SHIRIKA la Elimu, Sayansi na
Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limekabidhi vifaa vya radio kwa
radio za jamii nne vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi.
Unesco imesema kwamba utoaji wa vifaa hivyo umelenga kuongeza usikivu wa mawimbi ya radio katika maeneo ya vijijini.
Shughuli ya kukabidhiana imefanyika Agosti 17 mwaka huu.
Akizungumza wakati wakukabidhiana
vifaa hivyo Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Tanzania, Zulmira
Rodrigues alisema kwamba UNESCO inatambua kazi nzuri zinazofanywa na
radio hizo za jamii za kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha alisema ni muhimu sana kwa
radio hizo za jamii kujiangalia na kujitunza zenyewe ili wasiingie
katika matata na kuchapisha au kutangaza stori baada ya kukamilika
kwake.
Alisema ipo haja kwa vyombo vya
habari kufanyakazi kwa mujibu wa taratibu zao na kuhakikisha kwamba
hawachapishi habari ambazo zinahatarisha uwapo wa uandishi unaozingatia
maadili.
Meneja wa radio ya Jamii ya
Baloha FM, Samada Maduhu aliishukuru UNESCO kwa kusaidia kituo chake na
kwamba wanatarajia kufikia wilaya tano.
Alishukuru UNESCO kwa kuwawezesha
kufika katika wilaya tano na kwamba kwa msaada huo wataokoa shilingi
laki saba kwa mwezi kuazima transmita.
“Radio yetu inawafikia watu
500,000 lakini kwa kupatiwa hivi vifaa tutaweza kufikia watu milioni 1
katika wilaya zaidi ya tano za Kahama, Shinyanga Vijijini, Nyang’wale na
Mbogwe mkoani Geita na pia Nzega na Uyui mkoani Tabora ,” alisema meneja huyo .
Kwa mujibu wa Maduhu, kama wasingelipata transmita hiyo wangelikuwa wanatumia sh milioni 8.4 kwa mwaka.
Kwa upande wake, Ayubu Kalufya wa
radio ya jamii Uvinza alisema kwamba kituo chake kilikuwa kinakodisha
transmita kwash laki tano na kufanya kwa mwaka mzima kutumia sh milioni
6.
Alisema kwa kupata vifaa hivyo walikuwa wanaachama na ukodishaji huo.
Kwa mujibu wa Kalufya, transmita
hiyo mpya itawafikisha mbali zaidi katika pwani za Ziwa Tanganyika na
hivyo kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
Kalufya alisema wananchi wakisikia
mambo mbalimbali ya kuwaelimisha na wao wakapata nafasi ya kutoa maneno
yao haki za binadamu zitakuwa zimeheshimiwa sana nchini.
Aliishukuru Unesco kwa kuendelea
kuwasaidia na kusema kama si kwa msaada wa UNESCO jamii zilizopo
pembezoni zisingepata nafasi ya kutoa madukuduku yao.
Radio nyingine zilizonufaika na msaada huo ni Pangani FM. Radio hiyo sasa inaweza kusikika Tanga nzima badala ya Pangani pekee.
Katika orodha ya redio zilizopatiwa vifaa ipo pia Mkoani FM ya kutoka Zanzibar.
No comments:
Post a Comment