Mwandishi wetu, TJNCDF
TAFITI mbalimbali za hapa nchini zinaonyesha kuwa watu wengi wanaougua
saratani huwa hawajifahamu hadi hali zao zinapokuwa mbaya.
Taarifa ya Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) inaeleza
wagonjwa wengi hufikishwa katika hospitali hiyo wakiwa katika hali mbaya na
wengine huwa ni vigumu kupona.
Wanaeleza ya kuwa ni ukweli kwamba saratani nyingi zinaweza kutibiwa
kirahisi iwapo mgonjwa atawahi kupata matibabu.
Hii ndiyo kusema elimu ya ugonjwa huo ni ya msingi sana katika kuwafanya
watu wawahi hospitali mapema wanapoona dalili za saratani.
Kulingana na wataalamu wa afya, saratani ni ugonjwa unaosababishwa na seli
za eneo fulani la mwili kubadili tabia na kuzaliana kwa kasi bila mpangilio na
kuathiri utendaji wa mwili.
Zipo saratani za aina nyingi na kila moja ina dalili zake. Mfano ni
saratani ya koo, ubongo, damu, kibofu cha mkojo, shingo ya kizazi, matiti na
ngozi.
Takwimu za ORCI zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani
wanaofika kutibiwa inaongezeka kila mwaka.
Taarifa za serikali zinaeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoendelea zinazoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani za njia ya
mfumo wa chakula na ini, ikilinganishwa na nchi nyingine.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa wastani wa watu 30-35 kwa kila 100,000
hufariki dunia kila mwaka kutokana na saratani ya mfumo wa chakula, koo na ini.
Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2010,
ilibainika kuwa miongoni mwa sababu za ongezeko la saratani hapa nchini ni
pamoja na mtindo wa maisha usiofaa.
Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na mdomo
zinasababishwa na mtindo wa kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo.
Utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Environmental Care ya jijini
Dar-es-Salaam mwaka 2013, ulibaini kuwa tatizo la matumizi ya vipodozi
visivyofaa pia huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa ikiwa ni pamoja
na saratani ya ngozi.
“Hadi sasa asilimia 52 ya Watanzania wanatumia mkorogo, matokeo yake wengi
wameathirika na wanashindwa kuacha. Wengi wa watu wanaotumia kwa wingi vipodozi
vyenye sumu ni wanawake,” anasema Euphrasia Shayo, Meneja mradi wa kupambana na
vipodozi vyenye sumu katika Shirika la Envirocare.
Saratani si kwamba huwapata watu wazima pekee, bali hata watoto, na katika
nchi nyingi saratani ni chanzo kikubwa cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri
kati ya miaka mitano na 14.
Takribani asilimia 50 ya watu wanaopata saratani katika nchi zinazoendelea
ni wale wenye umri chini ya miaka 65.
Ripoti ya Shirika la Afya Duniani inaeleza kuwa asilimia 30 ya vifo vyote
vitokanavyo na saratani husababishwa na mambo matano.
Mambo hayo yanatajwa kuwa ni unene wa kupindukia, ulaji usiofaa hasa
kutokupata matunda na mboga kwa wingi, kutokufanya mazoezi, utumiaji wa tumbaku
na unywaji wa pombe.
Mambo mengine yanayochangia ongezeko la saratani hasa katika nchi
zinazoendelea ni pamoja na matumizi ya vifaa vinavyotoa mionzi mikali na sumu
ya ‘aflatoxin’ inayopatikana katika nafaka zilizovunda wakati wa kuhifadhiwa.
Mambo mengine yanayosababisha saratani ni uchafuzi wa mazingira ya hewa kwa
moshi wa tumbaku na wa mabaki ya plastiki.
Vile vile vitu vingine vinavyochochea saratani ni maambukizi ya magonjwa
kama vile Virusi Vya Ukimwi (VVU), virusi vya homa ya ini, virusi
vinavyosababisha asilimia 90 au zaidi ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) na
virusi vya Epstein Barr vinavyosababisha saratani ya uvumbe wa taya kwa watoto.
Utafiti wa Dk Catherine de Martel na wenzake uliochapishwa mwaka 2012
katika jarida la The Lancet Oncology, unaonyesha kuwa katika nchi zilizoko
Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 32.7 ya saratani zote hutokana na maambukizi
ya vimelea vya magonjwa.
Vimelea vingine ni Helicobacter pylori wanaosababisha vidonda vya tumbo na
wadudu wa kichocho wanaosababisha saratani ya kibofu cha mkojo.
Kwa wanaume saratani zinazoongoza ni ya mapafu, saratani ya ngozi (Kaposi’s
sarcoma), saratani ya tezi dume na saratani ya tumbo la chakula.
Kwa upande wa wanawake saratani zinazoongoza ni za mlango wa kizazi,
ikifuatiwa na ya matiti na ya utumbo.
Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania, Nsachris Mwamaja
anaelezea juu ya gharama za matibabu ya saratani:
“Pale Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), wagonjwa wanaotibiwa bure
ni wengi na tiba yao inagharimu fedha nyingi. Kwa mfano mgonjwa mmoja wa
saratani huweza kutibiwa kwa Sh. milioni 2. Ndiyo maana kuna changamoto kubwa
katika swala hili.”
Wachunguzi wengine wa masuala ya tiba wanasema kuwa, kuna dawa nyingine za
saratani ya damu inayowapata watoto zinazogharimu Sh milioni moja mfano dawa
aina ya Asparaginase.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari
Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana
na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au
ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam au tjncdf@gmail.com
SHARE
No comments:
Post a Comment