Kampuni
za
simu ni
shida
Julian Msacky
MIAKA ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kampuni za
simu nchini na bara zima la Afrika.
Simu hizo zimekuwa kiungo muhimu katika kurahisisha
mawasiliano kutoka mtu mmoja hadi mwingine.
Ni jambo la kawaida siku hizi kuzungumza na ndugu wa kijijini
bila tatizo kwa sababu ya uwepo wa simu za mkononi.
Kwa lugha nyingine zimekuwa mkombozi mkubwa wa mawasiliano
kuanzia mijini hadi kijijini.
Ni tofauti kabisa na miaka ya nyuma ambako ukitaka kumpigia
mtu simu hadi ufungashe safari ya kutwa nzima.
Hapa ilimlazimu mtu kutumia fedha nyingi za nauli ili tu
akazungumze na mhusika. Walioishi vijijini wanajua hili.
Lakini siku hizi mawasiliano yapo kiganjani mwa Watanzania na
wengi wao wanamiliki simu za mkononi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) idadi ya
Watanzania waliokuwa wanatumia simu Machi mwaka 2012 ni zaidi ya milioni 26.
Hii ni kuonesha namna teknolojia ya mawasiliano ya simu
ilivyopiga hatua nchini kwetu na hii ni faraja kubwa.
Mbali na kurahisisha mawasiliano ya mtu na mtu, simu za
mkononi ni chanzo kingine cha mapato.
Ndiyo maana zinatoa huduma mbalimbali za kifedha na kusema
kweli zimechangia pia kuongeza ajira.
Kadiri siku zinavyosogea ndivyo mawasiliano ya simu
yanavyozidi kuwa muhimu kwa watu wengi.
Hii ikiwa na maana kuwa ukiwa na simu ya mkononi unapata
taarifa zote muhimu unazohitaji.
Ndiyo maana idadi ya watumiaji wa simu inaongezeka hadi siku
huku kampuni zikizidi kujikusanyia fedha.
Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU) linasema idadi ya watu
wanaotumia simu za mkononi kote duniani imefikia bilioni sita.
Idadi hiyo inamaanisha kuwa kwa kila watu mia moja kote ulimwenguni,
watu themanini na sita wana simu za mkononi.
Kama hiyo
haitoshi shirika hilo linasema zaidi ya watu bilioni 2.3, ambao ni zaidi ya theluthi
moja ya idadi ya watu hao duniani, wameunganishwa na mtandao wa intaneti.
Ripoti hiyo
inasema Jamhuri ya Korea Kusini ndiyo nchi iliyoendelea zaidi katika sekta ya
teknolojia ya habari na mawasiliano, ikifuatiwa na Sweden, Denmark, Iceland na
Finland.
Haya ni
mabadiliko makubwa ya kiteknolojia si tu kwa hapa nchini lakini na duniani kwa
ujumla.
Pamoja na
uzuri wa simu za mkononi, lipo jambo ambalo baadhi ya kampuni zinakera wateja
wake.
Mteja
anaweza kuingiza salio la sh. 2000 lakini kabla hajatumia anaambiwa umekatwa
sh. 500 au 300 kwa sababu umeunganishwa na huduma fulani.
Wakati
akipewa taarifa hiyo mteja husika hajaomba kujiunganisha na huduma yoyote,
lakini anatumiwa ujumbe mfupi wa maneno kuwa “umeunganishwa na huduma hii”.
Suala hili
limegeuka kero na wakati mwingine kuonekana kama wizi wa mchana kwani mteja
anachukuliwa fedha bila ridhaa yake.
Tatizo hili
tayari limeniathiri mimi binafsi na baadhi ya watumiaji wa simu ambao walikiri
mchezo huu upo.
Swali hapa
ni je, kampuni za simu zinafahamu suala hilo au zinalifumbia macho kwa sababu
tu pilipili usioila inakuwashia nini?
Kusema kweli
huo ni mchezo mchafu na kampuni zinatakiwa kubadilika kwani zinawapa watu
hasara.
Mteja
anapoweka salio la sh. 500 anataka awasiliane na watu anaotaka na si
kurudishiwa ujumbe wa kukatwa kiwango fulani tena cha fedha.
Kinachosikitisha
ni kukatwa fedha bila kuomba huduma husika.
Hali hii
inasababisha baadhi ya kampuni za simu zionekana zipo kwa ajili ya kuchuma
zaidi kuliko kutoa huduma bora kwa mteja.
Endapo hali
hiyo itaendelea ipo hatari kwa baadhi ya kampuni kujikuta zikikimbiwa kwa sababu
ya kukosa uadilifu kibiashara.
Kwa msingi
huo kuna umuhimu wa kampuni zinazofanya mchezo huo kubadilika kwani si mzuri
kwa wateja.
Ni vema
viongozi wanaosimamia kampuni hizo kuhakikisha dosari hizo zinaondoka ili
kulinda wateja.
Kama mchezo
huo unafanywa na baadhi ya wafanyakazi ni jukumu la viongozi kubaini yalipo
madudu hayo.
Kampuni
zinatakiwa kumlinda mteja na si kuendelea kumkamua kwa huduma ambazo
hajajiunganisha nazo kama inavyolalamikiwa na watu wengi hivi sasa.
0718981221,
msackyj@yahoo.co.uk
SHARE
No comments:
Post a Comment