Timu ya Taifa ya Tanzania ya Vijana
wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys,
imefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye
umri huo.
Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF), imethibitisha hilo pasi shaka kwamba Tanzania ndiyo yenye
nafasi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Aprili 2, mwaka
huu huko Gabon baada ya Madagascar kuenguliwa kutokana na kutoandaa vema
fainali hizo.
Taarifa hizo za CAF kutoka Libreville,
nchini Gabon zinathibitisha kwamba Kamati ya Utendaji ya CAF imeipa
ushindi Tanzania dhidi ya timu ya Jamhuri ya Congo ambayo katika
michuano ya kufuzu, ilimchezesha mchezaji Langa Lesse Bercy aliyezidi
umri kinyume cha kanuni za kanuni za michuano hiyo.
Serengeti Boys iliyosimamiwa na Kamati
ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Jamal Malinzi, sera kubwa ilikuwa ni
kuangalia kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana, ilikusanywa na
kuandaliwa kwa michezo mingi ya kimataifa ambako kwa mwaka moja tu 2016,
ilicheza mechi zisizopungua 16 ya kimataifa.
Katika michezo hiyo ya kirafiki na
ushindani, Serengeti Boys ilipoteza mchezo wa 16 tu dhidi ya Congo
ilihali kulikuwa na rufaa kuhusu mmoja wa wachezaji wa Congo ambaye
alionekana kuwa na umri mkubwa. Mchezaji huyo ni Langa Lesse Bercy.
CAF, kwa nyakati tofauti ikiwamo Novemba
10, 2016 na Desemba 15, mwaka jana walitoa agizo kwa Congo Brazzaville
kumpeleka kijana huyo Cairo, Misri kwa ajili ya vipimo vya MRI ili
kuthibitisha au kupangua madai ya Tanzania. Congo Brazzaville
hawakupeleka.
Januari 12, mwaka huu 2017 iliamriwa kwa
mara nyingine kijana huyo kupelekwa jijini Libreville, Gabon ili
kufanyiwa vipimo vya MRI, lakini hakupelekwa na katika kikao cha Kamati
ya Utendaji ya CAF, kimeamua kumaliza suala hilo na kuipa ushindi
Tanzania.
Siku 10 ziliisha Januari 23, mwaka huu
lakini tangu hapo kumekuwa na maswali ya kutosha kuhoji nafasi ya
Tanzania yakitoka kwa Watanzania kupitia wanahabari, lakini TFF
ilisimama kidete kutangaza kuwa tunasubiri uthibitisho wa CAF ambayo leo
Februari 3, mwaka huu imetangaza rasmi kuwa Tanzania itacheza fainali
hizo.
SHARE
No comments:
Post a Comment