Mkurugenzi wa Tanzania Media
Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa
na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa Afisa Mahusiano kutoka
Clouds Media Group Simalenga Simon leo Jumamosi Septemba 16,2017 mkoani
Tanga-Habari/Picha na Oscar Assenga na Kadama Malunde
Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi
Mwangosi mwaka 2017 limeitangaza Clouds Media Group kuwa mshindi wa Tuzo
hiyo kwa mwaka 2017.
Tuzo hiyo imetolewa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini UTPC
wakati wa mkutano wake mkuu wa unaofanyika katika ukumbi wa Tanga Beach
Resort mkoani Tanga.
Tuzo hiyo imekabidhiwa kwa uongozi wa Clouds Media Group na Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura.
Mbali na kupewa tuzo hiyo,pia Clouds fm imekabidhiwa hundi ya shilingi
milioni 10 kama pole kwa changamoto waliyopitia baada ya kituo cha
matangazo kuvamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda
aliyekuwa ameambatana na askari polisi.
Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka
ya Daudi Mwangosi mwaka 2017,Jenerali Ulimwengu alisema madhumuni ya
tuzo ya mwangosi ni kumuenzi na kumkumbuka kwa kumpa mwanahabari au
chombo cha habari tuzo yenye jina lake.
“Jopo la majaji mwaka huu tunaitangaza Clouds Fm kuwa mshindi wa tuzo
ya Daudi Mwangosi mwaka 2017 kwa sababu tarehe 17,Machi,2017 wanahabari
wa Clouds walivamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam akiwa na askari
polisi akiwataka kutangaza habari ambayo hawakuitaka lakini wafanyakazi
hao wakakataa kutangaza habari hiyo,huu ni ushujaa kwani hawakukubali
kutii amri ambazo zilikuwa kinyume na kazi waliyofundishwa na uandishi
wa habari”,alisema Ulimwengu.
“Lengo la tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 2013 na UTPC ni kupinga
vitendo viovu wanavyofanyiwa waandishi wa habari , hutolewa kwa
mwandishi wa habari anayefanya kazi nchini aliyekutana na madhila katika
utendaji kazi wake ama chombo cha habari ambacho kimekutana na
madhila”,alieleza Ulimwengu.
Aliongeza kuwa tuzo hiyo inalenga kuwafanya wadau wa habari ikiwemo serikali kutambua kazi ya waandishi wa habari.
“Daudi Mwangosi alikuwa mwenyekiti Klabu ya waandishi wa habari mkoa
wa Iringa,aliuawa Tarehe 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo mkoani
humo,akitekeleza majukumu yake,ni mwandishi wa habari wa kwanza nchini
Tanzania kuuawa akiwa kazini, kifo chake kilishtua na kusikitisha watu
wengi duniani”,alieleza.
Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura akikabidhi tuzo
Tuzo ya Uandishi wa Kishujaa na Ulitukuka ya Daudi Mwangosi mwaka 2017
kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon
Mkurugenzi wa Tanzania Media Foundation,Ernest Sungura cheti cha ushindi
kwa Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon
Mkurugenzi wa Tanzania Media
Foundation,Ernest Sungura akikabidhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa
Afisa Mahusiano kutoka Clouds Media Group Simalenga Simon.
Habari/Picha na Oscar Assenga na Kadama Malunde
SHARE
No comments:
Post a Comment