TRA

TRA

Monday, January 22, 2018

Namna mazoezi yanavyotibu matatizo ya moyo, mishipa ya damu

Share On Facebook ! Tweet This ! Share On Google Plus ! Pin It ! Share On Tumblr ! Share On Reddit ! Share On Linkedin ! Share On StumbleUpon !


Mwandishi Wetu, TJNCDF
Wagonjwa wengi wenye tatizo la shinikizo la damu hushindwa kufanya mazoezi ya mwili kutokana na ukweli kwamba, yanalazimisha moyo kufanya kazi ya ziada.

Wagonjwa wengi wa moyo wanapojaribu kufanya mazoezi, hukabiliwa na uchovu pamoja na kushindwa kuongeza pumzi.

Dalili hizi huwafanya wengi wao kuishi bila kuushughulisha mwili, jambo ambalo huathiri zaidi afya zao, mipango yao ya kiuchumi na ubora wa maisha kwa ujumla.
Ingawa mazoezi hufikiriwa kuwa ni hatari kwa wagonjwa wenye maradhi ya moyo, tafiti za hivi karibuni zinabainisha kuwa mazoezi ni muhimu sana kwa watu wenye maradhi haya.

Tafiti za kitabibu zinaonesha kuwa, mazoezi huwasaidia wagonjwa wa moyo kutumia hewa ya oksijeni vizuri na kwa faida.
Mazoezi pia huongeza mzunguko wa damu katika misuli mwilini na hupunguza kiasi cha lehemu mbaya mwilini, uwezekano wa kupata magonjwa yatokanayo na uvimbejoto, uwezekano wa kulazwa hospitalini mara kwa mara, matumizi ya dawa na vifo vya mapema.
Hii ni kwa mujibu wa Julie Adsett na Robbie Mullins wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Queensland cha Uingereza, katika chapisho lao la ushahidi wa kisayansi kuhusu faida za mazoezi kwa watu wenye maradhi ya moyo ya muda mrefu, lililotolewa mwaka 2010.
Katika makala yake iliyochapishwa katika jarida la Chama cha Madaktari wa Marekani (JAMA) toleo la 288(16) la mwaka 2002, Dk. Jonathan Myers (PhD) wa kitengo cha magonjwa ya moyo katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani, anasema kwamba wagonjwa wapya wanaogunduliwa kuwa na shinikizo la damu, wanapata nafuu haraka wanaposhiriki katika mazoezi.
Lakini wanaweka bayana kuwa kabla ya kuanza programu ya mazoezi, watu wenye maradhi ya moyo wanahitaji kupata uchunguzi na uangalizi wa karibu wa daktari bingwa. Wagonjwa hawa wanashauriwa kufanya mazoezi mepesi na wasitumie muda mrefu sana.
Watu wenye matatizo ya moyo wanaweza kufanya mazoezi ya kutembea, kukimbia taratibu na kuendesha baiskeli kwa mwendo mdogo. Watu hawa pia wanaweza kufanya mazoezi ya kunyoosha misuli pamoja na kukunja na kukunjua viungo vya mwili mara kwa mara.

Mambo ya kuzingatia
Inashauriwa kuepuka mazoezi yanayohusisha kubeba uzito mkubwa na mazoezi kama vile pushapu. Pia ni vizuri kujiepusha na mazoezi katika sehemu zenye baridi kali hasa nje ya nyumba au katika sehemu zenye joto kali sana.
Wataalamu wa tiba za mazoezi wanapendekeza kuanza kwa mazoezi mepesi na taratibu, huku ukiongeza kadri siku zinavyokwenda na kwa kadri unavyoendelea kujisikia vizuri. Simamisha mazoezi mara moja pale unapojisikia kuchoka, kizunguzungu, moyo kudunda bila mpangilio, kifua kuuma, kichefuchefu au kuishiwa pumzi.
Andika kwenye daftari dalili yoyote inayojitokeza, wakati ilipotokea na aina ya mazoezi uliyokuwa unafanya wakati dalili hiyo ilipojitokeza. Mweleze daktari wako kuhusu taarifa hizo pale utakapokwenda kupata ushauri au huduma za kitabibu. Usifanye mazoezi kama hujisikii vizuri au kama ulikuwa mgonjwa sana katika siku za karibuni.
Kabla ya kufanya mazoezi pima mapigo yako ya moyo na kama yako zaidi ya 100 kwa dakika katika hali ya kupumzika, usifanye mazoezi na badala yake nenda kamuone daktari kwa ushauri wa kitabibu.
Kama mapigo ya moyo yatakuwa sawa kabla ya mazoezi, unatakiwa kupima tena baada ya mazoezi mepesi na kuona kuwa mapigo ya moyo yanarudi katika hali ya kawaida ndani ya dakika kumi baada ya kusimamisha mazoezi.
Usifanye mazoezi muda mfupi baada ya kula. Subiri angalau zipite dakika 90 ndipo ufanye mazoezi. Ili kupata faida zaidi, fanya mazoezi unayoyapenda, yanayokufurahisha na yasiyo kupotezea mapato yako.

Mazoezi ni nini?
Mzoezi siyoi lazima kwenda kwenye vituo maalumu vya mazoezi. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa jambo lolote ambalo mtu atafanya kwa kuushughulisha mwili wake kwa kusababisha viungo vifanye kazi na hata kumsababishia atoke jasho linatafsiriwa kuwa ni sehemu ya mazoezi.

Kwa sababu hiyo wanayataja baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuwa sehemu ya mazoezi kuwa ni kazi za kutoa jasho, kutembea, kukimbia kukimbia, michezo au mazoezi kulingana na wataalamu.

Baadhi ya mambo ambayo watu wanafanya na ikawa ni sehemu ya mazoezi ni kama vile kuendesha baskeli, kutembea, kulima pamoja na kazi nyingine zinazotoa jasho.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanashauri wenye matatizo ya moyo wanapaswa kufanya mazoezi kwa maelekezo na usimamizi wa mtaalamu wa afya mwenye taaluma kuhusu magonjwa ya moyo.

Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuamukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maoni au maswali tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam au tjncdf@gmail.com

Author:

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Post a Comment

 
Copyright ©2016 NCHI YANGU • All Rights Reserved.
Template Design by AT Creatives • Powered by Blogger