Chama cha Hamas kinasema kimekubaliana na hatua za
kuelekea kwenye utatuzi wa mpasuko wa muongo mzima na chama cha Fatah
kinachoongozwa na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina.
Tangazo hilo la leo (Jumapili Septemba 17) linasema kuwa Hamas iko
tayari kukivunja chombo kinachoonekana kama serikali hasimu na iko
tayari kwa uchaguzi.Taarifa hii inakuja baada ya viongozi wa Hamas kukutana na kwa mazungumzo na maafisa wa Misri wiki iliyopita na wakati Ukanda wa Gaza unaoongozwa na chama hicho kukabiliwa na hali ngumu zaidi ya kimaisha.
Hamas inasema imekubaliana na matakwa makubwa ya Fatah, likiwemo la kuivunja "kamati ya utawala" iliyoundwa mwezi Machi, huku pia ikielezea kuwa tayari kwa uchaguzi na mazungumzo juu ya uundwaji wa serikali ya pamoja.
Hamas yataka Fatah waende Gaza
Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniya, anawataka wenzake wa Fatah kuanza kazi pamoja.
Vile
vile, Hamas imetoa wito kwa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina
iliyo na makao yake kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel
"kuja Gaza kufanya kazi zake na kutekeleza majukumu yake haraka
iwezekanavyo."Mkuu wa Hamas, Ismail Haniya, alikubaliana na hatua hizo kwenye mazungumzo yake na maafisa wa Misri mjini Cairo wiki iliyopita, afisa mmoja wa Hamas ameliambia shirika la habari la AFP.
Hata hivyo, haikufahamika endapo hatua hizo zitapelekea nyengine kubwa zaidi kuelekea kukomeshwa kwa mgawanyiko mkubwa uliopo kati ya Hamas na Fatah.
Kwa sasa, Hamas inaendelea kuendesha utawala wake mbali na ule wa Fatah katika Ukanda wa Gaza na ina dhamana ya mambo yote ya usalama kwenye eneo hilo. Juhudi za hapo awali kuutatua mkwamo huu zilifeli mara kadhaa.
Fatah yaipokea kauli kwa mashaka
Rais Abbas wa chama cha Fatah alilipokea tangazo hilo, akisema ni matokeo ya "vikao vizito" kati ya wawakilishi wa Fatah na wale wa idara ya ujasusi ya Misri.
Afisa wa Fatah, Azzam al-Ahmad, alisema kuwa mkutano wa pande mbili na Hamas utaitishwa ili kupanga mwelekeo unaofuatia.
"Kutakuwa na hatua muhimu ndani ya siku chache zijazo, kwa kuanzia na serikali ya umoja wa wa kitaifa ya Palestina kurejea kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria katika Ukanda wa Gaza kama ifanyavyo katika Ukingo wa Magharibi, ili kuendeleza juhudi za kupunguza mateso ya watu wetu kwenye ukanda huo na kulifanyia kazi suala la kuondoa mzingiro wa kidhalimu," Ahmad aliliambia shirika rasmi la habari la Palestina, Wafa.
Ukanda wa Gaza umekuwa chini ya mzingiro wa Israel kwa takribani muongo mzima sasa, huku mpaka wake na Misri nao ukiwa umefungwa takribani wote ndani ya kipindi cha miaka ya hivi karibuni.
Kwa sasa, Abbas yuko mjini New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambako amepangiwa kuhutubia siku ya Jumatano (Septemba 20).
CHANZO: DW
SHARE
No comments:
Post a Comment