Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)
akiwaomba wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili
kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)
akiwaomba wananchi kulipa kodi ya Majengo mapema kwa mwaka wa Fedha 2017/18 ili
kuepuka usumbufu wa msongamano, alipofanya Mkutano na Waandishi wa habari
katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
NA BENNY MWAIPAJA
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh
bilioni 32.5 ya kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka
katika Majiji, Miji na Manispaa 30 nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) amewaambia
waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na
asilimia 56 ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi
bilioni 58.
Alisema kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe
jukumu la kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo
hayo, Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3 wakati TRA
imekusanya kiasi hicho cha shilingi bilioni 32.5 tangu ianze kukusanya kodi
hiyo mwezi Oktoba mwaka wa fedha 2016/2017.
“Mpaka kufikia tarehe 15 Julai mwaka huu TRA imekusanya sh. bil
32.5 kipindi ambacho ni kifupi, na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka
kutokana na mwitio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo”Alisema Dkt.
Mpango.
Dkt. Mpango aliwapongeza wananchi kwa mwitio wao mkubwa wa
kulipa kodi ya majengo na kwamba wameonesha uzalendo wa kweli na ndio maana
Serikali imeamua kuongeza muda wa kulipa kodi hiyo bila adhabu hadi Julai 30
mwaka huu, hali anayoamini itapandisha zaidi mapato hayo.
Katika hatua nyingine Dkt, Philip Mpango
aliwapongeza wamiliki wa vituo vya mafuta
waliotii maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za EFDs,
akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga mashine
hizo kwenye pampu zao zote.
Aliwaonya wamiliki wote wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga
mashine hizo za EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli linavyoelekeza na kwamba yeye kama Waziri mwenye dhamana
atahakikisha analisimamia kikamilifu na kwamba baada ya muda huo mtu
asijekuilaumu Serikali baada ya kuanza kuchukua hatua kali za kisheria.
Aliwataka wamiliki wa vituo hivyo kupitia chama chao cha
wamiliki wa vituo vya mafuta TAPSOA kuheshimu maelekezo ya Serikali na kuacha
majibizano yasiyo na tija kuhusu amri hiyo ya Rais kwenye vyombo vya habari kwa
kuwa huo ni utovu wa nidhamu.
Aliwageukia wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka
makubwa ‘supermarket’ nao watumie mashine hizo za kukusanyia mapato ya Serikali
(EFDs) kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao huku akiwaasa wateja nao kudai
risiti wanapofanya manunuzi kulingana na kiwango halisi cha bidhaa wanazonunua.
Alipiga marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs
kuwa mbovu na kuwaonesha wateja wao makaratasi waliyotoa taarifa TRA kwamba
mashine zao zilikuwa mbovu kwa kipindi kifrefu na kuaigiza Mamlaka ya Mapato
Tanzania-TRA, kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linakoma kabisa.
“TRA mtimize majukumu yenu mliyodhaminiwa na Serikali na
kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa
48 kwa kisingizio cha kuharibika zifungiwe na wamiliki watozwe faini na kulipa
kodi ya Serikali ipasavyo” aliagiza Dkt. Mpango.
“Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi, tumeazimia tutafanya
kazi kwa niaba ya wanyonge ili nchi yetu iende mbele na kwa hili watusamehe.”
Alisisitiza Dkt. Mpango
Dkt Mpango alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kujitoa kwake kuwatumikia wananchi na
kuongoza mapambano ya uchumi yatakayo ifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ambao
hata watu wa kawaida watajisikia kuwa unakua kwa kutatua changamoto zao za
maisha.
Alisitiza watanzania wafanye kazi kwa bidii kujenge nchi ili
kila Mtanzania apate huduma bora, barabara bora, tiba nzuri, maji, yote haya
hayawezi kufanyika bila mapato yakutosha na kwamba Tanzania itajengwa na
Watanzania wenyewe.
SHARE
No comments:
Post a Comment