Hali ya wasi wasi imeendelea kuwepo nchini Kenya tangu jana Jumapili (13.08.2017) baada ya watu 11 kuuawa katika maandamano ya ghasia na upinzani umeendelea kudai
kwamba kuchaguliwa tena kwa rais Uhuru Kenyatta kubatilishwe.
Wakati sehemu kubwa ya nchi iko tulivu, waungaji mkono wa
mgombea wa upinzani aliyeshindwa Raila Odinga waliokuwa wakirusha
mawe waliendelea kupambana na majeshi ya usalama siku ya Jumamosi
katika maeneo ya ngome ya wapinzani upande wa magharibi wa nchi
hiyo na maeneo ya mabanda katika mji mkuu Nairobi.Afisa mwandamizi wa polisi ameliambia shirika la habari la AFP kwa masharti ya kutotajwa jina kwamba miili ya watu wanane kutoka katika maeneo ya makaazi duni mjini Nairobi imewasili katika chumba cha kuhifadhia maiti mjini humo , na mpiga picha wa AFP alishuhudia mwili wa msichana ambae familia yake imesema alipigwa risasi mgongoni wakati akiangalia maandamano kutoka katika ukumbi wa juu ya nyumba.
Upande wa magharibi mwa Kenya , afisa wa polisi alisema mtu mmoja mwanamume alipigwa risasi na kufariki katika maandamano mjini Kisumu.
Bado haijawekwa wazi muungano wa vyama vya upinzani wa National Super Alliance NASA wa Raila Odinga utachukua hatua gani, lakini viongozi wa chama wamesema hawatarudi nyuma ama kupelela malalamiko yao mahakamani.
"Hatuta ogopa, hatuta kubali kupiga magoti," afisa wa NASA Johnson Muthama aliwaambia waandishi habari jana Jumamosi.
NASA yadai polisi inakandamiza waandamanaji
Yeye pamoja na viongozi wengine wa upinzani wanasisitiza kwamba uchaguzi uliofanyika siku ya Jumanne umechakachuliwa. Pia wamewashutumu polisi kwa ukandamizaji dhidi ya waandamanaji katika juhudi za kuulazimisha muungano huo "kupiga magoti."
Baadhi ya waandamanaji katika mtaa wa makaazi duni wakishikilia picha ya mgombea wanaemuunga mkono Raila Odinga
Akihutubia
vyombo vya habari jana Jumamosi(12.08.2017), Muthama alionesha
mfuko uliokuwa umejaa maganda ya risasi ambayo anadai yalitumiwa
na majeshi ya usalama kuwauwa "Wakenya ambao hawana hatia"
waliokuwa wakishiriki katika maandamano mitaani baada ya tangazo
la ushindi wa Kenyatta siku ya Ijumaa usiku."Tunataka kuwahakikishia wananchi kwamba tuna nia, na dhamira, na uwezo wa kuhakikisha kwamba kura yako ni muhimu mwishoni mwa siku," amesema.
Kenya haina ugeni katika machafuko ya baada ya uchaguzi, na makovu yako bado kutoka katika uchaguzi uliobishaniwa wa mwaka 2007 ambao ulisababisha mapambano ya miezi miwili ya siasa za kikabila , na kusababisha watu 1,100 kuuwawa na wengine 600,000 wakikimbia makaazi yao. Lakini wakati ghasia zimesambaa nchini Kenya, machafuko ya mwaka huu yana ukomo ambapo yamefanyika katika baadhi tu ya maeneo. Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiangi amepuuzia machafuko hayo, akiwaita waandamanaji "wahalifu " na kusema hakuna mtu aliyefariki.
"Polisi hawakutumia risasi za moto dhidi ya maandamano yoyote ya amani," amesema.
Odinga hajazungumza na wafuasia wake
Odinga , mwenye umri wa miaka 72 hajawahutubia wafuasi wake baada ya kushindwa kwa mara ya nne katika azma yake ya kuwania kiti cha urais. Anaamini uchaguzi mwaka 2007, 2013 na hivi sasa 2017 umeibiwa.
Ameelekeza shutuma za udukuzi wa kiwango cha juu kabisa kwa vifaa vya kuhifadhi data vya tume ya uchaguzi, na kusema upinzani una ushahidi wa matokeo sahihi , ambayo yanonesha kuwa yeye ndie mshindi, na yanafichwa.
Tume ya uchaguzi IEBC inakana shutuma hizo, na inadai nyaraka anazosema anazo zenye ushahidi zimekuwa na makosa ya kimahesabu na zinatoka kutoka programu ya kukusanyia data ya Microsoft wakati mfumo wa kukusanya matokeo wa kielekroniki ulikuwa wa programu ya Oracle.
Hatua hiyo ya kukana kwa tume ya uchaguzi wa IEBC imeungwa mkono na waangalizi wa kimataifa pamoja na kundi linaloangalia uchaguzi la Kenya ELONG, ambalo limesema waangalizi wake 8,300 pamoja na operesheni ya kukusanya matokeo haikugundua makosa yoyote katika matokeo hayo.
Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa mataifa Kofi Annan , ambaye alisaidia upatanishi katika mzozo wa mwaka 2007, alimpongeza Kenyatta kwa ushindi wake na kumtaka Odinga, "mtetezi imara wa demokrasia", kwenda mahakamani kupeleka malalamiko yake.
Siasa nchini Kenya imegawanyika kikabila, na mshindi mara zote katika uchaguzi wa nchi hiyo huzusha mpasuko kwa misingi ya kikabila.
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment