Julian Msacky
MWANDISHI Tonn Burgis alipoandika katika kitabu chake cha
“The Looting Machine” ama mtambo wa uporaji rasilimali za Afrika hakukosea.
Kwa mujibu wa Burgis anashangaa ni kwa nini Afrika inazidi kuwa
fukara wakati ina utajiri wa kila aina.
“Ni kwa nini bara hili ni maskini wakati limesheheni utajiri
wa kina aina,”alihoji Burgis katika kitabu hicho.
Anachozungumzia mwandishi huyo ni tatizo ambalo lipo nchi
zetu za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Niharakishe kusema hapa kuwa umakini mdogo wa viongozi wetu
ndiyo umesababisha Afrika iwe ilivyo.
Wanyama aina ya swala
Hii ni kwa sababu baadhi yao wamesimika “mtambo wa uporaji”
na kuacha watu pamoja na nchi zao zikiwa taaban.
Mtambo huo wa uporaji unafyonza kila kitu iwe kwa mikataba ya
kitapeli ili mradi tu mali zivunwe kama hazina wenyewe.
Angalia namna madini yetu yanavyonunwa kiholela kwa sababu ya
kusimika mtambo wa uporaji ili wachache waishi vizuri.
Haikutarajiwa kuona nchi kama yetu tukilia umaskini kwa
sababu Mungu ameibariki na kuipa kila kitu.
Swali ni je, neema hiyo nani ananufaika nayo? Je, tulistahili
kuwa maskini au tumetengenezewa umaskini?
Kwa nchi yenye almas, dhahabu, shaba na mengine mengi hivi
tuna sababu ya kusema nchi ni maskini?
Hivi tatizo ni umaskini kweli au ipo ajenda nyingine chini ya
mtambo wa uporaji anaosema mwandishi huyo?
Ni kwa nini tuwe hivyo wakati nchi kama Libya iliweza kutumia
mafuta yake na kujitosheleza kwa kila kitu?
Tuliona namna Muammar Gaddafi alivyofanya nchi yake iwe kama
peponi na wananchi wake walineemeka mno.
Ameuawa kwa kulinda rasilimali za nchi yake na leo hii Libya
imekuwa magofu na uwanja wa mapambano kila kukicha.
Wananchi walirubuniwa na kumchukia kiongozi ambaye aliwafanya
waishi kwa furaha na bila ombaomba.
Leo hii Libya haikabiliki. Leo hii Libya haifai. Mataifa ya
magharibi yamesimika mtambo wa uporaji na hakika wanavuna.
Swali hapa ni je, Tanzania tuna kila kitu lakini tumeshindwa
kuifanya ionekane kama nchi tajiri. Tumlaumu nani?
Tukisema wananchi ni kukosea. Viongozi wana kila sababu ya
kutuambia kwa nini maliasili zetu zimeshindwa kutuneemesha.
Nilitamani kuona madini kama tanzanite ambayo hayapatikani
kokote duniani yawe mhimili imara wa uchumi wetu.
Hili limeshindikana. Tanzanite inaendelea kuvunwa na baada ya
miaka michache tubakia na mahandaki.
Kama tungetumia vizuri utajiri uliopo nchini leo hii Tanzania
ingekuwa nchi ya viwanda zamani za kale.
Lakini kwa vile tumesimika mtambo wa uporaji, mali
zinaendelea kumalizika na hatuna viwanda vyovyote vya kujivunia.
Matokeo yake tunakuwa nchi ya kuombaomba hata kwa mataifa
ambayo hayana rasilimali kama zetu.
Huo ndiyo ukweli hata kama baadhi yetu hatutaki kusikia.
Yanayosemwa kuhusu sekta ya madini wala haishangazi.
Kinachotakiwa kwa sasa ni kuweka mifumo vizuri na viongozi kutanguliza
uzalendo kwa ustawi wa nchi yetu.
Bila kufanya hivyo kazi anayofanya Rais John Magufuli
itaonekana leo, lakini akiondoka mambo yanabaki vilevile.
Ni mifumo pekee itakayotusaidia na kuhakikisha utajiri wetu
unavunwa tukijua kuna leo na kesho.
Tukivuna mali zilizopo kana kwamba Tanzania hatakuwa tena na
watu itakuwa ni dhambi kubwa. Ni lazima tubadilike.
Ni lazima viongozi waoneshe kuguswa na matatizo ya wananchi
kama alivyokuwa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mwalimu alitunza rasilimali tunazochezea leo hii na pengine
baadhi yetu hatuna uchungu nazo ndiyo maana zinatapanywa.
Hii ikiwa na maana kuwa hazitumiwi kwa utaratibu. Zinatumiwa
kiholela na hata kile kinachopatikana hakisaidia nchi ipasavyo.
Kwa mfano, tukiulizwa leo hii fedha za dhahabu tunazitumia
kwa kazi gani tutakuwa na majibu ya kuridhisha?
Tukiulizwa fedha zinazopatikana sekta ya utalii zinakwenda
wapi au zinafanya jambo gani la kuonekana, tuna majibu mazuri?
Au tangu tuanze kuchimba madini ya tanzanite yamefanya nini
kwa nchi na watu wake au tunachimba tu ili siku ziende?
Binafsi ninadhani kuna kila sababu ya kujipanga upya na
kuweka mfumo maalumu wa uvunaji wa rasilimali zetu.
Natamani kuona fedha ya tanzanite inatengewa kazi maalumu
mathalani kutoa elimu bure wanafunzi wa chuo kikuu.
Fedha ya dhahabu ielekezwe kwa huduma mathalani za afya kwa
maana dawa na vifaa tiba vipatikane vizuri hospitalini.
Vivyo hivyo kwa rasilimali nyingine ambazo tumepewa bure na
Mungu lakini tunazitumia ndivyo sivyo.
Kwa kufanya hivyo ingesaidia kupunguza mitambo ya uporaji
ambayo imefanya nchi na Afrika iwe kama shamba la bibi.
SHARE
No comments:
Post a Comment