Mwandishi Wetu,
TJNCDF
KINYWA ni moja ya
viungo muhimu katika mwili wa binadamu hasa ikizingatiwa kwamba kinatumika
kula, kuzungumza, kuhisi na ni sehemu ya uzuri wa sura ya mtu.
Kutoboka meno na
kuharibika fizi vyote vinaweza kuathiri baadhi ya sifa za kinywa, kumfanya mtu
atumie fedha nyingi kwa matibabu na hata kuathiri muonekano halisi wa mtu.
Mfano mzuri ni
kwamba mtu aking’oa meno mengi mdomoni anaweza akaathiri muonekano mzuri wa
mdomo na mashavu, kushindwa kutafuna na hata kutamka maneno vizuri, na
asipokuwa mwangalifu katika kusafisha kinywa pia anaweza kuwa anatoa harufu
mbaya mdomoni.
Kuoza meno ni nini?
Ushirika wa Vyama
Vinavyokabili Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA) katika kuelimisha jamii
juu ya magonjwa ya kinywa inaeleza kuwa kuoza kwa meno ni hali ya sehemu ya juu
ndani ya jino kutoboka kutokana na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye
sukari.
Taarifa hiyo ya
TANCDA inasema vijidudu vya bakteria humeng’enya mabaki vya vyakula vya sukari
mdomoni na kutoa tindikali ambayo husababisha kudhoofu kwa sehemu ya nje ya
meno na baadae hutoboka.
Takwimu zinaonyesha
kati ya asilimia 60 hadi 90 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shule duniani
kote wana ugonjwa wa meno kutoboka.
Hapa nchini, watoto
wenye umri kati ya miaka mine hadi sita, mtoto mmoja kati ya watatu ana jino
lililotoboka au kuoza.
Vyakula
vinavyochochea bakteria kuathiri meno ni biskuti, soda, keki, chokoleti, pipi,
kashata, aisikrimu, visheti na ubuyu wenye sukari.
Dalili za kuoza meno
Kwa kawaida meno ni
meupe, hayana vitobo na kazi yake muhimu ni kukata, kusaga vyakula na kuweka
umbo zuri la mdomo kwa nje na anapotabasamu au kucheka.
TANCDA inaeleza kuwa
dalili za meno kuoza ni alama nyeusi sehemu za pembeni au kutafunia, uwepo wa
shimo kwenye jino au meno, maumivu ya meno, kuvimba sehemu ya fizi au shavu
upande ambao jino au meno yanauma.
Njia za kuzuia
kutoboka au kuoza kwa meno ni kupiga mswaki pamoja na dawa mara mbili kwa siku,
hasa asubuhi na jioni.
Namna nyingine ni
kuhakikisha unaondoa mabaki ya vyakula katikati ya meno kwa kutumia vijiti au
uzi na hakikisha unakula mlo kamili.
Wataalamu wa kinywa
pia wanashauri jamii kuepuka kuoza au kutoboka kwa meno kwa kupunguza ulaji wa
vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kujenga utamaduni wa kuhudhuria kituo
cha afya kwa ajili ya uchunguzi angalau mara moja kwa mwaka.
Kuchunguza afya ya
kinywa, hata kama huumwi ni njia ya kubaini mapema matatizo ya meno au fizi na
kuchukua hatua kabla ya tatizo kujitokeza. Wataalamu husafisha kinywa kwa
kutumia vifaa maalumu vya kuondoa uchafu na kufanya meno na fizi kuwa na afya
njema.
Nini kinatokea kama
jino likitoboka na kutotibiwa mapema? TANCDA inaeleza kuwa matibabu
yasipofanyika mapema mhusika atahisi maumivu, ukakasi au ganzi unapokula vitu
baridi au moto, jino linaweza kuvunjika, na hushindwa kutafuna vizuri chakula.
Matatizo mengine
yanayoweza kujitokeza ni kutoka usaha kinywani, kutoa harufu mbaya na kupungua
kwa ubora wa maisha.
Matatizo ya fizi
Nini maana ya
ugonjwa wa fizi? TANCDA inaelezea ugonjwa wa fizi kuwa ni athari zinazotokea
katika fizi, misuli na mfupa unaoshikilia jino kwenye taya.
Tafiti mbalimbali
zilizofanywa nchini, TANCDA inasema zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wana matatizo ya fizi.
Mtu anaweza
kujiuliza, nini kinachosababisha magonjwa ya fizi? TANCDA inaeleza kwenye
taarifa yake ya uelimishaji jamii kuwa kutosafisha kinywa vizuri ni moja ya
chanzo cha magonjwa ya fizi.
“Kutopiga mswaki kwa
ufasaha husababisha kutengenezwa kwa utando mlaini ambao hujishikiza kwenye
meno na hivyo kuruhusu vijidudu vya bakteria wanaoishi kwenye vinywa
kutengeneza tindikali ambayo huathiri fizi,” inaeleza sehemu ya taarifa ya
TANCDA.
Mambo mengine ambayo
yanaweza kusababisha matatizo ya fizi ni uvutaji wa sigara, mabadiliko ya
homoni kwa wanawake na magonjwa kama vile kisukari, Ukimwi na saratani.
Dalili za ugonjwa wa
fizi ni kutokwa na harufu mbaya mdomoni, fizi kuvimba na kuonekana katika rangi
nyekundu na maumivu au kutoka damu kwenye fizi.
Dalili nyingine ni
kuhisi maumivu wakati wa kutafuna chakula, meno kulegea, meno kuwa na hisia ya
ukakasi na sehemu ya mzizi wa jino kuonekana kutokana na fizi kuharibika.
Magonjwa ya fizi
yasipotibiwa huweza kusababisha maumivu, meno kung’ooka yenyewe au kulazimika
kuyaondoa na kupungua ubora wa maisha.
Kwa mama mjamzito
akiwa na matatizo ya fizi anaweza kusababisha kujifungua mtoto mwenye uzito
pungufu.
Ili kuepukana na
magonjwa ya fizi ni kuhakikisha unapiga mswaki kwa usahihi mara mbili kwa siku;
asubuhi na jioni kabla ya kulala, kuacha kutumia tumbaku na kusafisha meno kwa
kutumia vijiti na uzi.
Makala haya
yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza
(TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA).
Maoni na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam au tjncdf@jmail.com
MWISHO
SHARE
No comments:
Post a Comment