Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
(VPL), msimu wa 2017/18 inaanza rasmi kesho Jumamosi Agosti 26, 2017 kwa
michezo saba itayochezwa katika viwanja tofauti nchini.
Ni msimu mpya utakaotoa timu
bingwa mpya itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoandaliwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), msimu wa 2019.
Itakumbukwa, msimu wa CAF wa 2018,
timu itakayoiwakilisha nchi ni Young Africans SC ambayo ni Bingwa wa
VPL msimu 2016/17 wakati michuano ya Kombe la Shirikisho, Tanzania
itawakilishwa na Simba SC.
TFF tunazitakia kila la kheri timu
zote zinazoshiriki ligi hii, tukiamini kwamba uadilifu utaongoza mbele
ya taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia mpira wa miguu hapa nchini
na kwingineko.
Kwa mechi za kesho Jumamosi, Simba
inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting katika mchezo utakaofanyika
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Mbao watakuwa wageni wa Kagera
Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya
Majimaji ya Songea itakayosafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya City
kwenye Uwanja wa Sokoine jijini humo huku Njombe Mji ikiialika Tanzania
Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.
Kadhalika Uwanja wa Manungu ulioko
Turiani, Mtibwa mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar itaikaribisha Stand
United ya Shinyanga kwenye mchezo mwingine wa VPL ilihali Azam atakuwa
mgeni wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Mwadui watakuwa wenyeji wa Singida
United ya Singida kwenye Uwanja wa Mwadui huko Shinyanga na Jumapili
kutakuwa na Mchezo mmoja utakaokutanisha Young Africans na Lipuli kwenye
Uwanja wa Uhuru jijini.
SHARE








No comments:
Post a Comment