Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo
akifafanua jambo alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu kodi
za michezo ya kubahatisha leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Sehemu ya Huduma za
Habari na Picha Bw. Rodney Thadeus na kulia ni Mkuu wa Afisa Uhusiano
Mwandamizi wa TRA, Rachel Mkundai.
Baadhi ya Waandishi wa Habari
wakiendelea na kazi yao wakati wa mkutano baina yao na Mkurugenzi wa
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Richard Kayombo kuhusu kodi za michezo ya kubahatisha leo Jijini Dar es
Salaam.
Picha na: Paschal Dotto – MAELEZO
………………….
Na: Thobias Robert
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
imeanza rasmi kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha kama ambavyo
ilikabidhiwa jukumu hilo kuanzia Julai Mosi 2017 kwa mujibu wa Sheria ya
Fedha ya mwaka 2017.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard
Kayombo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu
utekelezaji wa jukumu la ukusanyaji wa kodi katika michezo hiyo kwa
mwaka wa fedha 2017/2018.
Kayombo alisema kuwa TRA
inakusanya mapato katika michezo mbalimbali ya kubahatisha hapa nchini
kama vile Casino, Sport Betting, Slot Machines, Lottery na kupitia
ujumbe mfupi wa simu (SMS) na kusisitiza kuwa kiwango cha kodi
kinatofautiana kati ya mchezo mmoja na mwingine.
“Jukumu hili limetokana na
mabadiliko ya sheria ambayo yapo katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2017
ambayo imetupa mamlaka kamili ya kusimamia zoezi la ukusanyaji wa mapato
katika michezo ya kubahatisha,” alifafanua Kayombo.
Alibainisha kuwa kwa
wanaojihusisha na michezo hiyo katika Casino wanapaswa kuwasilisha TRA
asilimia 15 ya mapato yatokanayo na mchezo huo kwa wiki na wanaochezesha
michezo ya Sport Betting wanatakiwa kuwasilisha asilimia 6.
Kayombo aliongeza kuwa kwa wale
wanaochezesha michezo hiyo kwa njia ya SMS wanatakiwa kuwasilisha
asimilia 30, kwa michezo ya kitaifa (National Lottery) wanatakiwa
kuwasilisha asilimia 10 na michezo ya slot machine wanatakiwa
kuwasilisha sh. 32,000 kwa mwezi kwa kila machine moja.
“Michezo ya kubahatisha ina pande
mbili yaani mchezeshaji na mchezaji hivyo kila mmoja anapaswa kulipa
kodi, ambapo mshindi wa mchezo huo pia anapaswa kulipa asilimia 18 ya
mapato yake ambayo hukatwa na mchezeshaji na kuiwasilisha TRA,” alisema
Kayombo.
Aidha Kayombo alieleza kuwa TRA
itajikita zaidi katika ukusanyaji wa mapato tu, jukumu la kuratibu na
kuendesha michezo hiyo litabakia kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha hapa
nchini ambayo ndiyo yenye mamlaka na wajibu wa kusimamia michezo yote
ya kubahatisha.
Alisema TRA inashirikiana na Bodi
ya Michezo hiyo katika kutoa elimu kwa wadau wote wanaohusika na michezo
ya kubahatisha wakiwemo wadhamini, wananchi, vyombo vya habari na wadau
wengine.
Pia TRA imetoa wito kwa makampuni
na wadau mbalimbali wanaohusika na michezo ya kubahatisha kuendelea
kutoa ushirikiano katika suala la ukusanyaji mapato yatokanayo na
michezo hiyo kwa ufanisi zaidi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka
2017 kama ilivyopitishwa na Bunge.
Michezo ya Kubahatisha inasimamiwa
na kuendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Board of
Tanzania) ambayo mwanzoni ndiyo ilikuwa na jukumu la ukusanyaji kodi
ambalo kwa sasa limerudishwa TRA kwa mujibu wa Sheria ya Fedha Na. 4 ya
mwaka 2017 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuifanyia
marekebisho.
SHARE
No comments:
Post a Comment