MIAKA 53 HATIMAYE WANANCHI WA MTAA WA IGUNGANDEMBWE MANISPAA YA IRINGA WAPATA MAJI SAFI NA SALAMA

Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) akikinga maji kwenye ndoo kuashiria sasa kisima cha maji kimefunguliwa na kuanza kutumia kwa wakazi wa mtaa wa Igungandembwe manispaa ya Iringa akiwa na diwani wa kata ya Nduli Bashir Mtove wakati wa uzinduzi wa kisima hicho.
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalam wa kujimba visima ambaye pia ndiye aliyechimba kisima hicho. 
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) akiangalia maji waliyokuwa wanatumia wananchi mtaa wa Igungandembwe manispaa ya Iringa.
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) akiangalia maji waliyokuwa wakitumia wananchi wa mtaa huo
Na haya ndio maji waliyokuwa wanatumia wananchiwa mtaa wa Igungandembwe manispaa ya iringa kabla ya kujimbiwa kisima 


Na Fredy Mgunda,Iringa.
Wananchi wa mtaa wa Igungandembwe manispaa ya iringa wamemshukuru mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) na diwani wa kata ya Nduli Bashir Mtove kwa msaada wa kuwachimbia kisima cha maji safi na salama.
Wakizungumza na blog hii wananchi hao wamesema kuwa wanatakribani miaka hamsini na tatu (53) hawajawahi pata maji masafi na salama.
“Angalia maji haya machafu ndio tulikuwa tunakunywa na kupikia ila mungu alikuwa anatusaidia tu kutuepusha na magonjwa mbalimbali kiukweli leo tunafuraha sana kuanza kutumia haya maji na ndio maana unaona wananchi wanafuraha nawameanza kunywa maji hapa hapa kwenye kisima hiki kwa kuwa bado hawaamini kilichotokea”,walisema wananchi.
Wananchi wao wamemuomba mbunge Ritta kabati na Diwani wa kata ya nduli Bashir Mtove kuendelea kutatua changamoto za wananchi kwa kuwa walichaguliwa na wananchi kwa lengo la kuwatumikia.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Iringa Ritta Kabati kupitia chama cha mapinduzi (CCM) alisema kuwa wataendelea kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa kuwa yeye ni mbunge wa wananchi wote bila kubagua vyama.
Kabati alisema kuwa ataendelea kuwachimbia visima na kukarabati majengo ya shule zilizochakaa katika mkoa wa Iringa kwa kuwa yeye ni mbunge wa mkoa wa Iringa hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kuiamini serikali ya chama cha mapinduzi kwa kazi kubwa wanayoifanya kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli.
“Hivi hamuoni nimeamua kufika huku ambako hata viongozi wengi hawajafika ila mimi nimekuja nimewaleta kisima na maji safi na nitaendelea kuja kutatua matatizo ya mtaa huu kwa kuwa tumetumwa na Rais kufanya kazi kwa wananchi wa chini ndio maana hata mimi nimeanza kufanya kazi huku mbali japo kuwa ndio jadi yangu kuwatumikia sana wananchi wa chini sasa naombeni mniunge mkono katika juhudi zangu za kuwaletea mandeleo”.alisema Kabati
Aidha Kabati alisema kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuleta maendeleo kuanzia huku chini kupanda juu hivyo tufanye kazi kwa kujituma ili tuende sambamba na kasi ya Rais wetu.
Naye Diwani wa kata ya nduli Bashir Mtove alimshukuru mbunge huyo kwa jihada zake za kuleta maendeleo na kumuomba kushugulikia changamoto alizozitoa kwa wananchi ili kuendelea kujijengea imani kwa wananchi wa kata hiyo.Mtove aliongeza kuwa atahakikisha kata yake inamaliza tatizo la maji ambao limetumu kwa miaka mingi hivyo wananchi wanatakiwa kufanya kazi kwa kujituma ili kukuza uchumi wa kata hiyo.
“Angalia hadi saizi tumechimba visima zaidi ya sita kwenye kata yangu japo bado sana kumaliza tatizo hili la maji hivyo naendelea kujituma kutafuta marafiki,wafadhili na kumshirikisha mbunge Kabati kusaidia kutatua tatizo la maji na changamoto nyingi ili wananchi wangu wafanye kazi kwa kujituma bila kuwa na vikwazo vyovyote vile vya kiafya”.alisema Mtove.

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger