Hebu
jaribu kulielezea jiji la Dar, au la Arusha, ama la Mwanza, Mbeya ama
jiji lolote lile, tena kwa kutumia ukurasa mmoja tu na uwe umefanikiwa
kulieleza kinagaubaga kiasi hata mtu ambaye hajawahi kufika hapo ajione
kama keshafika na anapafahamu vizuri.
Basi
huo ndio mtihani nilionao wakati naandika haya, tena kwa moyo mzito,
nikijaribu kumwelezea rafiki yetu, kaka yetu, ndugu yetu, jamaa yetu au
vyovyote vile upendavyo kumwita mtu kama Balozi Abdul Omar Cisco Mtiro.
Ni
kweli kwamba mtu akitangulia mbele ya haki huwa kuna hulka ya kumsifia
na kumuenzi mtu huyo. Lakini si uwongo kwamba haya niandikayo hapa, japo
yalikuwa nyuma ya ubongo wa wengi wetu siku zote, ni halisi na wala sio
kwa sababu Cisco hatunaye tena.
Kwa
wengi alikuwa mkarimu na mwingi wa bashasha saa zote. Kwa tuliobahatika
kuwa karibu naye, Cisco alikuwa hivyo na zaidi. Pamoja na kuwa na
wadhifa mkubwa serikalini (Balozi wetu nchini Nigeria na Malaysia katika
nyakati mbalimbali na baadaye Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya
Nje), Cisco alikuwa mtu wa kujichanganya na kila mtu bila kujali hali
ama mali zake. Hakuwa na makuu wala makidai.
Unapomkuta
na wanachama wenzie wa Klabu ya michezo ya TAZARA pale Leaders Club ama
kwa Octa (kijiwe maarufu jirani na ubalozi wa Ufaransa) ilikuwa huwezi
kuamini kwamba huyu mtu mchana ametoka kusuguana mabega na viongozi
wakuu wa nchi na wageni wao ambao, akiwa kama Mkuu wa Itifaki, jukumu
lake lilikuwa kuratibu na kusimamia kila kitu.
Ubaya,
ama uzuri wake, hukumsikia hata mara moja akizungumzia kazi yake ama
wadhifa wake. Huko alikuwa serious kama askari wa Mjerumani. Lakini
afikapo kijiweni, kama mlivyo nyinyi wakati huo, na yeye pia alijitosa
kuogelea nanyi kwenye soga za siku kama vile kandanda, stori zote za
mjini, pamoja na muziki ambao alikuwa anaupenda sana – hasa hasa Jazz na
classics.
Sifa
yake kubwa akiwa nasi kijiweni ilikuwa ni utani na vichekesho vya
kuvunja mabvu. Yaani Cisco alikuwa hakosi kuja na ‘mpya’ hata kabla ya
kuketi kitini, na wakati wa kuondoka kwenda kupumzika alikuwa hakosi
kuwaacha na ‘kibomu’ kingine cha kuchana mbavu. Vile vile kila ukutanapo
naye lazima ‘akuchape’ na kitu kipya.
Na
hiyo ilikuwa hivyo kwa takriban miongo yote miwili ambayo nilibahatika
kuwa karibu naye. Angeweza kuandika vitabu lukuki vya utani na
vichekesho na bado akabaki hajaishiwa.
Balaa
la vunja mbavu liliongezeka maradufu pale alipokutana na marafiki
wengine wa karibu kama vile Balozi Mohamed Maharage (aliyekuja
kumwachia kiti cha Mkuu wa Itifaki pale alipostaafu rasmi kazi takriban
miaka mitatu iliyopita) kina Mudhihir Mudhihir, Job Juma, Max Rutihinda,
David Mgwassa, Muddy Pizzaro, Makongoro Nyerere, Ronnie Mtawali na
wengi wengine ambao nashindwa kuwataja wote kwa ufinyu wa nafasi. Hawa
wakutanapo unakuwa hutaki kuondoka…
Yote
tisa. Cisco pia alikuwa hodari katika kuhamasisha wadau kushiriki
katika shughuli za mwenzetu wakati wa shida ama raha, iwe harusi ama
msiba.
Huyu
braza hatosahaulika pale alipoasisi kufanyika kwa michezo baina ya timu
za veteran kutoka kila pembe ya jiji iliyokuja kujulikana kama Sunday
Soccer Bonanza. Yaani kila Jumapili wachezaji wa vilabu vya Veterans
kutoka Sinza, Kinondoni, Ilala, Temeke walikutanika Leaders Club na
kuchuana katika mchezo wa soka na baada ya hapo burudani ya muziki wa
aidha Msondo ngoma ama Twanga Pepeta ilifuata. Umati uliokuwa unajaa
hapo mahali si mchezo. Hakika
Bonanza hilo lilifanikisha kwa kiasi kikubwa kuunganisha na kudumisha
undugu miongoni vijana na watu wazima wa sehemu mbalimbali za Dar es
salaam. Kama kuna mtu aliyekuwa ananung’unika san asana kwa kufifia kwa
Bonanza hilo hivi sasa, basi wa kwanza alikuwa Cisco.
Kama
hilo Bonanza lilikuwa halitoshi, Cisco na wanachama wenzie wa TAZARA
Club wakabuni hadhara ya kukutana mara moja kila mwaka kuwakumbuka na
kuwaombea wenzetu wote waliotangulia mbele za haki kwa kisomo na dua za
dini zote. Baada ya hapo ‘mpunga’ ulifinywa huku Balozi akichana mbavu
za wadau kutwa nzima kwa vichekesho na stori za mjini.
Nashindwa
kukubali kwamba katika kisomo kifuatacho hapo Leaders Club jina la
Abdul Omar Cisco Mtiro litatajwa katika orodha ya kuwarehemu wenzetu
wote waliotangulia mbele ya haki.
Kama
nilivyosema hapo awali, ugumu wa kumueleza mtu kama Cisco hauna tofauti
na kuelezea jiji lolote kwa kutumia ukurasa mmoja tu. Yaani naweza
kuandika kurasa mia kama hizi lakini bado nisiweze kusimulia robo tu ya
Cisco alikuwa ni mtu wa aina gani huku 'uraiani'.
Itoshe
tu kusema kwamba kifo kimetupoka mtu mmoja muhimu sana sana katika
maisha yetu, na daima jina lake litabaki kuwa midomoni na ndani ya
vilindi vya mioyo yetu daima.
ADIOS AMIGO, BRAZA CISCO!
SHARE
No comments:
Post a Comment