Julian Msacky
NCHI nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania zilikubali soko
huria bila kujua madhara yake kwa nchi na watu wake.
Zilikimbilia kupokea mfumo huo kwa nderemo na vifijo ili kufurahisha
mataifa makubwa na leo hii kila mtu analia.
Soko huria (free market) linachoangalia ni kuchuma tu faida
na kumuacha mwananchi akichuruzika jasho la damu.
Ukweli uliopo ni kuwa mara nyingi penye soko hilo Serikali
haina cha kufanya bali huangalia raia wake wakiteseka tu.
Hii ikiwa na maana kuwa haina nguvu za kuamua bidhaa ziuzwe
namna gani kwa sababu nguvu zipo kwa wafanyabiashara.
Ndiyo maana leo hii bidhaa zinapanda kiholela na serikali
inangalia tu kwa sababu za nguvu za soko huria.
Angalia namna unga wa mahindi ulivyopanda. Angalia bei ya
sukari isivyoshikika. Ni shida kweli kweli.
Pamoja na kwamba tupo kwenye soko huria ambalo halina rafiki
ni muda wa serikali kuingilia kati.
Serikali ni lazima ifanyie hivyo ili kulinda wananchi wake na
si kuwaachia tu wafanyabiashara waamue watakavyo.
Isipofanya hivyo mwananchi atabaki mtu wa kubebeshwa mzigo
mzito hata kama hana uwezo wa kuufikisha panapotakiwa.
Wakati akiumia wafanyabiashara wanazidi wanakenua tu hasa wa
bidhaa za nyumbani kwani wamepata mahali pa kupandia.
Hebu tujiulize kama kilo moja ya sukari inanunuliwa hadi
2,800 tunamtakia heri mwananchi?
Nimemsikia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema sukari ipo ya
kutosha na kwamba wananchi wasiwe na hofu yoyote.
Ni sawa kabisa. Sukari ipo ya kutosha, lakini wananchi wenye
uwezo wa kuinunua ni wachache mno.
Leo hii kunywa chai inamlazimu mwananchi afikirie mara mbili
mbili kwa sababu ya bei kubwa ya sukari.
Huenda ni kwa sababu hiyo wimbi la vijiwe vya kuuza kahawa
vinazidi kuongezeka kila kukicha mijini.
Badala ya mtu kunywa chai nyumbani na familia anakimbilia
kijiwe cha kahawa kupata ya sh. 100 pamoja na kashata.
Kuna umuhimu wa serikali kuangalia kwa umakini suala hili
kwani linaathiri maisha ya watu wengi hasa wa kipato kidogo.
Tunafahamu unga wa mahindi ndiyo kimbilio la wengi. Unga huo
ndiyo hutumika kutengenezea watoto uji.
Kama na wenyewe utashindikana mbona familia zitakuwa kwenye
wakati mgumu.
Zipo taarifa kuwa baadhi ya wanaume wameanza kukimbia familia
zao.
Waziri wa viwanda, Charles Mwijage
Sababu kubwa ni maisha kuwa magumu.
Hata kama tunajenga uchumi imara ni lazima tuhakikishe ustawi
wa maisha ya watu wetu yanakuwa na uahueni.
Kuwa na uchumi usiogusa maisha ya watu wa kawaida ni tatizo.
Uchumi ukiimarika maisha ya watu nayo yaimarike.
Vinginevyo itakuwa vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuamiani uchumi
wa nchi yake unakuwa kwa kasi kubwa.
Hii ikiwa na maana kuwa kuwepo uwiano wa karibu kati ya kukua
kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi
wa kawaida.
Lakini kama unga bei ni juu au sukari bei kubwa kumwambia
mwananchi uchumi unakwenda vizuri ni vigumu kuamini.
Hapa kuna kila sababu ya viongozi wa serikali kukuna vichwa
na kuhakikisha gharama za bidhaa zinakuwa chini.
Gharama za bidhaa zinapokuwa chini thamani ya fedha
inaonekana, lakini ilivyo sasa bado tuna kazi kubwa ya kufanya.
Kwa lugha nyingine ni kuwa ni lazima serikali soko huria
linafanya shughuli zake bila kuathiri maisha ya wananchi wake.
Si hivyo tu, bali tuna jambo la kufundisha chini ya soko
huria kwamba serikali nayo inatakiwa iwe inazalisha.
Kama itajitoa kuendesha kila kitu eti kuachia tu sekta
binafsi kwa hakika itajikuta ikishikana mashati na raia wake.
Hayo yametokea nchini Senegal na Haiti, hivyo lazima serikali
ijipange vizuri kutetea haki na maslahi ya watu wake.
Katika nchi hizo kwa nyakati tofauti ilifikia hatua wananchi
wakaingia mitaani na mifuko mitupu ili waweze kupatiwa unga.
Walifanya hivyo wakimuomba Rais wa wakati huo, Abdulaye Wade
awapatie unga kutokana na bei yake kuwa kubwa mno.
Hali ya namna hiyo ilijitokeza pia nchini Haiti ambako
wananchi walikuwa wanalalamikia gharama kubwa za unga.
Kama tatizo ni mfumuko wa bei wataalamu tunao. Tuwatumie ili
watuoneshe ni wapi tulipokosea ili mambo yaende vizuri.
SHARE
No comments:
Post a Comment