Kaimu Meneja wa Manunuzi kutoka
Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) Bernard
Makhanda (kushoto) akitoa utaratibu wa kufuatwa na Mmiliki wa Kiwanda
cha Nyuzi Tabora ili aweze kupata fursa ya kuwauzia nyuzi kwa ajili ya
wakulima wa tumbaku. Kulia ni Meneja wa Kanda wa Bodi ya Pamba Jones
Bwahama.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri(kushoto) akitoa ufafanuzi jana kwa mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi
Tabora alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kujionea hali halisi ya
uzalishaji wa nyuzi. Kulia ni Mkurugenzi wa Kiwanda Mtendaji wa Kiwanda
cha Nyuzi Tabora Urveshi Rajani.
picha na RS_Tabora
Na Mwandishi wetu.
RS –TABORA
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima
wa Tumbaku Kanda ya Magharibi(WETCU) kisema kuwa kinaweza kununua kamba
kutoka Kiwanda cha Nyuzi Tabora kama watakuwa tayari kuzisambaza hadi
kwenye Vyama vya Misingi(AMCOS) na kwa bei nafuu isiyowauza wakulima.
Kauli hiyo ilitolewa jana na
Kaimu Meneja wa Ugavi wa WETCU Bernard Makhanda jana mjini Tabora
wakati wa mkutano wa wadau mbalimbali wanaotumia bidhaa za pamba na
wamiliki wa Kiwanda hicho ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey
Mwanri.
Alisema kuwa hatua hiyo
itasaidia kuhakikisha kuwa WETCU inaunga mkono juhudi za Serikali za
kuinua viwanda vya ndani kwa kununua bidhaa zilizozalishwa hapa nchini
na kufikisha huduma karibu na wakulima wa tumbaku.
Makhanda alisema kuwa baada ya
kupitia maombi ya Kampuni na watu mbalimbali waliomba kusambaza kamba
,wanachosubiri ni kukutana na Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora kwa
ajili ya kujadiliana jinsi ambavyo wanaweza kufikisha bidhaa hizo kwa
wakulima kupitiaa Vyama vyao vya Msingi(AMCOS) badala ya kuishia kwa
WETCU.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Mwanri alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono Kiwanda
hicho kwa kununua bidhaa mbalimbali wanazozalisha kwa ajili ya
kukiwezesha kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa watu wengi na
hatimaye kuongeza mapato ya Serikali.
Aliongeza kuwa wamiliki wa Kiwanda
hicho wamesema wanaweza kuongeza uzalishaji wa nyuzi kwa ajili ya
shughuli mbalimbali kama kama watakuwa na uhakika wa soko.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda
Mtendaji wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora Urveshi Rajani alisema kuwa yuko
tayari kuzalishaji nyuzi nyingi iwapo viwanda vya nguo hapa na Chama
Kikuu cha Ushirika wa wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU)
wakimuunga mkono katika kuchukua bidhaa zake.
Alisema kuwa Kiwanda hicho
kilipunguza uzalishaji kwa sababu ya Viwanda vya hapa nchini vilivyokuwa
vinachukua nyuzi kwake kwa ajili ya kutengenezea nguo kuanza kuagiza
bidhaa hizo kutoka nje ya nchi na hivyo yeye kukosa soko.
Naye Mkuu wa Wilaya Tabora Queen
Mlozi alisema kuwa wapo wakulima wa tumbaku ambao alikutana nao na
kumhakikishia kuwa kamba zinazozalishwa na Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora
ni bora sana.
Kufuatia hali aliwaomba wamiliki wa Kiwanda hicho kuongeza uzalishaji wa kamba kwa kuwa soko lipo kubwa kwa wakulima wa tumbaku.
Kiwanda cha Nyuzi Tabora hivi sasa kinao watumishi 24 badala ya 350 waliokuwepo hapo awali.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora yupo katika
ziara ya kukagua viwanda mbalimbali kuangalia hali halisi ya uzalishaji
wake kama vipo ambavyo vimeshindwa viweze kuchukuliwa kwa ajili ya
kuwapa wawekezaji wengine.
SHARE
No comments:
Post a Comment