Said Mwishehe
KWA Ujinga Wangu kabla ya kuendelea na kile ambacho nimepanga kukizungumza Jumapili ya leo hii nikakumbuka yale mashairi ambayo wengi wetu tumeyaimba tukiwa shuleni. Ni mashairi yenye ujumbe wa kizalendo kwa nchi yetu. Yanasema hivi;
Tazama ramani utaona nchi nzuri
Yenye mito na mabonde mengi ya nafaka,
Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri,
Nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania
Majira yetu haya, yangekuwaje sasa
Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2
Chemchem ya furaha amani nipe tumaini,
Kila mara niwe kwako nikiburudika,
Nakupenda sana hata nikakusitiri,
Nitalalamika kukuacha Tanzania.
Majira yetu haya, yangekuwaje sasa
Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2
Nchi yenye azimio lenye tumaini,
Ndiwe peke yako mwanga wa Watanzania,
Ninakuthamini hadharani na moyoni,
Unilinde name nikulinde hata kufa.
Majira yetu haya, yangekuwaje sasa
Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha X2
Baada ya kukumbusha mashairi hayo ambayo nimeona ni vema tukajikumbusha sasa nije kwenye ajenda yangu ya leo na hii inahusu mijadala mbalimbali inayoendelea kwenye kila kona ya nchi yetu kutokana na maelezo ambayo Rais John Magufuli ameyatoa alipopokea ripoti ya uchunguzi kuhusu mchanga wa madini ambao husafirishwa nje ya nchi makontena kwa makontena.
Kuna mambo mengi yameelezwa kwa kina ndani ya ripoti hiyo ambayo sisi wengine tumeisikia kupitia Rais Magufuli wakati anaeleza yaliyomo ndani ya ripoti hasa namna ambavyo madini yamekuwa yakipotea na mambo mengine kadhaa wa kadhaa.
Kwa bahati nzuri ripoti hiyo itatoa dira na mwelekeo wa miongozo inayotakiwa kufuatwa na kufanyika kunusuru rasilimali zetu kwa maslahi ya Watanzania.
Kwa Ujinga Wangu kuibeza ripoti hiyo ambayo imekuwa gumzo ni kutojielewa lakini ukweli ni kwamba lazima watu tuendelee kujadili nini hatima ya madini yetu.
Nieleze mapema hapa sipo kwa ajili ya kuangalia waliokuwa wanachimba wamefanya udanganyifu kwa kiwango gani maana hilo si jukumu langu. Zipo mamlaka ambazo zinahusika na ndizo zenye jikumu la kuzungumzia suala hilo kwa kina.
Ila kama Mtanzania mzalendo mapema kabisa nieleze namna ambavyo Rais Magufuli ameugusa moyo wangu na kuungezea furaha maishani. Kimsingi Rais amefanya jambo ambalo litamfanya abaki kwenye akili za Watanzania kwa miaka mingi ijayo.
Najua viongozi wetu wa ngazi tofauti na hasa wa kitaifa tunawakumbuka kwa michango yao mbalimbali lakini kwa Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kuunda tume maalumu ya kuchunguza mchanga huo itamfanya awe Rais wa mfano wa kuigwa na wengine.
Kwa Ujinga Wangu nimekuwa nikijiuliza kwanini tumekuwa omba omba kila kukicha? Kwanini tunashindwa kujisimamia katika kufanya maendeleo yetu? Hivi tumerogwa na nani hadi tunashindwa kupiga hatua?
Maswali ni mengi ambayo hakuna mwenye majibu yake kamili lakini kwa sasa naanza kupata majibu ya kwanini tumekuwa masikini na tunashindwa kujisimamia wenyewe katika mambo mengi ya kimaendeleo. Kama kwenye madini hali iko hivyo unatarajia nini.
Kwa Ujinga Wangu naanza kuona Rais Magufuli ameanza kutoa majibu sahihi ya kwanini tulikuwa tumeshindwa kuendelea. Kwa ripoti hii ya mchanga wa madini inatuonesha namna ambavyo kwa muda mrefu tumekuwa tukikosa mabilioni ya fedha kutoka sekta ya madini.
Rais Magufuli amefafanua kwa kina kuhusu fedha ambazo kama tungesimamia sekta ya madini vizuri zingepatikana na hakika zingetufanya tuishi kwenye Tanzania ambayo kila mmoja wetu angeifurahia tofauti na sasa wapo wenye uhakika wa mila mitatu kwa siku na wengine mlo mmoja kwao taabu.
Nafahamu moja ya mjadala mkubwa ambao unaendelea baada ya Rais Magufuli kutoa ripoti hiyo acha sie tunayoipongeza lakini mjadala mkubwa kwa wengine ni kwamba tutashitakiwa kimataifa kwani ripoti hiyo kama haitakuwa na ukweli itatusabisha nchi kuingia kwenye hasara kubwa.
Kwa Ujinga Wangu haya mambo ya kuogopa kushitakiwa ndio ambayo yametufanya tufike ambako tumefika.Madini yetu yapo kwenye ardhi kwa miaka mingi na si mingi tu bali tangu kuumbwa kwa dunia. Hivyo tulikuwa na nafasi ya kutosha kabla ya kuanza kuyachimba.
Hivyo Rais Magufuli anafanya jambo ambalo lilipaswa kufanywa miaka mingi tu iliyopita.Sawa tunaweza kusema ingekuwa ngumu wakati wa ukoloni na baada ya wakoloni kuondoka tumefanya nini?
Kuna wabunge wengi wa hasa wa upinzani wamekuwa wakielezea namna ambavyo tunadhulumiwa kwenye eneo la madini. Wamekuwa wakisikitishwa na namna ambavyo nchi yetu inabaki na mashimo ambayo hata kuyafukia kwake ni vigumu na madini yanakwenda nje ya nchi yetu.
Kwa Ujinga Wangu natambua namna ambavyo mikataba ambayo ipo kwenye sekta ya madini ilivyokuwa imewekia vigingi ambavyo wakati mwingine vinasababisha kama nchi kushindwa kuchukua hatua. Maana ukitaka kuchukua hatua utaambiwa mkataba unazuia.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo
Matokeo yake nchi yetu madini yanazidi kuondoka na sisi tupo kimya. Ukiuliza kwanini tunaogopa mikataba iliyopo itatuingiza kwenye mgogoro. Tayari tumeanza kusikia eti wale wenye michanga watatushitaki kwa sababu tumewakosea kutokana na ripoti hiyo.
Kwa Ujinga Wangu acha nisubiri kuona nini ambacho kitatokea lakini ukweli utabaki pale pale tumekuwa tukipoteza fedha nyingi katika eneo la madini. Wabunge wa upinzani wakizungumzia namna ambavyo madini yetu yanaondoka wanaambiwa wachochezi.
Ripoti ya mchanga wa madini ambayo Rais Magufuli amekabidhiwa juzi imenifanya nikumbuke namna ambavyo Mbunge wa Chadema Zitto Kabwe ambaye sasa yupo ACT-Wazalendo alivyoingia kwenye matatizo.
Zitto alimama imara bungeni kutetea mgodi wa Buzwagi lakini matokeo yake alisimamishwa kuingia bungeni kwa madai eti amesema uongo bungeni.
Nafahamu wabunge wa pande zote za chama tawala na upinzani wamekuwa wakizungumzia sekta ya madini na umuhimu wake.
Watanzania ni wakati wa kuwa kitu kimoja ili kupigania rasilimali za nchi yetu.Kama ambavyo shairi lile ambalo nimeanza nalo hapo juu linavyosema Tazama ramani utaona nchi nzuri huo ndiyo ukweli.
Tusikubali nchi nzuri Tanzania ikawa sehemu ya wengine kunuifaka nayo wakati wenyewe tupo, tunaona, tunasikia na tunajua namna ya kuzitetea.
Kwa Ujinga Wangu naomba nihitimishe kwa kusema kwenye madini yetu tusikubali kuwa wanyonge, tusimame imara kuyatetea. Ramadhan Njema. Usijali, tuwasiliane.
0713833822
SHARE
No comments:
Post a Comment