Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya
kupokea ripoti mbili za Kamati Maalum za Bunge zilizofanya uchunguzi
wa Biashara ya Madini ya Almasi na Tanzanite Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameamuru wateule wake wote waliotajwa
kuhusika na suala la upotevu wa madini ya Almasi na Tanzanite kukaa
pembeni ili vyombo vya usalama vifanye kazi yake.
Mhe. Rais ameyasema hayo jana
Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti za Kamati za Bunge
zilizochunguza madini ya Almasi na Tanzanite.
Amesema viongozi hao waliotajwa
iwe ni Waziri, Katibu Mkuu, Katibu Tawala, Mkurugenzi au kiongozi yeyote
aache kazi kwani Tanzania haiwezi kuendelea kuibiwa wakati viongozi hao
wanaendelea kuwa serikalini.
Rais Magufuli amesema mapendekezo na yote yaliyoandikwa kwenye ripoti hizo mbili Serikali itayatekeleza kwa asilimia 100.
“Nchi yetu ni ya maajabu kweli, ajabu kubwa mojawapo ni kuwa hata hatujali raslimali zetu,”alisema Rais Magufuli.
Akionyesha kusikitishwa na upotevu
wa raslimali hizo, Rais Magufuli amasema kuwa Tanzania imechezewa kwa
kipindi kirefu na kuwafanya watanzania kuishi maisha magumu wakati
wanaoibia nchi wakineemeka.
“Hao wanaotuchezea wanatuona sisi
si binadamu au ni majitu tu, wangetuona kama binadamu wangetupa basi
asilimia inayofaa,”alisema Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka
watanzania kuwa wazalendo kwa kujali na kuthamini mali na raslimali za
umma ili kuondoa nchi katika utegemezi wakati nchi ina kila kitu cha
kuifanya kuwa tajiri hadi kutoa misaada kwa nchi nyingine.
Ameagiza vyombo vya ulinzi na
usalama kufuatilia mapendekezo na matokeo ya ripoti hizo kwa haraka ili
hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Katika kusisitiza utekelezaji wa
hatua hizo, Rais Magufuli amekabidhi ripoti hizo mbili kwa Mkurugenzi wa
TAKUKURU, Bwana Valentino Mlowola na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Jenerali Venus Mabeyo.
SHARE
No comments:
Post a Comment