Tufufue viwanda vyetu
Julian Msacky
NOVEMBA 4, mwaka jana, Rais John
Magufuli alijitokeza kwa mara ya kwanza mbele ya wahariri na
kuzungumzia masuala yanayohusu nchi kwa ujumla.
Rais Magufuli alizungumza mengi, lakini kwa muktadha wa safu hii
ninapenda kujadili athari za kukosekana kwa viwanda hapa nchini
kwetu.
Wakati wa majadiliano na wahariri Rais
Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa anataka kujenga nchi ya
viwanda na kwake ni kazi tu.
Niharakishe kusema hapa kuwa chimbuko kubwa la wamachinga
ambao tunahangaika nao leo hii nchini kwetu ni kuua viwanda vilivyokuwepo.
Hakuna asiyefahamu namna Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyojitahidi
kuweka viwanda kila kona ya nchi pamoja na vyama mbalimbali
vya ushirika.
Chini ya uongozi imara wa Mwalimu Nyerere sekta ya viwanda ilionesha
mafanikio makubwa na kuwa kimbilio kwa vijana wengi wa Tanzania.
Ni kipindi hicho ambacho vijana walibaki vijijini wakiendelea
na shughuli mbalimbali za uzalishaji na mijini walikuja wasomi na wafanyabiashara.
Hadi Mwalimu Nyerere anang’atuka
madarakni aliacha viwanda vingi vikifanya kazi, lakini awamu
zilizofuata hazikuangaika na sekta hiyo hadi ilipozirai.
Ni kuanzia wakati huo vijana walioviona vijiji mahali
pasipofaa kuishi kutokana na sekta ya kilimo kukosa mwenyewe pamoja viwanda
kufa kifo cha mende.
Tulikuwa na viwanda vya nguo kila kona ya nchi na hili
viongozi wetu wanalifahamu vizuri, lakini leo hii tunaishi kana kwamba hatujawahi
kuwa navyo.
Viwanda hivyo vilichochea wakulima wa pamba katika mikoa ya
kanda ya ziwa kuongeza kasi ya uzalishaji na kusema kweli hawakuona sababu ya
kuja mijini.
Ninachotaka kusema hapa ni wamachinga tumewataka wenyewe
baada ya kuua viwanda alivyotuanzishia Mwalimu Nyerere na
kuviacha vikiwa magofu.
Swali linaloulizwa na wengi kwa sasa ni je, Rais Magufuli
atahimili misuli ya mataifa makubwa ambayo hayapendi kuona viwanda katika nchi
maskini?
Tunavyofahamu ni kuwa viwanda vilivyokufa kwa namna moja au nyingine
mataifa hayo yana mikono yao. Kama hivyo ndivyo
yatamsaidia Rais huyo?
Mataifa hayo yatamsaidia kujenga viwanda au watapalilia wimbi
la wamachinga wazidi kuzagaa miji mbalimbali nchini?
Na je, tumejipanga kiviwanda?. Shirika la Fedha Dunia (IMF)
na Benki ya
Dunia (WB) zitakubali ndoto ya Rais Magufuli itimie katikati
ya sera zisizopenda mkulima asaidiwe hata kwa ruzuku?
Uzoefu unaonesha kuwa mataifa makubwa
yanaishi au yanazidi kupiga hatua kwa kutumia
rasilimali zinazotoka katika nchi zetu
zinazoitwa maskini.
Kwa hiyo ili viwanda vya wakubwa hao
viendelee kufanya kazi kusema kweli itabidi waue kabisa mfumo
wa uzalishaji katika mataifa machanga kama Tanzania.
Suala hili wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu siku
hizi viongozi wetu wamejiweka kando katika masuala muhimu na kuachia sekta
binafsi.
Wanaambiwa wasijiingize katika biashara wala
kusimamia viwanda vyake kwani kufanya hivyo ni sawa na dhambi
isiyovumilika.
Kama ni mkulima asipewe ruzuku yoyote na badala yake aendeleze
sekta ya kilimo kwa nguvu zake mwenyewe eti kwa jembe lile lile la mkono.
Wakati wakisema hivyo kwa viongozi wetu serikali zao zipo
tayari kumhudumia ng’ombe mmoja kwa kutoa ruzuku ya dola zaidi ya mbili ili
kumbeba mfugaji.
Hizi zote ni jitihada tu za kuhakikisha nchi zetu hazipigi
hatua yoyote ya kujivunia ili
tuendelea kuwa vibaraka wao hata karne hii ya sayansi na
teknolojia.
Hii ina maana kuwa wakati nchi changa
zikikata mnyororo mguuni nchi tajiri zinazidi kuukaza ili
tusiondoke hapa tulipo kwa usalama wa nchi zao.
Ndiyo kusema Rais Magufuli ili atimize ndoto yake ya kuwa na
nchi ya viwanda itabidi afanyekazi ya ziada na kuwa na ujasiri kama alivyokuwa
Mwalimu Nyerere.
Tukijenga ama kufufua viwanda vilivyo tuna uhakika wimbi la
wamachinga lililozagaa nchini litapungua, lakini tutaweza au tutaishia tu
kusema?
Kama nilivyowahi kushauri siku za nyuma
kuwa hakuna sababu ya Rais Magufuli kujenga viwanda
kinachotakiwa ni kufufua vilivyopo.
Tukifufua viwanda vya nguo tutapanua wigo wa ajira kuanzia
kwa wakulima wa pamba.
Tukifufua viwanda kama machine tools
tutapunguza wamachinga mitaani.
Si hivyo tu bali tukifufua viwanda tutaweka mazingira mazuri
ya nchi kujipatia fedha za kigeni na kuepusha nchi kuwa jalala la kutupa bidhaa
za ovyo ovyo.
Ili kufanikisha ufufuaji wa viwanda na
kuhakikisha wamachinga wanaondoka au
kupungua katika miji yetu ni lazima viongozi wetu wafanyie
kazi ya ziada.
SHARE
No comments:
Post a Comment