Mkurugenzi wa
Shughuli za Kitakwimu Irenius Ruyobya wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
akizungumza na Waandishi wa Habari jana jijini Dar es Salaam wakati
akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Oktoba, 2017 ambao
umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilimia 5.3
ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017. Kulia Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei
Bi. Ruth Minja.
………………
Na: Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa
mwezi Oktoba, 2017 umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 ikilinganishwa na
asilimia 5.3 ilivyokuwa mwezi Septemba, 2017.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu
Irenius Ruyobya wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) amesema kupungua kwa
Mfumuko wa Bei kunamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na
huduma kwa mwaka ulioishia Oktoba, 2017 imepungua ikilinganishwa na
kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Septemba, 2017.
Ruyobya ameongeza kuwa,
kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017 kumechangiwa na
kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia
mwezi Oktoba, 2017 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba, 2016.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula
zilizochangia kupungua kwa Mfumuko wa Bei ni pamoja na unga wa mtama
kwa asilimia 2.6, samaki kwa asilimia 7.1, matunda kwa asilimia 2.7,
mbogamboga kwa asilimia 7.4, maharage kwa asilimia 2.9, viazi kwa
asilimia 14.4 na karanga kwa asilimia 7.8”, amesema Ruyobya.
Akizungumzia Mfumuko wa Bei
kwa upande wa Afrika Mashariki, Irenius Ruyobya amesema Mfumuko wa Bei
wa Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika
Mashariki ambapo nchini Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Oktoba, 2017
umepungua hadi asilimia 5.72 kutoka asilimia 7.06 mwezi Septemba, 2017
na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 4.8 mwezi Oktoba, 2017 kutoka
asilimia 5.3 mwezi Septemba, 2017.
Mfumuko wa Bei wa Taifa
unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote
zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
SHARE
No comments:
Post a Comment