TRA

TRA

Wednesday, February 15, 2017

Mikoa ya Dar, Pwani na Morogoro yashauriwa kujikita katika kilimo na ufugaji

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


WANANCHI katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam inayopatikana kanda ya mashariki wametakiwa kujikita katika kilimo na ufugaji ili kujiinua kiuchumi kwani ndizo shughuli zinazoleta maendeleo ya haraka hasa kutokana na rasilimali zilizopo nchini.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe, mkoani Pwani jana wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya viongozi na waratibu wa uwezeshaji kutoka mikoa hiyo mitatu yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Dkt. Kebwe alisema, ni ajabu kuona Tanzania inashindwa kupiga hatua kiuchumi huku ikiwa na eneo kubwa la kilimo na mifugo kuliko baadhi ya mataifa mengine duniani.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt.Kebwe Steven Kebwe akisisiiza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa Viongozi na Waratibu wa Uwezeshaji katika Kanda ya Mashariki mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro mafunzo hayo yanafanyika Kibaha mkoani Pwani na kuratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi(NEEC), Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi NEEC, Dkt.John Jingu . wapili kushoto ni Katibu Mtendaji wa NEEC,Bi.Beng’i Issa. Kulia kwake ni Katibu Tawala- Pwani, Bw.Zuberi Semataba na wapili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha,Bi.Asumpta Mshama.

“Tanzania ina ng’ombe milioni 26 sawa na nchi ya Australia, kwa taarifa yenu Australia kwa mwaka wanaingiza Sh trilioni 28 kutokana na bidhaa za mifugo hiyo ni sawa na bajeti yetu ya serikali kuu. Tuna utajiri mkubwa hatuna sababu ya kulalamika, kwa sababu Morogoro tu ni sawa na nchi ya Malawi pamoja na maji yake na ardhi.

“Kwa hiyo viongozi mliofika katika mafunzo haya muondoke mkiwa mmepikwa hasa kwa kuwa muongozo huu ndio dira ya kusimamia uwezeshaji wananchi kiuchumi, wananchi wakiendelea kiuchumi maana yake taifa limeendelea,” alisema Dkt. Kebwe.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa wa Morogoro ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo aligusia suala la nchi kujitegemea kiuchumi ili kuondokana na aibu ya kutegemea wahisani.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC),Bi.Beng’i Issa akisisitiza jambo wakati ufunguzi wa mafunzo ya siku nne kwa Viongozi na Waratibu wa Uwezeshaji katika Kanda ya Mashariki mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro , mafunzo hayo yanafanyika Kibaha mkoani Pwani na yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi(NEEC). Kushoto kwake ni mwenyekiti wa bodi NEEC, Dkt.John Jingu na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Kebwe Steven Kebwe.

“Ng’ombe kuanzia kwato hadi pembe ni mali tupu, tutumie viwanda vyetu kuwawezesha wafugaji kujinufaisha kiuchumi. Taifa kuwa tegemezi kwa wahisani ni aibu, utajiri tunao kikubwa ni kujipanga kwa sababu wapo watu wana ng’ombe zaidi ya 10,000 halafu bado wanaitwa wafugaji hapana hao ni wawekezaji wanaweza kuajiri watu na kulipa kodi,” alisema Dkt Kebwe.

Akimkaribisha mgeni rasmi Mwenyekiti wa NEEC, Dkt. John Jingu alisema ili taifa liendelee lazima wananchi walio wengi wasaidiwe namna ya kujiletea maendeleo, ndio maana wakachagua kuwawezesha wakulima na wafugaji kwa kuwa ndilo kundi kubwa.

“Wakulima ndio wanaotulisha lakini hawana mitaji, wafugaji nao ni wawekezaji lakini hawana mikakati mizuri ya malisho. Katika mikakati yetu tunatafuta namna ya kuondokana na vurugu za wakulima na wafugaji kugombania ardhi kwa kuunganisha wafugaji wadogo katika ranchi moja.
Viongozi na Waratibu wa Uwezeshaji wa Kanda ya Mashariki wakifuatilia wakisikiliza mada wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo viongozi hao juu ya dhana ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia fursa zilizopo katika maeneo yao. Mafunzo hayo yameratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (NEEC).

“Kwa mfano ranchi ya Kongwa ina uwezo wa kuchukua ng’ombe 20,000 lakini hadi sasa ina ng’ombe 9,000 tu. Hilo eneo lililobaki tunaweza kuunganisha wafugaji wadogo wenye ng’ombe kuanzia 200 wakawekwa pamoja itasaidia kupata malisho ya uhakika na kuiepusha mifugo na maradhi ambayo hushusha thamani ya ngozi, nyama na maziwa,” alisema Dkt Jingu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa, alisema lengo la mafunzo hayo ni kujadiliana kwa pamoja na viongozi ili kupata njia muafaka za kuwakwamua wananchi na machungu ya umasikini.

“Lengo la baraza hili ni kusimamia, kuonyesha njia, kufanya utafiti na kutafuta fedha kwa ajili ya kuwainua wananchi kiuchumi. Tunataka kila kiongozi kufanya kazi katika maeneo yao kwa sabbu wapo ambao hawajui mipaka na kulazimika kufanya kazi za wengine.

“Matarajio yetu baada ya mafunzo haya kila aliyehudhuria atakuwa na taarifa sahihi pamoja na nia ya kusaidia wananchi, kwa sababu wananchi wanahitaji kuelekezwa na kusimamiwa katika kila shughuli za kiuchumi wanazofanya,” alisema Bi. Beng’i.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya waliohudhuria mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Ally Hapi alisema “Sisi ndio tunaokaa na wananchi na kujua matatizo wanayokumbana nayo, kwa muda mrefu katika wilaya yangu tunakabiliwa na tatizo la ajira kwa hiyo tuanpiga kelele viajana wajiajiri.

“Kama mnavyofahamu Kinondoni ni wilaya ya mjini hakuna wakulima wala wafugaji asilimia kubwa ni wafanyabiashara, lakini kuna aina mpya ya ufugaji kama kuku, samaki na kilimo cha Greenhouse, vilevile kuna vikundi vya usindikaji uyoga, maembe na matund amengine. Tulijipanga kuandaa programu ya mafunzo ya usindikaji kwa vijana 10,000 tayari vijana 3,000 wameshapata mafunzo, pia ufugaji wa samaki hauhitaji maeneo makubwa nio biashara yenye tija katika wilaya yangu,” alisema Hapi.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt.Kebwe Steven Kebwe(katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakuu wa Wilaya wa Kanda ya Mashariki mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro mara baada ya kufungua mafunzo ya siku nne kwa Viongozi na Waratibu wa Uwezeshaji wa Kanda hiyo yanayofanyika Kibaha mkoani Pwani. Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi(NEEC).

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger