NA BEATRICE
LYIMO-MAELEZO, DODOMA
SERIKALI imemshtaki John Hima (29) kwa kosa la kushindwa
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Namba 9 ya mwaka 2015.
Akisoma kesi hiyo namba 9 ya mwaka 2018 katika Mahakama ya
Wilaya ya Bahi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Suniva Mwajumbe, Inspekta
Msaidizi Amani amesema kuwa mshtakiwa ametenda kosa hilo Januari 7 mwaka huu
katika kijiji cha Nghulukano, Kata ya Chikola, Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa ni mwajiriwa wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwa ni mkusanya taarifa (mdadisi) katika Utafiti wa
Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa Mwaka 2017/2018 kwa Tanzania Bara.
Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mdadisi Hima alikana
mashitaka na kesi hiyo itasomwa tena tarehe 7 Februari, 2018 ambapo amerudishwa
rumande baada ya kukosa wadhamini.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, Mwanasheria
wa NBS Oscar Mangula amesema kuwa, mtuhumiwa Hima aliingia mkataba na NBS kuwa
mmoja wa wadadisi wa Utafiti huo unaoendelea hivi sasa ambao ulianza Desemba
mwaka jana.
“Kwa mujibu wa sheria akiwa kama mdadisi majukumu yake alitakiwa
kuwa katika eneo la kazi kulingana na mkataba na kiapo
alichopata ambapo yeye kwa makusudi aliamua kutelekeza majukumu hayo
na kuwa nje ya kituo cha kazi hivyo kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ametenda
kosa la kijinai” amesema Mwanasheria Mangula.
Mwanasheria Mangula ameongeza kuwa, “Mkataba wa kazi ni wa miezi
12 ambapo ulianzia Desemba 2017 hadi Novemba 2018 lakini mdadisi huyu aliacha
kutimiza majukumu yake kuanzia tarehe 7 Januari ambapo sisi tulifika pale tarehe
13 na 14 Januari mwaka huu ila hakuweza kufanya kazi yake kama ilivyotakiwa”.
Mwanasheria Mangula alieleza kuwa kesi hiyo inawakumbusha
wadadisi waliopewa jukumu la kukusanya taarifa za kitakwimu kutekeleza majukumu
yao kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira, kiapo na mafunzo waliyopewa ili
kuepuka kutenda makossa ya kijinai kama analodaiwa kutenda na mtuhumiwa.
Aidha, inawakumbusha wananchi umuhimu wa kuendelea kutoa
ushirikiano kwa wadadisi mbalimbali wanaopewa jukumu la kukusanya taarifa za
kitakwimu kwani kufanya hivyo ni kutekeleza matakwa ya Sheria ya Takwimu ya
mwaka 2015.
SHARE
No comments:
Post a Comment