Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Meneja Uhusiano wa TTCL Ndg Nicodemus Thom Mushi amesema, TTCL inathamini sana makundi yenye mahitaji maalumu kama Yatima ndio maana mara zote imekuwa mstari wa mbele kuwasaidia kadiri uwezo wa Kampuni unavyoruhusu.
“Nawaomba mpokee salamu za Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndg Waziri Kindamba, anawasalimu na kuwatakia kila la kheri katika kukamilisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sherehe njema za Eid. Watoto wanaopata malezi katika vituo vyenu wana haki sawa na watoto wenye wazazi na wanaoishi na familia zao. Kwa ushiriano mwema kati yetu, tutawezesha Watoto hawa kukua salama na kua Raia wema wa nchi yetu na nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa letu” amesema ndugu Mushi.
Akishukuru kwa Niaba ya Vikundi vilivyopokea msaada, Mkuu wa Kituo cha New Life Orphanage home cha Boko Dawasa Bi Mwanaisha Magambo amesema, Kituo chake chenye watoto 132 kitafaidika sana na msaada huu wa TTCL uliowafikia wakiwa wamekata tamaa kwa kutopata msaada wowote katika sherehe hizi. Nawaombea kwa Mungu, Kampuni hii idumu, mfanikiwe katika malengo yenu yote.
Msaada huu ni mkubwa, hatukuutarajia na tulikuwa tumekata tamaa kwa kuwa maombi yetu yote hayakupata majibu kutoka kwa Wafadhili wetu. Mmetushika mkono kipindi tulichowahitaji hasa, Mungu awabariki sana TTCL, msichoke kusaidia kundi hili la watoto lenye mahitaji makubwa ya msaada hasa wa chakula na vifaa vya Elimu.
Msaada wa TTCL umetolewa kwa vikundi Viwili vya New Life Orphanage Home (Watoto 132) na Kituo cha Sifa Group Foundation cha Vikawe Bondeni chenye watoto 50. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Mchele kg 300, Unga wa mahindi kilo 300, Unga wa Ngano kg 200, Sukari kg 200, Maharage kg 200, Mafuta Ndoo 6, Mbuzi 2, Soda katoni 40, Maji Katoni 40, Juice Katoni 80 na Viungo mbalimbali vya chakula na vifaa vya nyumbani kama mafuta ya kujipaka na Sabuni.
SHARE
No comments:
Post a Comment