NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed amesema sasa ni wakati
muafaka kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) kuwekeza Visiwani
Zanzibar ili kuchagiza juhudi za Serikali za kuwawezesha kiuchumi wakazi wa
visiwa hivyo wanaojishughulisha na sekta za kilimo, uvuvi na uchakataji mazao.
Mhe. Hamad amesema Visiwa vya
Zanzibar vina maeneo mengi ya uwekezaji yenye kuweza kuongeza tija na ongezeko
la uchumi visiwani humo ikiwa kutakuwa na uwekezaji mkubwa katika maeneo hayo.
“Nawahakikishia, mkianza
kuwekeza katika miradi kama ya mwani, uvuvi na karafuu Bebki itapata matokeo
makubwa sana na mnaweza kuitumia Zanzibar kama mfano rejea katika utoaji wa
mikopo yenye tija nchini,” alisihi.
Kwa mujibu wa Mhe. Waziri,
Zanzibar ni miongoni mwa visiwa vyenye utajiri mkubwa ambavyo kukiwa na
uwekezaji wa kimkakati vinaweza kutokea matokeo makubwa na yenye kuwanufaisha
wananchi wengi.
Akizungumza na Mhe. Waziri,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga amesema Serikali iliamua
kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana
na mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika
sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika kilimo nchini.
Bw. Assenga ameongeza kuwa
Benki inatambua fursa za uwekezaji Visiwani Zanzibar na amemuahidi kuwa
wamejipanga kuanza uwekezaji mkubwa wa wadau wa sekta za kilimo na uvuvi ambazo
ni sekta za kipaumbele zinazopatiwa mikopo na TADB.
Ameongeza kuwa Benki yake
imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa sekta hizo ili kuongeza tija
sekta hizo ili kupambana na umaskini nchini.
TADB ni taasisi ya serikali ambayo ilianzishwa kwa
ajili ya kutatua ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha mikopo kwa ajili ya
maendeleo ya kilimo nchini ambao ulikuwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na
mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye upande wa biashara
za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo ya muda mfupi; masharti
magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya sekta ya kilimo na mazao
ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Waziri wa Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed (kushoto) akimkabaribisha
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB),
Bw. Francis Assenga (kulia) wakati walipomtembelea Ofisini kwake mjini Unguja.
Mkurugenzi wa Mikopo na
Biashara wa TADB, Bw. Augustino Chacha (wapili kushoto) akikaribishwa na Waziri
wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, Mhe. Hamad Rashid Mohamed
(kulia) wakati viongozi wa TADB walipomtembelea Mhe. Waziri Ofisini kwake mjini
Unguja. Wengine pichani ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis
Assenga (wapili kulia) na Meneja Mikopo wa TADB, Bw. Samuel Mshoto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TADB, Bw. Francis Assenga (aliyesimama) akieleza dhima ya Benki ya Kilimo
wakati walipomtembelea Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar,
Mhe. Hamad Rashid Mohamed (wapili kulia).
SHARE












No comments:
Post a Comment