ULAJI wa nyama choma na chipsi umetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu
zinazochochea watu wengi hasa vijana kupata shinikizo la juu la damu.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa
Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Pedro Pallangyo,
alipozungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili.
Dk. Pallangyo alisema vyakula hivyo huchochea hali hiyo kutokana na
matumizi makubwa ya mafuta yanayotumika kuviandaa na chumvi nyingi
inayotumika wakati wa kula.
“Jinsi vyakula hivyo vinavyoandaliwa mafuta mengi hutumika na wakati wa
kula watu hupendelea kuweka chumvi nyingi, jambo ambalo ni kosa. Ulaji
huu si mzuri kiafya,” alisema.
Dk. Pallangyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa JKCI
alisema katika miaka ya nyuma idadi kubwa ya watu katika nchi
zilizoendelea ndiyo walikuwa wakipata tatizo hilo lakini sasa idadi
kubwa inagundulika katika nchi zinazoendelea.
Alisema mbaya zaidi watu wanaokutwa na tatizo katika nchi zinazoendelea ni wale walio katika umri wa uzalishaji.
“Katika nchi zilizoendelea wastani wa umri wa watu wanaokutwa shinikizo
la damu ni wale walio juu ya umri wa miaka juu ya 50 na kuendelea.
“Lakini kwa upande wa nchi zinazoendelea, hasa zilizopo Kusini mwa
Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo, picha ni tofauti. Huku wanaokutwa
na tatizo ni wenye umri wa miaka 35 hadi 45, yaani kwa wenzetu ugonjwa
huu unajulikana kwamba ni wa watu wazima huku kwetu ni ugonjwa wa
vijana,” alisema.
Pia alisema tafiti zinaonesha magonjwa ya moyo yanachangia theluthi moja
ya vifo vyote vinavyotokea duniani na zaidi ya asilimia 50 ya vifo
hivyo vinatokana na shinikizo la juu la damu.
“Utafiti mmoja uliowahi kufanywa katika nchi 23 Barani Afrika, Tanzania
ikiwamo ulionesha shinikizo la damu ni sababu ya moyo kushindwa kufanya
kazi na kusababisha vifo vya ghafla,” alisema.
Dk. Pallangyo alisema katika nchi hizo ilionekana asilimia 86 ya magonjwa yote ya moyo yanatoka na shinikizo la damu.
“Hapa JKCI kwa miaka mitatu iliyopita tumeweza kufanya utafiti
mbalimbali, utafiti huo ulihusisha watu waliopo kwenye jamii na wagonjwa
waliolazwa wodini, kwenye jamii asilimia kati ya 42 hadi 56 ya wagonjwa
wote tuliowapima walikutwa na shinikizo la juu la damu.
“Asilimia 35 hadi 47 ya wagonjwa waliokuwa wodini wengi mioyo yao
ilikuwa imeshindwa kufanya kazi na kusababisha shinikizo la damu,”
alisema.
NA VERONICA ROMWALD – MTANZANIA DAR ES SALAAM-
SHARE
No comments:
Post a Comment