Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari jana jioni amekutana
na wanafunzi wa kike 82 wa Chibok walioachiliwa huru na kundi la itikadi
kali la Boko Haram.
Kisha baadaye Rais Buhari aliondoka nchini humo kuelekea London,
Uingereza kwa kile ofisi yake imesema kuwa ni kufanyiwa vipimo zaidi vya
matibabu.Wasichana, waliochukuliwa mateka kutoka shuleni mwao katika mji wa kaskazini mashariki wa Chibok zaidi ya miaka mitatu iliyopita, walipokelewa na Buhari pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu serikalini.
Picha zilizotolewa na serikali zilimwonesha rais ambaye mwili wake umepungua, akiwahutubia wasichana hao katika makaazi yake rasmi jana jioni "Nina furaha sana kukutana nanyi binafsi na nawahakikishia kuwa ofisi ya rais itasimamia utendaji kazi wa wale waliopewa majukumu ya kusimamia huduma za kijamii zinazotolewa na serikali kuu".
Rais ameahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha kuwa watu wengine wote waliochukuliwa mateka na Boko Haram watapata uhuru wao hivi karibuni. Mapema jana, wasichana hao walifanyiwa vipimo vya kiafya.
Mkurugenzi wa Matibabu katika Idara ya Huduma za Serikali Anne Okorafor amesema wengi wao walikuwa katika hali nzuri.
"Tutafanya kila tuwezalo, kama tu ilivyokuwa kwa wasichana wengine. Hivyo mko kwenye mikono salama kabisa na hakuna haja ya yeyote kuwa na hofu".
Serikali ya Nigeria ilifanya mazungumzo ya kuachiwa kwao pamoja na serikali ya Uswisi, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ndani na nje ya Nigeria.
Aleksandra Mosimann, ni msemaji wa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu "Kando na kundi la Chibok kuna watoto wengine huko, maelfu ambao hawajakutana na familia zao leo kwa sababu ya mzozo wa kivita ambao unaendelea kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Pia wanastahili kuungana tena na familia zao na natumai familia nyingi zaidi zitapata habari njema kama walizopata leo familia za wasichana 82"
Afisa mmoja wa serikali ya Nigeria amesema makamanda watano wa Boko Haram waliachiliwa huru kwa kubadilishana na wasichana hao. Lakini hakuna maelezo kamili yaliyotoka kwa serikali wala Boko Haram.
Baadhi ya wazazi walishangilia katika mji mkuu Abuja kuwaachiwa kwa wasichana hao, wakati wengine walielezea wasiwasi wao kuhusiana na hatima ya wasichana wengine 113 wasiojulikana waliko baada ya kutekwa kutoka shule moja ya Chibok mwaka wa 2014.
Mwaka jana, kundi la kwanza la wasichana 21 wa CHIBOK waliachiwa mwezi Oktoba, na wamekuwa wakitunzwa na serikali na kupewa huduma za matibabu, ushauri nasaha kuondoa kiwewe, na kurekebishwa hali zao. Mashirika ya haki za binaadamu yanakosoa hatua ya kuwaweka wasichana hao kizuzini mjini Abuja.
Dakika chache baada ya kukutana na wasichana hao, Rais Buhari ambaye ana umri wa miaka 74, alilishangaza taifa kwa kutangaza habari kuwa anaondoka usiku kuelekea London kwa ajili ya matibabu zaidi.
Buhari ambaye hajaweza kuhudhuria mikutano ya baraza lake la mawaziri kwa wiki tatu mfululizo, alikuwa jijini London kwa mwezi mmoja na nusu mapema mwaka huu. Mpaka sasa hakuna maelezo kuhusu ugonjwa unaomsumbua rais huyo.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment