Na. Said Ameir – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya
Misri amesifu ushirikiano kati ya taasisi za Tanzania na Misri
zinazoshughulikia mapambano dhidi ya rushwa na kumpongeza Rais John
Pombe Magufuli kwa kuonesha mfano wa uongozi bora unaopambana na maovu
katika nchi yake.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa
jitihada zake za kupambana na rushwa na ufisadi na huo ni mfano wa sifa
za uongozi bora” alieleza Rais Al Sisi wakati akizungumza na waandishi
wa habari jana jijini Dar es salaam.
Rais wa John Magufuli (kushoto) akiwa na Rais wa Misri,
Rais Al Sisi
Rais wa John Magufuli (kushoto) akiwa na Rais wa Misri,
Rais Al Sisi
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa Tanzania (TAKUKURU) na Taasisi ya Udhibiti wa Utawala ya Misri
(Administration Control Authority of Egypt) zimekuwa na ushirikiano wa
karibu kwa kubalidilishana utaalamu, uzoefu na mbinu katika kutekeleza
majukumu yao.
Katika mkutano, huo ambao
uliofanyika mara baada ya kumalizika mazungumzo rasmi kati ya nchi hizo,
Rais Al Sisi alieleza dhamira ya nchi yake ni kuendelea kushirikiana na
Tanzania katika kuunga mkono jitihada za kuleta amani barani Afrika na
kuendelea kuwa na msimamo mmoja katika masuala ya kimataifa.
“Tunampongeza Rais Magufuli na
Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kutafuta amani barani Afrika
hasa katika eneo la Maziwa Makuu” Rais Al Sisi alisema na kumpongeza
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za
usuluhishi katika mgogoro wa Burundi.
Rais huyo ambaye alikuwa nchini
kwa ziara rasmi ya siku mbili, ameeleza kutambua mzigo mkubwa inaoubeba
Tanzania katika kushughulikia migogoro ikiwa ni pamoja na kuhudumia
maelfu ya wakimbizi kutoka katika nchi mbalimbali.
Katika mkutano ambao ulihutubiwa
pia na mwenyeji wake Rais Magufuli, Rais huyo wa Misri alieleza utayari
wa nchi yake kuendeleza na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania kwa
kuhimiza kubuni na kutekeleza miradi ya pamoja, kuongeza biashara na
uwekezaji pamoja na kubadilishana wataalamu.
”Misri na Tanzania hatma yao ni
moja, tutaendelea kushirikiana kwa hali na mali na kwa kuwa tuna
dhamira, matumaini yetu makubwa ni kufanikiwa” Rais Sisi alisisitiza.
Kabla ya mkutano huo na
wanahabari, Rais wa Misri alikuwa na mazungumzo ya faragha na mwenyeji
wake Rais Magufuli na baadae kuhudhuria mazungumzo rasmi ya mashauriano
kati ya Tanzania na Misri.
SHARE
No comments:
Post a Comment