Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akizungumza na madiwani na watendaji katika baraza maalumu la
madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni la kujadili hoja za Mkaguzi
na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Watendaji wa halmashauri ya Wilaya
ya Manyoni wakifuatilia kwa umakini hoja zikijadiliwa katika baraza
maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali.
Madiwani wa halmashauri ya Wilaya
ya Manyoni wakifuatilia kwa umakini hoja zikijadiliwa katika baraza
maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni
Miraji Mtaturu akizungumza katika baraza maalumu la madiwani la kujadili
hoja za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
Mkaguzi wa ndani na Mweka hazina
wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni wakipitia hoja zilizowasilishwa
katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na
Mdhibiti wa Hesabu za Serikali.
……………………………
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi ameagiza na kutoa mwezi mmoja mali za watendaji 21 wa vijiji
katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni zitaifishwe na kuuzwa ili
kufidia fedha walizotumia za chakula cha njaa katika kipindi cha mwaka
2012.
Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo
katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za mkaguzi na
mdhibiti wa hesabu za serikali ambapo kulikuwa na hoja ya watendaji wa
vijiji 30 waliokusanya kwa wananchi shilingi milioni 15,268,700 kwa
ajili ya chakula cha njaa na hawakuziwasilisha katika halmashauri hiyo.
Amesema kitendo hicho ni wizi na
hakistahili kuvumiliwa licha ya watendaji tisa kurejesha kiasi cha
shilingi milioni 3,277,000 na hivyo kusalia watendaji 21 wanaodaiwa
shilingi milioni 11,991,700 walizokusanya.
“Huu ni wizi na hatutauvumilia,
hao watendaji wa vijiji hakikisheni wanarudisha fedha za serikali, Mkuu
wa Wilaya na Mkurugenzi, anzisheni utaratibu wa mahakama tembezi
muwafuate huko waliko, kamateni mbuzi, kuku, uzeni tupate hiyo fedha na
zoezi hilo lifanyike ndani ya mwezi wa nane” ameagiza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kwa kusema kuwa,
“watendaji hawa nasikia wengine wameshaandikiwa barua za onyo zaidi ya
mara tatu, kwanini wanaendelea kuwa watumishi wa umma?, kwanini wasikae
pembeni tupate watanzania wengine wazalendo wazibe nafasi hizo?. Hawa
hawafai kuwa watumishi wa umma, ila hakikisheni kwanza fedha inarudi
ndipo hatu nyingine zichukuliwe”.
Dkt. Nchimbi amesema hoja nyingi
katika halmashauri hiyo zimetokana na uzembe wa watumishi pamoja na
kutegemea taarifa za makaratasi badala ya kutembelea maeneo husika
kujionea hali halisi ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali
mpaka ngazi ya vijiji na mitaa.
Aidha amemtaka mwanasheria wa
halmashauri na mkaguzi wa ndani kuisaidia halmashauri kuepuka kuwa na
hoja nyingi zinazoepukika kwa kutoa ushauri sahihi na kwa wakati, huku
akiwasisitiza watumishi wote kubadilika, kuacha uzemba na kufanya kazi
kwa mazoea bali waendane na kasi ya serikali ya awamu ya tano.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Nje wa
Hesabu za Serikali Anna Kakunguru amewataka viongozi kuhakikisha
wanasimamia ili hoja zifungwe kabla ya watendaji waliosababisha hoja
hizo kustaafu, kuhama au kuachishwa kazi ili kuepuka hasara.
Kakunguru amesema imekuwa
ikichukua muda mrefu kwa halmashauri kufuta hoja jambo linalosababisha
waliotengeneza hoja hizo kutopatikana na kuzijibu ili halmashauri
isibaki na hoja nyingi.
Ameongeza kuwa uwepo wa hoja za
serikali ni kiashiria kuwa kuna sehemu katika utendaji wa halmshauri
kuna mapungufu au umelegalega na hivyo halmashauri inapaswa kushirikiana
na Mkaguzi wa nje na ndani ili kurekebisha na kuzuia kabisa udhaifu
huo.
Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Manyoni Miraji Mtaturu amesema atahakikishika kufikia tarehe 30 Agosti
watendaji 21 watakuwa wamerejesha fedha walizochukua za wananchi huku
akiagiza apatiwe orodha ya watendaji hao ili aweze kuwashughulikia
vizuri.
Mtaturu ameongeza kuwa atasimamia
kikamilifu ili mahakama tembezi itakayoanzishwa iweze kutekeleza agizo
hilo na kurejesha fedha hizo na endapo watatokea watendaji watakaokaidi
kutoa ushirikiano atawachukulia hatua zaidi za kisheria.
Ameongeza kwa kumtaka Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manyoni kuweka utaratibu wa kukutana na watendaji wake
mara mbili kwa mwezi ili wajadili namna ya kufuta hoja zilizojitokeza
pamoja na kupeana maelekezo ya namna ya kuepuka kutengeneza hoja
nyingine.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa
Singda Dkt Rehema Nchimbi amewashauri madiwani wa halmashauri hiyo
kutenga ekari tano kwa ajili ya kilimo cha korosho katika kata zao ili
kuongeza kipato kwa wananchi wao, kutunza mazingira na kufikia lengo la
kuwa wazalishaji wakubwa wa korosho nchini.
Dkt Nchimbi pia ameshauri madiwani
hao na watendaji kutofanya mzaha na waliovamia misitu ya hifadhi
kwakuwa wanahatarisha usalama wa raia kutokana na wanyama kutoka katika
hifadhi na kuvamia makazi ya watu.
Amesema “Tusifanye mzaha kwa hili,
na hakuna siasa hapa, sio kwamba tunawajali wanyama kuliko wananchi
hapana, watu wameingia katika maeneo ya hifadhi wamesababisha wanyama
watoke huko na kuja kuvamia watu, mpaka sasa wananchi saba
wameshafariki, tuwe wakali kweli kwa wavamizi hawa”.
Halmashauri ya Manyoni imepata
imepata hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za
Serikali na hoja zilizojadiliwa katika baraza hilo maalumu ni 74 ambazo
zilikuwa hazijafungwa kwa kipindi cha mwaka 2012/13 mpaka 2015/16.
SHARE
No comments:
Post a Comment