SERIKALI imeipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), shilingi 209.5 bilioni kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo hapa nchini, leo, Jijini Dar es salaam.
Akiongea kwa niaba ya Serikali wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makabidhiano ya fedha hizo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ni sehemu ya shilingi 800 bilioni ambazo Serikali inatarajia kuipatia Benki hiyo ili iweze kukuza mtaji wake.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo (hawamo pichani).
“Ninaishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kuipatia Serikali mkopo wa Dola za Marekani 93.5 milioni ambazo ni sawa na kiasi hicho cha fedha cha Sh. 209.5 bilioni kwa ajili ya kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu” alisema Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya kilimo na mifugo ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika ukuaji wa pato la Taifa kuliko ilivyo sasa.
“Mwaka jana kilimo ambacho kinategemewa na idadi kubwa ya Watanzania kilichangia wastani wa asilimia 29.1 ya Pato la Taifa lakini tunataka kupitia Benki hiyo Sekta ya kilimo iiwezeshe nchi kukua kiuchumi kwa zaidi ya asilimia 7 hadi 10 katika kipindi kifupi kijacho” aliongeza Dkt. Kazungu.
Akiongea baada ya kutia saini makubaliano ya kupokea fedha hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Bw. Francis Assenga, ameishukuru Serikali kwa kuiongezea Benki yake mtaji utakaotumika kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji nyuki.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kitaiwezesha Benki hiyo ambayo imekwisha wafikia wakulima zaidi ya 3,700 hapa nchini, kuanza kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wakulima wadogo na wa kati ili kuinua Sekta hiyo kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na kilimo na mifugo.
Ameihakikishia Serikali kwamba Benki yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa matunda ya fedha hizo yanaonekana na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Ras Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwakwamua wananchi wake katika lindi la umasikini.
“Riba za Mikopo ya Benki yetu ziko chini ikilinganishwa na Benki nyingine ambapo sisi tunatoza asilimia 8 hadi 12 kwa wakulima wadogo na asilimia 15 kwa wakulima wa kati wenye viwanda wakati viwango vya riba katika soko ni asilimia 18 na wakati mwingine vinafika hadi asilimia 40.” alisema Bw. Assenga wakati akijibu maswali ya wanahabari.
SHARE
No comments:
Post a Comment