NA OWM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi
wote waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao
.
Pia ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka
alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika
wazibomoe.
Agizo hilo amelitoa leo jioni (Ijumaa, Julai 21, 2017) alipotembelea eneo la
ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na
Zambia, ambacho kinajengwa na Serikali ya Tanzania na kitagharimu sh. bilioni
12.
“Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na
kuendesha biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha
Serikali mapato.”
Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa
watu wote waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50
kutoka Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari.
“Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu
wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka
husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia.”
Awali Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini
Zambia, Bw. Field Simwinga ambaye alisema wamekubaliana na utekelezaji wa agizo
hilo kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.
Bw. Simwinga alisema tayari wameshaanza kuwaeleza wananchi wao
waliojenga ndani ya mpaka huo kuanza kuondoka, ambapo Waziri Mkuu amesema
wanataka eneo hilo liwe wazi ili iwe rahisi kuutazama mpaka huo kwa umakini.
SHARE
No comments:
Post a Comment